Wenger: Nitawakosa sana mashabiki na wachezaji wa Arsenal

Arsene Wenger celebrates one of his team's goals Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wenger akisherehekea Arsenal kufunga dhidi ya Burnley

Arsene Wenger aliaga uwanja aliosaidia kuujenga wa Emirates kwa ushindi, sawa na alivyofanya alipoanza kazi kama meneja wa Arsenal siku 7,876 zilizopita.

Alishuhudia vijana wake akicharaza Burnely 5-0 Jumapili. Alianza kazi 1996 kwa ushindi wa 2-0 Ewood Park dhidi ya Blackburn Rovers.

Matumaini yake ya kuondoka na kikombe msimu wake wa mwisho yalizimwa Alhamisi waliopoondolewa na Atletico Madrid kutoka michuano ya ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League hatua ya nusu fainali.

Jumapili, baada ya ushindi mkubwa wa Arsenal, ulikuwa ni wakati wa kutafakari kuhusu ufanisi wa Wenger katika klabu hiyo aliyoiongoza kwa miaka 22.

Uwanja wa Emirates, mashabiki walibeba mabango ya kumsifu Wenger na kumshukuru. Kulikuwa na bango kubwa lililosema "Merci Arsene" (Asante Arsene) nje ya uwanja kwa Kifaransa. Wenger ni Mfaransa.

Fulana za rangi nyekundu zenye ujumbe sawa na tarehe ziliwekwa kwenye kila kiti kati ya viti vyote 60000 vya uwanja huo.

Wachezaji wa Arsenal na Burnley waliandaa gwaride la heshima kumkaribisha Wenger uwanjani. Meneja wa Burnley Sean Dyche alikuwa miongoni mwa walioandaa gwaride hilo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Arsenal wamefunga mabao 53 ya Ligi ya Premia msimu huu - mabao mengi zaidi tangu 2004/05 (54)

Kumekuwa na kupanda na kushuka na shutuma kutoka kwa mashabiki lakini zaidi wengi waliangazia ufanisi wa mataji matatu ya Ligi ya Premia, pamoja na ufanisi mkubwa wa msimu wa 2003-04 walipomaliza msimu bila kushindwa.

Wenger ameshinda pia vikombe saba vya FA.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wenger alimpatia shabiki mmoja tai yake baada ya kikao cha baada ya mechi

Wakati wa Wenger kuzungumza, kwanza alimtakia uponaji wa haraka mpinzani wake mkuu wa muda mrefu Sir Alex Ferguson.

Wenger alikuwa amepewa zawadi na Sir Alex siku saba zilizopita uwanjani Old Trafford, lakini sasa Sir Alex yupo hospitalini akiwa hali mahututi baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye ubongo wake.

Akihutubu, mashabiki walikaa kimya.

'Nitawakosa sana'

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wenger alikabidhiwa kikombe cha dhahabu kilichopewa klabu hiyo msimu wa 2003-04 baada ya kumaliza msimu bila kushindwa

Wenger, huku bendera kubwa yenye picha yake ikipepea, alizungumza kwa upole na kwa kuonyesha hisia na kusema: "Nitawakosa sana."

Wenger alisemaje?

Baada ya mechi, Wenger alisema: "Haiwezekani kutohisi chochote, labda uwe wewe ni roboti.

"Imekuwa ni miaka 22 ya kujitolea kikamilifu na ya umoja. Kwa jumla, ningependa kuwashukuru yote. Nilikuwa na bahati ya kufanya kazi hii kwa miaka 22 katika klabu moja na nashukuru sana kwa hilo.

"Ni vigumu kutathmini msimu huu kwa yale ambayo timu hii imefanya. Nyumbani umekuwa uchezaji wa kushinda ligi, lakini ugenini uchezaji haujatosha. Tulifika pia fainali Kombe la Ligi na nusu fainali Europa League.

"Mashabiki huenda wakaona mambo yakiwa tofauti msimu ujao, lakini watakuwa na meneja mpya na wanaweza kuendelea na kazi kwani msingi wa kila kitu upo."

Wenger alisema pia kwamba atasalia kuwa shabiki wa Arsenal.

"Mimi ni shabiki zaidi ya yote, na nitasalia kuwa shabiki," alisema.

Shabiki kupewa tai

Shabiki mmoja mtoto alitimiziwa matamanio yake baada ya kukaa adhuhuri yote akiwa ameinua bango bango kubwa lenye ujumbe: "Arsene - unaweza kunipa tai yako?"

Wenger atahitimisha kazi yake Arsenal kwa mechi ugenini dhidi ya Huddersfield Town wiki ijayo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mmoja wa wachezaji 83 waliofanikiwa kupanda kutoka kwa akademi hadi kwenye timu kubwa alitawazwa mchezaji bora wa mechi

Wenger: Nataka mashabiki wafurahi

Kabla ya mechi, Wenger alikuwa amesema: "Nilijaribu kujitolea kwa miaka mingi sana, kuwafanya watu wengi wafurahi na natumai kwamba watu wanaopenda klabu hii wataendelea kufurahi siku zijazo na kupata matamanio yao na wanayoyapenda.

"Nimekutana na watu ambao kwao mimi ndiye meneja pekee wa Arsenal wanayemfahamu, kwa hivyo sasa ni fursa nzuri kwa klabu kuwa na watu wapya na mawazo mapya ya kuendelea kusongeza mbele klabu, jambo ambalo ndilo nimejaribu kulifanya maisha yangu yote."

"Arsenal imekuwa klabu ambayo hufanikiwa kuunganisha utamaduni na kupiga hatua. Nilipofika hapa changamtoo kuu ilikuwa kupigisha hatua klabu na kuheshimu utamaduni. Nilipotua, Liverpool na Man United silikuwa ndizo klabu bora zaidi, na zilikuwa na wachezaji wazuri sana. Na hiyo ndiyo changamoto niliyokumbana nayo."

"Ninajivunia kwamba kwa miongoni iliyopita, tulifanikiwa kudumisha utambulisho wa wachezaji wetu. Wachezaji wetu wana uhusiano wa kipekee na klabu. Sehemu ya maisha ya mchezaji na kukumbana na pahala maalum pa kipekee, na hapo ni Arsenal."

Wenger, pia alisema hatachangia kuamua mrithi wake.

"Sihusiki katika kuamua mrithi wangu atakuwa nani, hiyo si kazi yangu, lakini ninachoweza kumwambia ni kwamba anafaa kufanya analofikiria ndilo sahihi kwa klabu. Nimeongozwa na hilo maisha yangu yote hapa."

Takwimu muhimu kuhusu Wenger London kaskazini

  • Hiyo ilikuwa mechi ya 606 kwa Arsenal Wenger na yake ya mwisho nyumbani akisimamia Arsenal (ameshinda 415 sare 120 kushindwa 71). Hiyo ilikuwa mara ya 27 kwa timu yake kushinda kwa mabao matano au zaidi nyumbani.
  • Hakuna meneja aliyesimamia mechi nyingi zaidi nyumbani enzi ya Ligi ya Premia zaidi ya Arsene Wenger (414), ambapo alishinda 286 kati ya hizo. Ni Sir Alex Ferguson anayemzidi kwa kushinda mechi nyingi zaidi Ligi ya Premia (305).
  • Arsenal watamaliza msimu wakiwa wamefunga mabao 54 msimu huu ligini Emirates, ambapo wamefikia rekodi yao ya 2004-05 (54).
  • Sean Dyche alipokezwa kichapo chake cha 50 akiwa meneja Ligi ya Premia, lakini amechapwa mara 11 pekee msimu huu ukilinganisha ma mara 19 mwaka 2014/15 na 20 mwaka 2016-17.
  • Burnley wamefungwa mabao mengi zaidi wakiwa Emirates kuliko uwanja mwingine wowote ule Ligi ya Premia (mabao 13 katika mechi nne).
  • Pierre-Emerick Aubameyang sasa amefunga mabao 20+ ligini katika misimu mitau iliyopita katika ligi kuu za Ulaya (25 msimu 2015-16 na 31 msimu wa 2016/17, akiwa Borussia Dortmund).
  • Aubameyang amefunga mabao saba ligini akichezea Arsenal msimu huu, zaidi kushinda mchezaji yeyote yule wa Arsenal katika mechi za kwanza saba nyumbani Ligi ya Premia.
  • Alexandre Lacazette ameshiriki moja kwa moja katika ufungaji wa mabao tisa katika mechi tisa alizocheza karibuni.

Nini kinafuata?

Arsenal watasafiri Leicester Jumatano nao Burnley wawe wenyeji wa Bournemouth Jumapili.

Mechi ya mwisho ya Arsenal msimu huu itakuwa dhidi ya Huddersfield Town.

Mada zinazohusiana