Jose Mourinho: Imekuwa vigumu kwa Manchester United kuwakimbiza Manchester City

Manchester United manager Jose Mourinho

Chanzo cha picha, Reuters

Meneja wa Manchester United Jose Mourinho anaamini kwamba haiwezekani kukimbizana na Manchester City msimu huu huku klabu hiyo ya Etihad ikikaribia kushinda taji la Ligi ya Premia.

City walilaza Everton 3-1 Jumamosi, na hiyo ina maana kwamba watashinda taji kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2013-2014 iwapo watafanikiwa kuwalaza United uwanjani Etihad wikendi ijayo.

United, ambao wanashikilia nafasi ya pili, wana alama 68 baada ya kucheza mechi 31.

Lakini wameachwa nyuma na City kwa alama 16.

"Katika ligi nyingine, tungekuwa bado tunapigania taji," amesema Mourinho.

United wamo mbioni kumaliza ligi wakiwa na alama za juu zaidi Ligi ya Premia kwao tangu msimu walioshinda ligi 2012-13 wakiwa na Sir Alex Ferguson msimu wake wa mwisho kwenye usukani.

Misimu iliyofuata, walimaliza nafasi ya saba, nne, tano na sita.

Alama zao ni sawa na walizokuwa nazo Tottenham msimu uliopita baada ya kucheza mechi 31.

Vijana hao wa Mauricio Pochettino walikuwa wakati huo alama saba pekee nyuma ya viongozi Chelsea.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Sanchez aliwafungia Manchester United bao lao la pili dhidi ya Swansea, bao lake la pili kuwafungia ligini

Lakini baada ya kuondolewa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya hatua ya 16 bora na Sevilla, na kisha kutuhumiwa kwa kucheza mchezo usio wa kuvutia, Mourinho amekosolewa sana msimu wake wa pili akwia kwenye usukani United.

Mreno huyo wa miaka 55 ametetea sana matokeo ya klabu hiyo, na mapema mwezi huu alitoa hotuba ya dakika 12.

Kabla yao kushinda 2-0 nyumbani dhidi ya Swansea Jumamosi, Mourinho alitumia ujumbe wake kwenye ratiba ya mechi kusisitiza tena kwamba United ni "klabu iliyo kwenye mpito".

Baadaye, alitaja rekodi yao ligini na pia kwamba wanacheza nusufainali Kombe la FA dhidi ya Tottenham kama ishara kwamba wameimarika msimu huu.

Chanzo cha picha, PA

"Msimu uliopita, tulishinda vikombe lakini tukamaliza nafasi ya sita ligini," alisema Mourinho ambaye alishinda Kombe la Ligi na Europa League msimu uliopita.

"Tunataka kumaliza wa pili msimu huu na tuna alama 10 zaidi ya msimu uliopita, tumefunga mabao mengi, tumefungwa mabao machache, lakini kuna klabu ambayo imeifanya kuwa vigumu sana kuwakimbiza.

"Tumekuwa na msimu mzuri sana na bado tunacheza Kombe la FA. Tutapigania nafasi yetu huko."