Arsene Wenger: Sina wasiwasi wa kufutwa kazi Arsenal

Arsene Wenger

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Arsenal wameshindwa mechi sita kati ya 12 walizocheza 2018

Arsene Wenger amesema hana wasiwasi kuhusu kufutwa kazi Arsenal, hata baada ya klabu hiyo kushindwa mechi sita kati ya 12 walizocheza 2018.

Vijana wa Wenger watakuwa wenyeji wa viongozi wa ligi Manchester City mechi ya Ligi ya Premia mnamo Alhamisi, siku nne baada yao kupokezwa kichapo cha 3-0 katika fainali ya Kombe la Carabao na Manchester City uwanjani Wembley.

Arsenal kwa sasa wamo alama 27 nyuma ya City na alama 10 nyuma ya Tottenham walio nafasi ya nne na walio nafasi ya mwisho ya kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Wenger, ambaye amekuwa meneja wa Arsenal tangu 1996, amesema "bado inanishangaza kwamba natakiwa kujibu maswali ya aina hii".

Mfaransa huyo wa miaka 68 alitia saini mktaba mpya wa miaka miwili Mei 2017 baada ya kuwaongoza Arsenal kushinda Kombe la FA mara ya tatu katika miaka minne, ingawa walishindwa kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika miaka 20.

"Nimeukataa ulimwengu wote kuhakikisha naheshimu mikataba yangu," ameongeza.

"Nafasi yangu haininyimi usingizi kwa sasa. Wasiwasi wangu ni jinsi ya kuhakikisha timu inabaki makini na kuwa tayari kwa mechi ya kesho."

Alhamisi, Arsenal watakuwa wakicheza mechi yao moja ambayo hawajacheza wakilinganishwa na Spurs.

Wakishinda, badi watakuwa alama saba nyuma ya wapinzani hao wao wa London kaskazini, na alama tano nyuma ya Chelsea, zikiwa zimesalia mechi 10.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Arsenal walilazwa 3-0 na Manchester City fainali ya Kombe la Carabao Jumapili

Kushinda Europa League ni njia nyingine ambayo Arsenal wanaweza kutumia kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Wamepangiwa kukutana na AC Milan katika hatua ya muondoano.

Wenger amekuwa akikosolewa sana misimu ya karibuni na kutakiwa ajiuzulu.

Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Ian Wright alisema kwa sasa hakuna sababu yoyote ya kumfanya Mfaransa huyo kusalia klabu hiyo baada ya mwisho wa msimu huu.

Lakini Wenger kwa mara nyingine alishutumu wanaouliza maswali kuhusu kuwepo kwake Arsenal.

"Kazi yangu ni kuangazia matokeo na ni jukumu la watu wengine kunihukumu na kupima uwezo wangu," amesema.

"Huwa mnakosa usingizi kwamba nina uhakika au sina uhakika kuhusu kazi yangu? Mechi hiyo ya Alhamisi ndiyo muhimu zaidi."

"Haiwezekani kila wakati kushinda mechi. Ni lazima tuishi kukosolewa, ni sehemu ya mchezo huu siku hizi. Lakini lazima tuangazie mechi ijayo, na kujibu wakosoaji wetu kwa umoja."