Mwakyembe: Haiwezekani tena Tanzania iambulie patupu michezo ya Jumuiya ya Madola

Wanariadha wa Tanzania wakishiriki mazoezi
Image caption Wanariadha wa Tanzania wakishiriki mazoezi

Tanzania itawakilishwa kwenye michezo ya riadha, ndondi, kuogelea na tenisi ya meza katika mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika mjini Gold Coast, Australia, kuanzia Aprili tarehe 4-15.

Swali ambalo kila Mtanzania anajiuliza: je mwaka huu wawakilishi wa taifa hilo watasafari kama watalii warudi nyumbani mikono mitupu kama ilivyofanyika katika michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka wa 2010 na 2014?

Waziri anayehusika na michezo Harrison Mwakyembe anasema haiwezekani tena Tanzania iambulie patupu mjini Gold Coast.

"Watanzania tuna hasira kukosa medali hata moja michezo iliyopita, kwa hiyo nawahakikishia nyote mwaka huu hatutakosa medali kama mbili ama tatu hivi,'' anasema Mwakyembe katika mazungumzo yake na BBC Swahili mkoani Dodoma.

"Hata miaka ambayo tulipokua tunashinda medali, dhahabu moja na zingine mbili ama tatu zilikua zatosha. Kama ni maandalizi tuko sawa kabisa kwani wanamichezo wetu hasa wanariadha wameshiriki mashindano mbali mbali ya kimataifa.''

Kufikia sasa Tanzania imezoa jumla ya medali 21 katika michezo ya Jumuiya ya Madola. Wameshinda dhahabu sita, fedha sita na shaba tisa.

Image caption Bw Mwakyembe

Mwaka wa 1982 huko Brisbane, Australia, ndiyo Tanzania ilinawiri zaidi kwenye michezo hii ilipomaliza katika nafasi ya 12 na dhahabu moja fedha mbili na shaba mbili.

Gidamis Shahanga ndiye aliyeipatia Tanzania dhahabu hiyo moja aliposhinda mbio za mita elfu kumi.

Zakaria Barie (mbio za mita elfu kumi) na Juma Ikangaa (mbio za marathon) waliipatia Tanzania medali za fedha na za shaba zikapatikana kupitia mrushaji mkuki Zakayo Malekwa na bondia Willy Isangura uzani wa heavy.

"Kwa kweli miaka ya sabuini na themanini tulikua juu sana, wanariadha kama Gidamis Shihanga, Juma Ikangaa na Filbert Bayi walituweka juu,'' anasema waziri.

"Tumepitia milima na mabonde lakini sasa Tanzania tunarudi kwa sababu tumehakikisha michezo ya shule za msingi na sekondari tunaipa umuhimu wake. Hapo ndio kuna vipaji.''

Waziri anasema atatilia maanani sana mchezo wa ndondi mwaka huu kwa sababu ni mchezo ambao umeiletea Tanzania sifa kubwa. Miongoni mwa mabondia ambao wameiweka Tanzani juu ni Emmanuel Mlundwa, marehemu Titus Simba, Willy Isangura na Habibu Kinyogoli.

"Mlundwa huyu tumecheza naye ndondi tukiwa shuleni Tabora lakini mimi sikjuendelea kwa sababu mwalimu wangu alitaka tuvunje mfupa wa katikati ya pua langu ndio nisitoe damu, nikaona hapana wacha kina Mlundwa waendelee.''

Waziri anasema mwaka jana alijaribu awezavyo kulainisha kandanda na usimamizi wake, na anafurahi kwa sasa mambo yako sawa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii