Simba ‘wanguruma’ kombe la SportPesa Super Cup Kenya, Yanga na JKU wa Zanzibar hoi

Simba Haki miliki ya picha HISANI/SPORTPESA

Mabingwa wa ligi kuu ya Tanzania Simba wametolewa jasho na Kariobangi Sharks ya Kenya kabla ya kuibuka mshindi kwa mabao 3-2 ya penalti.

Hii ni baada ya sare tasa katika mashindano ya kandanda ya SportPesa Super Cup kwenye uwanja wa Afraha mjini Nakuru eneo la Bonde la Ufa Jumatatu.

Nusra Papa hao wa Kariobangi wameze Simba lakini Jonas Mkude akawapatia mabingwa mara 19 wa ligi kuu ya Tanzania ushindi kwa kufunga bao muhimu lililowawezesha Wekundu wa Msimbazi kufuzu kwa nusu-fainali.

Sasa Simba watakutana na Kakamega Homeboyz ya Kenya Alhamisi wiki hii..

Jumanne AFC Leopards ya Kenya itajitosa uwanjani Afraha kupimana nguvu na Singida FC ya Tanzania.

Endapo Leopards watashinda basi patachimbia Nakuru Alhamisi kwani Leopards watakutana na wapinzani wao wakuu Gor Mahia

Timu zingine ambazo tayari zimefuzu kwa nusu-fainali ni bingwa mtetezi Gor Mahia na Kakamega Homeboyz zote za Kenya.

Tofauti na matarajio ya wengi, Kakamega Homeboyz iliibandua mashindanoni timu kongwe nchini Tanzania Yanga kwa kuipachika mabao 3-1 kwenye mechi ya ufunguzi.

Huwezi kusikiliza tena
Wayne Rooney alivyofunga bao dhidi ya Gor Mahia

Allan Wanga alikuwa nyota wa mechi hiyo kwa kupachika wavuni mabao mawili naye Wycliffe Opondo, ambaye aliingia kipindi cha pili, akaongeza la tatu.

Simon Matheo aliifungia Yanga bao lao la pekee.

Matokeo ya mechi za sasa

  • Kakamega Homeboyz 3-1 Yanga
  • Gor Mahia 3-0 JKU
  • Simba 3-2 Kariobangi Sharks

Mwaka jana Yanga iling'olewa na AFC Leopards ya Kenya kwa mabao ya penalti kwenye nusu-fainali ya mashindano haya ya SportPesa Super Cup yalipofanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Matokeo hayo ni sawa na kumimina pilipili kwenye kidonda kibichi kwani ni hivi karibuni tu mahasimu wakuu wa Yanga, Simba walitwaa taji la ligi kuu ya Tanzania huku mashabiki wa Yanga wakibubujikwa na machozi wengine wakisema hiyo ni hujuma sasa.

Haki miliki ya picha HISANI/SPORTPESA

Kocha wa Kakamega Homeboyz Paul Nkata wa Uganda alikuwa anatembea juu ya keki akisema ana matumaini makubwa ya kufuzu kwa fainali

``Tulikua tumejiandaa vyema kwa mechi hii kwa hivyo huu si ushindi wa bahati tumeufanya kazi lakini sikufurahishwa na kiwango chetu,'' alisema Nkata.

Licha ya kipigo hicho na Kakamega Homeboyz ambayo inashikilia nafasi ya tisa kwenye ligi kuu ya Kenya, kocha wa Yanga Noel Mwandile alijikakamua na kuzungumza na waandishi wa habari.

``Hatukutumia nafasi zetu tulizopata za kufunga lakini tunarudi nyumbani kujipanga upya na mtatuona mwakani kwa mashindano haya,'' alisema Mwandile.

Gor Mahia ilifuzu kwa nusu-fainali kwa kuizaba Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) ya Zanzibar mabao 3-0.

George "Blackberry'' Odhiambo aliipatia Gor Mahia bao la kufungua kinywa dakika ya 29 kisha dakika sita baadae mchezaji kutoka Uganda Godfrey Walusimbi akaongeza la pili huku Medi Kagere akifunga la tatu dakika ya 82.