Wenger asema matatizo hayadumu milele maishani baada ya Arsenal kulaza AC Milan 2-0 Europa League

Arsenal manager Arsene Wenger Haki miliki ya picha Getty Images

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger alifananisha klabu yake na bondia ambaye anajikakamua kuinuka baada ya kupigwa kondena kuangushwa ulingoni na jinsi klabu hiyo ilivyojikwamua na kulaza AC Milan 2-0 katika Europa League baada ya msururu wa matokeo mabaya.

Wenger alisema pia kwamba matatizo hayadumu.

Arsenal walikuwa wanakabiliwa na uwezekano wa kushindwa mara ya tano mtawalia wka mara ya kwanza tangu 1977 walipoandikisha ushindi huo wa kuvutia uwanjani San Siro.

Mabao kutoka kwa Henrikh Mkhitaryan - aliyetawazwa mchezaji bora wa mechi - na Aaron Ramsey yaliwaweka vijana hao wa Wenger katika nafasi nzuri ya kufika robo fainali katika ligi hiyo ndogo ya klabu Ulaya.

"Ni ushindi muhimu sana kwa sababu tulikuwa na wiki ya masaibu," alisema Wenger.

Gunners walikuwa wamecharazwa na Brighton katika Ligi ya Premia Jumapili, baada ya kulazwa mara mbili mfululizo 3-0 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi uwanjani Wembley na katika Ligi ya Premia.

Aidha, walikuwa wamelazwa pia 2-1 na wanyonge wa Sweden Ostersunds FK, ambapo walinusurika kutokana na ushindi wao mkubwa mechi ya kwanza na kusonga hadi hatua ya 16 bora ambapo walipangwa kucheza na Milan.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Arsenal wakisherehekea ushindi wao wa kwanza tangu walipowalaza Ostersunds mwezi uliopita

Mashabiki wa klabu hiyo wameendelea kumshutumu Wenger, huku asilimia 88 ya wanachama wa Wakfu wa Mashabiki wa Arsenal (AST) ambao una wanachama wakipiga kura mapema wiki hii kuunga mkono mkataba wa Mfaransa huyo mwenye miaka 68 utamatishwe mwisho wa msimu.

Hii ina maana kwamba Arsenal walifika San Siro uungwaji mkono wa Wenger ukiwa chini sana katika miaka 22 ambayo ameongoza klabu hiyo.

Lakini walicheza kwa ustadi mkubwa saa na kuwaonjesha Wataliano kichapo cha kwanza kabisa katika mechi 13.

"Unapokuwa na masikitiko makubwa huwa unasahau upesi kwamba una sifa fulani nzuri. Katika kipindi cha wiki moja, haugeuki na kuwa timu baya au mchezaji mbaya. Hakuna linalodumu milele maishani," amesema Wenger.

"Unapoangushwa inakuwa kidogo ni kama katika mchezo wa masumbwi ambapo unakuwa umeangushwa na mchezaji chini, hauna muda wa kutosha wa kuinuka na kujikwamua na unapokezwa konde jingine. Hilo lilitutendekea.

"Lakini inafika wakati fulani ambapo unajua ni lazima uchukue hatua. Sifa zako na hamu yako ya kutaka kuonyesha ustadi ni lazima vionekane katika mchezo."

'Wachezaji wasifu uchezaji wa Arsenal'

Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Mesut Ozil anaamini walicheza vyema zaidi ugenini wakicheza dhidi Milan
Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Aaron Ramsey aliyefunga bao la pili pia alifurahishwa na uchezaji wa timu hiyo
Haki miliki ya picha Twitter
Image caption Kipa David Ospina alifurahia kutofungwa

Mada zinazohusiana