French Open: Serena Williams asema vazi lilimfanya kujihisi kama shujaa wa Wakanda

Serena Williams Haki miliki ya picha Rex Features

Serena Williams amesema alijihisi kama "shujaa" alipovalia vazi lake jeusi la kubana mwili wakati wa mchezo wake mkubwa wa kwanza wa ushindani alipocheza katika French Open.

Williams alipata ushindi wa 7-6 (7-4) 6-4 dhidi ya Kristyna Pliskova.

Kulikuwa na joto kali lililofikia 25C jijini Parislakini hilo halikumzuia mshindi huyo mara 23 wa mashindano makubwa ya tenisi duniani kushiriki mchezo wake wa kwanza wa Grand Slam tangu Septemba mwaka jana.

"Najihisi kama shujaa nikiwa na vazi hili, kama malkia kutoka Wakanda [akirejelea filamu ya Black Panther] pengine," alisema.

"Ni vazi lisilosumbua ukilivaa."

Mchezaji huyo wa miaka 36 aliongeza: "Daima nimekuwa nikiishi maisha ya ndoto. Nilitaka kuwa shujaa, na hii kwa kiasi fulani ndiyo njia yangu ya kuwa shujaa."

Williams pia alisema vazi hilo lilimsaidia kukabiliana na tatizo la kuganda kwa damu kwenye mishipa yake, tatizo alilofichua kwamba limekuwa likimtatiza Februari.

Alisema tatizo hilo lilitishia maisha yake.

"Nilikuwa na shida nyingi sana kutokana nazo - sijui damu yangu ilikuwa imeganda mara ngapi kwenye mishipa kipindi cha miezi 12 iliyopita,2 alisema.

"Bila shaka, vazi hili lina kazi nyingine pia.

"Ni vazi la kupendeza na kuvutia, lakini pia lina manufaa hayo maalum hivyo ninaweza kucheza bila shida yoyote."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Serena Williams alirejea kucheza tenisi miezi sita baada yake kujifungua mtoto wake wa kwanza

Mchezo huo kati ya wachezaji hao wawli hatari kwa kurusha mpira - ambao walirusha mpira mara 28 kati yao - ilikuwa ya ushindani wa karibu sana lakini Williams aliibuka kidedea.

Bingwa huyo mara tatu wa French Open atakutana sana na Ashleigh Barty wa Australia raundi ijayo.

Williams, aliyerejea kucheza tenisi Machi, aliulizwa kuhusu uwezekano wake wa kushinda mashindano hayo ambayo yanafanyika Roland Garros, michuano ambayo alishinda mara ya mwisho 2015.

Alisema: "Sijui. Lakini bila shaka niko hapa kushindana na nitafanya kila niwezalo.

"Sijiwekei presha yoyote kama inavyokuwa kawaida kwangu kufanya."

Mmarekani huyo alipoulizwa iwapo -ameshuhudia mabadiliko yoyote akicheza Grand Slam baada yake kuwa mzazi, alisema: "Tofauti kuu ni kwamba naharakisha kiasi leo. Ni kwa sababu nataka kufika nyumbani kumuona [binti wangu] Olympia, kwa sababu nimekuwa hapa siku yote.

"Kulitokea kucheleweshwa kidogo kutokana na mvua kwa hivyo sikuweza kumuona. Iwapo mimi sifanyi mazoezi, huwa tuko pamoja.

"Nina wasiwasi kuhusu jinsi hilo litafanikishwa kwangu, kwa sababu kawaida katika Grand Slam huwa natumia muda mwingi sana uwanjani. Yeye bado mdogo sana, kwa hivyo huwa siji naye uwanjani."

Haki miliki ya picha Saj Chowdhury

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii