Veronica Mbithe: Bondia wa Kenya aamua heri jeshi kuliko Michezo ya Jumuiya ya Madola

Veronica Mbithe

Bondia wa Kenya Veronica Mbithe amejiondoa kwa timu ya taifa ya ndondi itakayoshiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mwezi ujao mjini Gold Coast, Australia.

Mbithe ameajiriwa na Jeshi la Kenya hivyo basi hataweza kusafiri Australia kwa sababu mafunzo ya Jeshi yananaanza Machi tarehe 25.

Mbithe anasema haikuwa rahisi kuamua kati ya safari ya Gold Coast ama achukue kazi ya Jeshi.

"Makocha wangu, mabondia wenzangu na wazazi wamenishauri ni bora niingie Jeshi kwa sababu hapo nitakuwa na mshahara wa kila mwezi," anasema Mbithe ambaye angeiwakilisha Kenya katika uzani wa light-fly kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola.

Amejaribu kila njia kuwashawishi wakuu wa Jeshi wampe ruhusa kushiriki michezo ya Gold Coast lakini wakamweleza haiwezekani.

"Jeshi wana sheria zao na hawawezi kubalisha. Sasa itabidi niende Eldoret Jumapili kwa mafunzo ya miezi saba.

"Wameniambia nikimaliza mafunzo watanipa muda mwingi wa kufanya mazoezi nitimize ndoto yangu katika ndondi.''

Bi Mbithe ni miongoni mwa mabondia wachache waliowahi kuajiriwa kwenye jeshi la Kenya

"Najua sasa mabondia wengi wanawake watajiunga na ndondi kwa sababu ni mchezo huu umenisaidia nikapata kazi.Wenzangu wa klabu ya Dallas mtaa wa Muthurwa hapa Nairobi wamefurahi tu sana."

Mbithe alianza kucheza ndondi mwaka wa 2014, na mwaka huu mwezi wa Januari akiiwakilisha Kenya kwa mara ya kwanza nchini India katika mashindano ya kimataifa.

Anampongeza sana kocha wake Charles Mukula kwa kumfunza mbinu kabambe za ndondi zilizomwezesha kufanikiwa.

Image caption Mbithe (tatu kulia) ni miongoni mwa mabondia wachache kuajiriwa kwenye jeshi la Kenya

"Mukula amenisaidia sana. Sitamsahau kocha wangu huyu. Ingewezekana apate usaidizi wa vifaa ningefurahi sana kwa sababu shida yetu kubwa ni gloves, kamba, speedballs na vifaa vingine vya ndondi."

Michezo ya Jumuiya ya Madola itafanyika Aprili 4-15.

Timu ya Kenya inaondoka Machi 24.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii