Barcelona yawaondoa Chelsea kwenye michuano ya UEFA kwa kuwacharaza 3-0

Ousmane Dembele na Messi wakishangilia
Image caption Ousmane Dembele na Messi wakishangilia

Chelsea wametupwa nje ya michuano ya klabu bingwa Ulaya katika hatua ya 16 bora, baada ya kupokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Barcelona.

Kufuatia suluhu ya goli 1-1 katika mchezo wa awali, Chelsea walianza kufungwa na Lionel Messi ambaye alikuwa mchezaji bora kwenye mtanange huo hii ikiwa ni dakika ya 3 tokea kuanza kwa mchezo.

Mlinda mlango wa Chelsea Thibaut Courtois hakuwa katika kiwango bora kwenye mchezo huo na kushuhudiwa kuruhusu magoli mepesi.

Image caption Messi amefikisha magoli 100 kwenye michuano ya UEFA

Dakika ya 20 Ousmane Dembele akaiandikia Barca goli la pili kufuatia pasi safi ya Messi baada ya kiungo wa zamani wa Barcelona Cesc Fabregas kupoteza mpira aliokuwa akiumiliki.

Messi ambaye aling'ara vilivyo kwenye mchezo huo, akicheza anavyotaka, aliiandikia tena Barcelona goli ya tatu dakika ya 63.

Ilishuhudiwa pia mkwaju wa Marcos Alonso ukigonga mwamba baada ya kupiga mkwaju wa adhabu nje kidogo ya eneo la hatari la Barcelona.

Alsonso pia alinyimwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mlinzi kisiki wa Barcelona Gerard Pique.

Kwa sasa Barcelona wanaungana na Real Madrid pamoja na Sevilla katika droo itakayofanyika Ijumaa.

Kwa upande wa Chelsea wanaungana na Manchester United pamoja na Tottenham kuyaaga mashindano hayo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii