Wenger: Mashabiki wa Arsenal watarudi Alhamisi

Arsene Wenger and Steve Bould

Arsene Wenger anaamini kwamba hali ya klabu hiyo kutofana katika Ligi ya Premia ndiyo iliyochangia mashabiki wa klabu hiyo kutojitokeza kwa wingi wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Stoke Jumapili.

Arsenal walilaza Stoke 3-0.

Gunners walizomewa na mashabiki wakati wa mapumziko uwanjani Emirates, baada ya Aaron Ramsey kugonga mwamba wa goli kwa kombora lake ambayo ilikuwa nafasi pekee kwa Arsenal kupata dakika 45 za kwanza.

Lakini Pierre-Emerick Aubameyang alifunga penalti iliyopatikana kwa njia ya utata, baada Bruno Martins Indi kumchezea visivyo Mesut Ozil, na kuwazawadi bao la kwanza kipindi cha pili.

Mshambuliaji huyo wa Gabon aliongeza la pili kupitia kona iliyopigwa na Ozil.

Aubameyang kisha alikosa kutumia nafasi ambayo ingemuwezesha kupata hat-trick walipopata penalti nyingine baada ya Badou Ndiaye kumsukuma na kumwangusha Alexandre Lacazette.

Alimwachia Lacazette apige mkwaju huo na akafunga.

Arsenal, ambao watakuwa wenyeji wa CSKA Moscow katika ligi ndogo ya klabu Ulaya Europa League Alhamisi, wamesalia alama 13 nje ya eneo la kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya Tottenham kulaza Chelsea 3-1 Jumapili.

Wenger anasema anafahamu ni kwa nini hakukuwa na mashabiki wengi uwanjani Emirates.

Maelezo ya picha,

Pierre-Emerick Aubameyang aliyatoa wakfu mabao yake kwa bibi yake marehemu, ambaye alikuwa amechora jina lake kwa rangi kwenye nywele zake kichwani

"Hii yote inatokana na ukweli kwamba hatupiganii tena kushinda ligi," alisema baada ya mechi hiyo.

Maelezo ya picha,

Pierre-Emerick Aubameyang amefunga mabao matano katika mechi sita za kwanza alizochezea Arsenal katika Ligi ya Premia tangu ajiunge nao

"Watu wanajua kwamba hilo halitabadilika kwa sasa. Watarudi Alhamisi, msiwe na wasiwasi.

"Inaeleweka pia kutokana na ukweli kwamba ni wakati wa Pasaka. Ni kipindi cha sikukuu za familia ambapo watu husafiri na ni jambo ambalo si watu wengi sana hulizingatia katika Ligi ya Premia. Kuna pia hali kwamba tumekuwa na kipindi cha mapumziko ya kimataifa."

Maelezo ya picha,

Arsenal walidhibiti mpira 86.7% dakika tano kabla ya Bruno Martins Indi kumchezea visivyo Mesut Ozil

Maelezo ya picha,

Xherdan Shaqiri alitoa krosi tisa upande wa Stoke, zaidi ya wachezaji wengine wote wa Stoke kwa pamoja

Baada ya mechi dhidi ya CSKA Moscow, Gunners watarejea uwanjani Ligi ya Premia mnamo Jumapili tarehe 8 Aprili watakapokuwa wenyeji wa Southampton. Stoke watakutana na Tottenham Juamamosi 7 Aprili.