Singida United wajiunga na Simba nusu fainali kombe la SportPesa Super Cup

Mashabiki wa AFC Leopards Haki miliki ya picha SPORTPESA

Klabu ya Singida United ya Tanzania Bara imeishinda AFC Leopards ya Kenya kwa mabao 4-2 ya penalti na kufuzu kwa nusu-fainali ya mashindano ya kandanda ya SportPesa Super Cup katika uwanja wa Afraha mjini Nakuru, Kenya.

Mechi hiyo iliyochezwa Jumanne jioni ilimalizika kwa sare tasa.

Lakini Leopards watajilaumu wenyewe kwani mchezaji wao wa kiungo Whyvonne Isuza alishindwa kufunga penalti katika kipindi cha pili.

Leopards wanajiunga na Yanga ya Tanzania, JKU ya Zanzibar na Kariobangi Sharks ya Kenya ambao tayari wameng'olewa mashindanoni.

Fainali ni Jumapili, na mshindi atasafiri England mwezi ujao kupambana na Everton.

Singida itakutana na bingwa mtetezi Gor Mahia Alhamisi wiki hii kwenye nusu-fainali, huku Simba ikimenyana na Kakamega Homeboyz. Timu mbili za Kenya na Tanzania ndizo zimefuzu kwa nusu-fainali.

Wakati huo huo, mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati kugombania kombe la Rais Kagame yatafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni tarehe 28 hadi Julai tarehe 13.

Haki miliki ya picha SPORTPESA
Image caption Sindinda United wakikabiliana na AFC Leopards

Habari hizi ni kwa mujibu wa katibu wa baraza la kandanda la mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, kwa kifupi Cecafa, Nicholas Musonye. Akihutubia waandishi wa habari Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam, Musonye ametangaza ratiba ya mashindano hayo.

Bingwa mtetezi Azam iko kundi A pamoja na waakilishi wa Uganda, JKU ya Zanzibar na Kator FC ya Sudan Kusini. Mechi ya kwanza ya Azam ni dhidi ya Kator Juni tarehe 29.

Mechi ya kufungua dimba siku hiyo ni kati ya JKU na waakilishi wa Uganda, ya tatu ikiwa ni kati ya Yanga ya Tanzania na Dakadaha ya Somalia. Yanga iko kundi la C na mahasimu wao Simba, St George ya Ethiopia na Dakadaha. Yanga itapambana na Simba Julai tarehe tano mechi za makundi.

Bingwa wa ligi kuu ya Kenya Gor Mahia wako kundi B pamoja na Rayon ya Rwanda, Lydia Ludic ya Burundi na Ports ya Burundi ambayo itacheza mechi ya nne Juni tarehe 30 dhidi ya Lydia Ludic kisha Simba ipambane na Dakadaha.

Mechi za robo-fainali ni tarehe 8 na 9 mwezi ujao na fainali ni tarehe 13.

Mada zinazohusiana