Europa League: Arsene Wenger hataki Arsenal wapangwe kukutana na Atletico Madrid

Arsene Wenger Haki miliki ya picha Reuters

Menaja wa Arsenal Arsene Wenger amesema angependa sana Arsenal wasipangwe kukutana na Atletico Madrid ya Uhispania katika ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.

Hii ni baada ya Gunners kulaza AC Milan ya Italia 3-1 (Jumla 5-1) katika hatua ya 16 bora.

Atletico Madrid wamekuwa wakicheza vizuri na walifika robofainali Europa League baada ya kuwalaza Lokomotiv Moscow 5-1 mechi ya marudiano.

Nyota wa zamani wa Liverpool na Chelsea Fernando Torres alifunga mabao mawili nao Angel Correa, Saul Niguez na Antoine Griezmann wakafunga moja kila mmoja Alhamisi na kuwawezesha Atletico kupata ushindi wa jumla wa 8-1.

Atletico wameshinda Europa League mara mbili na walifika fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara mbili 2014 na 2016 - walishindwa mara zote mbili.

Mabao ya Arsenal yalifungwa na Danny Welbeck (mawili) na Granit Xhaka naye Hakan Calhanoglu akawafungia Milan bao la kufutia machozi Alhamisi.

"Bila shaka tungependa kuwakwepa Atletico Madrid," alisema Wenger.

Hata hivyo, alisema hana usemi wowote na wakikabidhiwa klabu hiyo hawatakuwa na budi ila kukutana nao.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Fernando Torres na Antoine Griezmann

Droo ya robofainali - ambapo kuna klabu nane kutoka mataifa manane - itafanyika leo Ijumaa saa 12:00 GMT.

Huu ulikuwa ushindi wa tatu wa Arsenal katika kipindi cha wiki moja baada ya kuwalaza Milan 2-0 mechi ya kwanza mjini Milan na pia wakalza Watford 3-0 Ligi ya Premia Jumapili.

Lakini kabla ya ushindi huo San Siro, walikuwa wameshindwa mechi nne mtawalia mashindano yote - mara mbili ikiwa mikononi mwa Manchester City.

"Mambo ni mazuri sana leo. Tulihitaji kujikwamua kutoka kwa matokeo yetu," Wenger alisema.

"Inaonesha jinsi timu ilivyochukua hatua. Tulikuwa na mechi ngumu lakini mwishowe tulishinda. Tukiwa na matokeo mazuri na jinsi tunavyocheza soka, mashabiki watatuunga mkono."

Waliotinga robofainali
Arsenal, Atletico Madrid, CSKA Moscow, Lazio, Marseille, RB Leipzig, RB Salzburg na Sporting Lisbon.
Droo itafanyika Nyon, Uswizi saa 12:00 GMT mnamo Ijumaa

"Ilikuwa mechi wazi. Tulicheza kwa kurejesha mpira nyuma mara nyingi zaidi kipindi cha kwanza kujilinda na kujaribu kutetea matokeo ya mechi ya kwanza. Tulicheza dhidi ya timu nzuri sana," alisema Wenger.

"Ni lazima tujiimarishe katika safu ya ulinzi, lakini kwa jumla yetu ni timu yenye ustadi kiufundi ambayo zaidi huangazia kushambulia.

"Huwa twatatizika zaidi wakati tunahitajika kujilinda. Tulimaliza mechi hiyo tukiwa imara zaidi."

Haki miliki ya picha PA
Image caption Danny Welbeck alianguka baada ya kukabiliwa na Ricardo Rodriguez

Bao alilofunga Welbeck kupitia mkwaju wa penalti lilizua utata kwani Welbeck alionekana kuguswa tu kidogo kabla ya kuanguka na mwamuzi kuwapa Arsenal penalti.

Wenger alisema angetoa jibu baada ya kutazama tena tukio hilo.

Lakini meneja wa AC Milan Gennaro Gattuso alisisitiza kwamba haikufaa kuwa penalti.

"Kwa njia sawa ambapo mchezaji anaweza kufanya kosa, mwamuzi anaweza kufanya kosa," alisema.

"Hata mimi mwenyewe nilipokuwa mchezaji, ningejaribu kufaidi kutokana na nafasi kama hizo. Sitatoa hukumu kuhusu hilo."

Kiungo wa kati wa zamani wa England Jermaine Jenas aliambia BT Sport kwamba ni wazi Welbeck alijiangusha.

"Hilo linatia kasoro matokeo hayo kidogo. Ni Wenger mwenyewe aliyesema kwamba wachezaji wa England wameanza kuzidi katika kujiangusha; ilikuwa ni mmoja wa wachezaji wake leo."

Ushindi huo uliwawezesha Arsenal kufika robofainali katika michuano mikuu ya klabu Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2010.

Wakati huo waliondolewa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na Barcelona kwa matokeo ya jumla ya 6-3.

Ikizingatiwa kwamba Arsenal wamo alama 12 kutoka eneo la kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika Ligi ya Premia, ushindi Europa League inaonekana kuwa njia yao pekee kwa sasa kwao kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Haki miliki ya picha Twitter

Nini kitafuata?

Arsenal watapumzika wiki mbili kabla ya kurejea dhidi ya Stoke City Ligi ya Premia uwanjani Emirates mnamo 1 April (13:30 GMT).

AC Milan watarudi kusaka ushindi wao wa tano mtawalia wa ligi ya Serie A watakapokuwa wenyeji wa Chievo Jumapili (14:00 GMT).

Mada zinazohusiana