Wenger kuhusu Arsenal kushindwa na Manchester City tena: Tulishindwa na timu bora zaidi kwa sasa

Arsene Wenger Haki miliki ya picha Reuters

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amesema klabu hiyo ilishindwa na klabu iliyo bora zaidi kwa sasa Uingereza baada yao kulazwa 3-0 kwa mara ya pili katika kipindi cha wiki moja na Manchester City Alhamisi.

Gunners walikuwa wamelazwa 3-0 na City katika fainali ya Kombe la Carabao Jumapili.

Mechi ya Ligi ya Premia kati ya timu hizo mbili iliyochezwa Alhamisi iliamuliwa katika dakika 33 za kwanza kutokana na mabao ya Bernardo Silva, David Silva na Leroy Sane.

Gunners walipoteza nafasi ya kukomboa bao moja kipindi cha pili pale mchezaji waliyemnunua £56m, Pierre-Emerick Aubameyang, aliposhindwa kufunga mkwaju wa penalti kipindi cha pili.

"Nahisi kwamba tulijizatiti sana usiku wa leo," Wenger aliambia BBC.

"Tulicheza tukiwa kiwango chetu cha kujiamini kikiwa chini. Ungeona hili tangu mwanzoni mwa mechi, na tuliadhibiwa."

"Tulihitaji mkwaju huo wa penalti uingie, lakini hilo lilikuwa jambo jingine la kusikitisha. Tulishindwa na timu iliyo bora zaidi nchini kwa sasa."

Kuhusu kutojitokeza kwa wingi kwa mashabiki wa Arsenal uwanjani, alisema: "Hauwezi kutarajia kitu tofauti hasa baada ya kilichotokea Jumapili, na tena leo usiku. Hali ya hewa ilichangia pia."

Haki miliki ya picha Getty Images
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Pierre-Emerick Aubameyang amefungia Arsenal bao moja pekee mechi zake za kwanza nne alizochezea Arsenal
Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waliojitokeza walikuwa 58,420 kwa mujibu wa takwimu, ingawa idadi halisi ya mashabiki uwanjani ilionekana ndogo

Mwandishi wa BBC Phil McNulty anasema kuna dalili kwamba mwisho wa Wenger katika klabu ya Arsenal unakaribia.

Arsenal hawajashinda ligi tangu msimu wa 2003-04.

McNulty anasema: "Itakuwa siku ya huzuni Wenger atakapoondoka Arsenal - lakini ni siku ambayo haiwezi kuepukika kwa muda zaidi."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Baadhi ya mashabiki wa Arsenal waliojitokeza walibeba mabango ya kumtaka Wenger ajiuzulu

Takwimu zinazoonesha masaibu ya Arsenal

  • Gunners sasa wameshindwa mechi nyingi zaidi mashindano yote 2018 kuliko klabu nyingine zote zinazocheza Ligi ya Premia (7).
  • Arsenal wamepokezwa kichapo kinachofanana na vichapo vikubwa zaidi walivyowahi kupigwa nyumbani Ligi ya Premia, ambapo walishindwa kwa magoli matatu na Coventry (1993), Middlesbrough (2001) na Chelsea (mara mbili 2009).
  • Ushindi wa Alhamisi Manchester City ulikuwa mkubwa zaidi wa City ugenini dhidi ya Arsenal katika mashindano yote tangu ushindi wao wa 4-0 Novemba 1912.
  • Arsenal sasa wameenda muda mrefu zaidi Ligi ya Premia bila kukosa kufungwa (mechi 10) tangu Februari 2002 (mechi 11).
  • Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kufungwa mabao matatu kipindi cha kwanza Ligi ya Premia na mara yao ya kwanza kwao kufanya hivyo mechi ya ligi nyumbani tangu Machi 1989 walipofungwa na Nottingham Forest.

Wenger, ambaye amekuwa meneja wa Arsenal tangu 1996, alipoulizwa kuhusu hatima yake mapema wiki hii alisema "bado inanishangaza kwamba natakiwa kujibu maswali ya aina hii".

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry amesema angependa kuwa meneja wa klabu hiyo

Mfaransa huyo wa miaka 68 alitia saini mktaba mpya wa miaka miwili Mei 2017 baada ya kuwaongoza Arsenal kushinda Kombe la FA mara ya tatu katika miaka minne, ingawa walishindwa kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika miaka 20.

Wenger amekuwa akikosolewa sana misimu ya karibuni na kutakiwa ajiuzulu.

Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Ian Wright alisema kwa sasa hakuna sababu yoyote ya kumfanya Mfaransa huyo kusalia klabu hiyo baada ya mwisho wa msimu huu.

Mada zinazohusiana