Loris Karius: Kipa wa Liverpool atumwa kwa madaktari Marekani

Loris Karius Haki miliki ya picha Getty Images

Mlinda lango wa Liverpool Loris Karius alitumwa kwa madaktari wataalamu nchini Marekani baada yake kuwasiliana na klabu hiyo akiwa likizoni Marekani.

Mjerumani huyo mwenye miaka 24 alitembelea hospitali moja Boston, Massachusetts na ikabainika siku tano baada ya fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwamba alikuwa anauguza jeraha la ubongo kutokana na mkitisiko.

Karius alifanya makosa ya kushangaza wakati wa fainali hiyo na kusababisha goli la kwanza na la tatu.

Liverpool walishindwa kwa kuchapwa magoli 3-1 na Real Madrid wakati wa mechi hiyo iliyochezwa 26 Mei.

Dokta Ross Zafonte amesema kuna uwezekano kwamba jeraha hilo liliathiri uchezaji wake.

Kabla yake kufanya kosa lililozalisha goli la kwanza, Karius aligongana na beki wa Uhispania Sergio Ramos.

Lakini katika taarifa iliyotolewa kwa idhini ya mchezaji huyo Mjerumani, madaktari hawajasema iwapo kugongana huko ndiko kulikomsababishia jeraha hilo.

Karius alionekana kutoonesha dalili zozote za kujeruhiwa na hakuomba apewe matibabu wakati wa mechi hiyo iliyochezewa Kiev, Ukraine.

mlinda mlango huyo aligongana na nahodha huyo kipindi cha pili.

Dakika chache baadaye, aliurusha mpira kuelekea kwa mshambuliaji wa Real,Karim Benzema ambaye alikuwa mbele yake.

Benzema aliupiga mpira na kufunga.

Bao la tatu lilifungwa baada ya Karius kutomakinika alipojaribu kuudaka mpira wa kutoka mbali wa Gareth Bale na ukamponyoka kutoka kwenye mikono yake na kutumbukia wavuni.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos alihusika pia katika kuumia kwa mchezaji nyota wa Misri Mohamed Salah
Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Loris Karius aligongana na Sergio Ramos kabla yake kufanya kosa lake la kwanza

Dkt Zafonte, ambaye ni mmoja wa wataalamu wakuu wa majeraha ya kichwa katika ligi ya soka ya Marekani, NFL.

Amesema uchunguzi wa Karius ulifanywa kwa kuangalia pia video ya mechi hiyo, kumpima kichwa chake na kufanya kuzingatia mambo mengine muhimu.

Amesema kuna uwezekano kwamba Karius alikumbwa na 'kuduwaa kwa muda" ambako huathiri uwezo wa mtu kupokea na kuzingatia maelezo kuhusu umbali wa vitu.

Tatizo kama hilo hutokea punde baada ya tukio lililosababisha mtikisiko wa kichwa.

Dkt Zafonte amesema anatarajia Karius atapata nafuu.

Karius, alijiunga na Liverpool kwa £4.75m kutoka Mainz mwaka 2016.

'Mabadiliko yanahitajika'

Punde baada ya kisa hicho, shirika linaloangazia majeraha ya kichwa la Headway limetoa wito kwa sheria kuhusu mtikisiko wa kichwa na majeraha ya ubongo kufanyiwa mageuzi ya haraka.

Kanuni kuhusu majeraha ya kichwa zilianzishwa na Ligi ya Premia na Uefa mwaka 2014 ambao walisema ni madaktari pekee wanaweza kuamua iwapo mchezaji anaweza kuendelea kucheza baada ya tukio linalohofiwa kumjeruhi kichwa mchezaji.

Kanuni za Ligi ya Premia zilibadilishwa baada ya Tottenham kushutumiwa kwa kumruhusu kipa wao Hugo Lloris kuendelea kucheza muda baada ya kupoteza fahamu.

'Itamchukua miezi mitatu hivi kusahau'

Mwanasaikolojia wa michezo Dkt Steve Peters, ambaye amewahi kufanya kazi na timu ya taifa ya England anasema Karius atahitaji muda kuyasahau makosa yake.

"Hii ni michezo na siku moja mambo wakati mwingine huenda mrama. Jambo muhimu zaidi ni kukubali kwamba hajapoteza kipaji chochote au uwezo wowote. Ni makosa kadha tu, kwa hivyo vyema zaidi huwa kukubali ukweli. Huenda asiwahi kurudia makosa hayo tena.

"Kwa kawaida, itamchukua miezi kama mitatu hivi kwake kukubali kwamba hayo yalipita. Hatujui ni kwa sababu gani huchukua muda kama huo - akili huchukua muda kutafakari na kulikubali jambo. Kwa usaidizi wa wataalamu, hili linaweza kufanikiwa hivi kwamba mwishowe unatokea ukiwa hata na nguvu zaidi badala ya kukudhoofisha."

Haki miliki ya picha Getty Images

Kipa wa zamani wa Ray Clemence, aliyeshinda Kombe la Ulaya akiwa na Liverpool kati ya 1977 na 1981, anasema kipindi cha mapumziko ya majira ya joto kitakuwa kirefu sana kwa Karius ambaye hakutajwa kikosi cha Kombe la Dunia cha Ujerumani.

"Alifanya makosa mawili makubwa wakati muhimu kwenye mechi na itamulazimu kuishi na hilo maisha yake yote," kipa huyo wa zamani wa England Clemence aliambia BBC Radio 5.

Mada zinazohusiana