Kombe la Dunia Urusi 2018: Neymar arejea na kufungia Brazil baada ya kuuguza jeraha

Neymar celebrates Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Neymar sasa amefunga mabao 54 katika mechi 83 alizochezea Brazil

Neymar alifunga bao mechi yake ya kwanza baada ya kurejea kutoka kuuguza jeraha alipowachezea Brazil mechi ya kujiandaa kwa Kombe la Dunia dhidi ya Croatia uwanjani Anfield, Uingereza.

Brazil walishinda 2-0.

Nyota huyo wa Paris St-Germain mwenye miaka 26 alitoa kombora lililogonga mwamba wa goli kabla ya kutumbukia ndani, baada ya uchezaji mzuri uliowashirikisha Willian wa Chelsea na Philippe Coutinho wa Brazil.

Croatia walikuwa wamecheza mchezo wa kasi sana kipindi cha kwanza na kuunda nafasi za kufunga kupitia Dejan Lovren na Andrej Kramaric.

Lakini mchezaji wa Liverpool Roberto Firmino alifunga muda wa ziada na kukamilisha ushindi wa Brazil.

Brazil, ambao walikuwa timu ya kwanza kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi Machi, watakutana na Austria Jumapili kabla ya kuanza kampeni yao Kundi E dhidi ya Uswizi mnamo 17 Juni.

Kurejeakwa Neymar, aliyehamia PSG kutoka Barcelona kwa £200m Agosti mwaka jana, ni nafuu kubwa kwa Brazil.

Alikuwa amekosa kucheza kwa miezi mitatu tangu aumie kwenye kifungo cha mguuni Februari.

Alikosa pia mechi ya mwisho ya Brazil Kombe la Dunia 2014 baada ya kuumia mfupa mgongoni wakati wa mechi ya robofainali ambayo walishinda 2-1 dhidi ya Colombia.

Bila Neymar, Brazil waliaibishwa 7-1 na Ujerumani nusufainali.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Luka Modric na Gabriel Jesus wakikabiliana

Kwa Firmino, ulikuwa ni mchezaji mzuri kwake. Kufikia sasa, mchezaji huyo wa miaka 26 amefunga mabao 15 akicheza Anfield akichezea klabu na taifa tangu kuanza kwa msimu wa 2017/18.

Croatia watapata matumaini kutokana na uchezaji wao mzuri kipindi cha kwanza.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mshambuliaji wa Hoffenheim Kramaric akimkabili beki wa Real Madrid Marcelo

Wachezaji wao wawili waliadhibiwa kipindi hicho, Kramaric kwa kumchezea visivyo Thiago Silva, na Ivan Perisic alipomkabili mchezaji wa Manchester City Gabriel Jesus.

Mameneja wote wawili walifanya mabadiliko ambayo yalipunguza kasi ya mchezo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Brazil wameshinda mechi 16 kati ya 20 walizocheza chini ya Tite

Croatia hata hivyo walionekana kuishiwa na ubunifu hasa baada ya kuingizwa kwa Neymar kipindi cha pili.

Kocha wa Brazil Tite amekiri kwamba alishangazwa na uchezaji mzuri wa Neymar baada yake kukaa nje kipindi kirefu tangu afanyiwe upasuaji Machi.

"Kwa mechi ya kwanza baada ya kurejea kutoka kuuguza jeraha, sikutarajia mengi kutoka kwake. Ningeridhishwa na uchezaji wa hata chini zaidi," alisema.

"Alichokifanya kilikuwa cha ajabu. Neymar ni mchezaji mwenye kipaji adimu lakini bao alilofunga lilitokana na uchezaji, wa pamoja, ulioshirikisha timu yote."

"Anafahamu yale anayoyapata kutoka kwao (wachezaji wenzake)."

Coutinho anaamini Neymar anaweza hata kung'aa zaidi ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo nchini Urusi

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii