Mohamed Salah: Nina 'matumaini makubwa' ya kucheza Kombe la Dunia Urusi 2018

Mohamed Salah amefunga magoli 44 kwa msimu huu ndani ya Liverpool
Maelezo ya picha,

Mohamed Salah amefunga magoli 44 kwa msimu huu ndani ya Liverpool

Mshambuliaji wa Liverpool na Misri Mohamed Salah amesema ana uhakika wa kuwepo kwenye michuano ya kombe la dunia baada ya kupata majeraha ya bega kwenye mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.

Salah, 25, aliondoka uwanjani mjini Kiev akiwa analia baada ya kuchezewa rafu na mlinzi wa Real Madrid Sergio Ramos.

''Upendo wenu na kuniunga mkono kwa pamoja vitanipa nguvu ninayoihitaji,'' alisema Salah.

Misri itacheza mchezo wake wa kwanza June 15 dhidi ya Uruguay katika mji wa Yekaterinburg.

Maelezo ya picha,

Tiyari Sergio Ramos ameomba radhi kwa kitendo hicho

Baada ya mchezo wa mjini Kiev, meneja wa Liverpool Jurgen Klopp alisema maumivu aliyoyapata Salah ni makubwa sana.

Lakini chama cha soka cha Misri kilisema matokeo ya vipimo yanaonyesha kuwa Salah hajaumia sana na anaweza kuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa nchini Urusi.

Salah ambaye amefunga magoli 44 kwa klabu yake msimu huu aliangushwa na Ramos dakika ya 26.

Licha ya kutaka kuendelea na mchezo alijikuta akitoka uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Lallana.