Kombe la Dunia Urusi 2018: Urusi tayari kwa michuano mechi ya kwanza ikiwa Russia v Saudi Arabia

The World Cup 2018 mascot

Chanzo cha picha, Getty Images

Michuano ya Kombe la Dunia ya Fifa ya mwaka 2018 inaanza leo nchini Urusi ambapo Urusi watacheza dhidi ya Saudi Arabia baada ya kufanyika kwa sherehe ya ufunguzi katika uwanja wa Luzhniki, mjini Moscow.

Mechi hiyo itaanza saa kumi na mbili jioni saa za Afrika Mashariki.

Michuano hiyo itashirikisha mataifa 32, wakiwemo mabingwa watetezi Ujerumani, na itakuwa na mechi 64 zitakazochezwa katika kipindi cha siku 32.

Fainali itachezwa 15 Julai.

Fainali za sasa za Kombe la Dunia ambazo ni za 21 zitachezwa katika viwanja 12 katika miji 11 nchini Urusi, ambayo inapatikana eneo la upana wa maili zaidi 1,800.

Kutokana na hili, kutakuwa na tofauti kubwa katika wakati mechi zinachezwa.

Ujerumani, waliowashinda Argentina katika fainali ya Kombe la Dunia 2014, wanapania kuwa taifa la kwanza kushinda kombe hilo mtawalia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1962.

Brazil nao wanatafuta kuweka rekodi nyingine kwa kushinda kombe hilo kwa mara ya sita.

Michuano hiyo ya mwezi mmoja inatarajiwa kuwavutia mashabiki nusu milioni kwenda Urusi na kote duniani inatarajiwa kutazamwa na watu zaidi ya bilioni tatu.

Kuna makundi manane, kila kundi likiwa na timu nne.

Timu mbili ambazo zitamaliza juu kwenye kundi ndizo zitakazosonga hadi hatua ya 16 bora.

Fainali itachezewa katika uwanja wa Luzhniki ambao hutoshea mashabiki 81,000 mnamo 15 Julai.

Nani atashinda Kombe la Dunia?

Mabingwa watetezi Ujerumani, mabingwa mara tano Brazil, washindi wa Euro 2016 Ureno, waliomaliza wa pili 2014 Argentina, Ubelgiji, Poland na washindi wa mwaka 1998 Ufaransa ni timu nane ambazo zilikuwa kwenye chungu wakati wa kufanywa kwa droo.

Wote wanapigiwa upatu kushinda.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ujerumani ndio mabingwa watetezi

Wenyeji Urusi walikuwepo kwenye chungu pia ingawa ndio walioorodheshwa wa chini zaidi kwa viwango vya soka kwa kufuata orodha ya Fifa ya kila mwezi, ambapo kwa sasa wameorodheshwa wa 70.

England, ambao wameshinda mechi moja pekee kati ya nane walizocheza karibuni zaidi Kombe la Dunia hawakuwa kwenye chungu, sawa na mabingwa wa mwaka 2010 Uhispania.

Ujerumani wamefika angalau nusu fainali katika kila michuano minne iliyochezwa karibuni, na baada ya kuwa timu pekee kufuzu kwa kushinda mechi zote Ulaya, wanatarajiwa kutoa ushindani mkali.

Wamo Kundi F na Mexico, Sweden na Korea Kusini.

"Ujerumani watawindwa kama ambavyo haijawahi kutokea awali," anaamini kocha wao Joachim Low.

"Ni sisi pekee, kama mabingwa watetezi, tuna kitu cha kupoteza."

Brazil ndiyo nchi pekee ambayo imeshiriki michuano hiyo bila kukosa tangu ilipoanzishwa lakini hawajashinda tangu 2002.

Mara ya mwisho kwao kushinda wakiwa barani Ulaya ilikuwa ni mwaka 1958.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hata hivyo, Brazil wana matumaini, hasa kupitia nyota wao Neymar aliyeweka rekodi ya dunia kwa kununuliwa £200m alipohamia Paris Saint Germain ya Ufaransa kutoka Barcelona Agosti 2017.

Alikuwa ameumia mapema mwaka huu lakini amepona na kucheza mechi kadha za kirafiki za kimataifa akiwa na Brazil, na kufunga.

Uhispania wana mabingwa kadha wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kutoka Real Madrid kwenye kikosi chao na watatakakutwaa kombe hilo tena kama walivyofanya miaka minane iliyopita, na waliposhinda ubingwa Ulaya 2008 na 2012.

Ronaldo na Messi watafanikiwa?

Upande mwingine, Cristiano Ronaldo naye atakuwa anatafuta medali yake ya kwanza ya kushinda Kombe la Dunia baada ya kuwasaidia Ureno kushinda Euro 2016, Lionel Messi naye akitumai kwamba atashinda kombe lake la kwanza kuu akiwa na Argentina.

Ufaransa wana kikosi kichanga na kilichojaa wachezaji wa kusisimua, akiwemo mshambuliaji wa miaka 19 Kylian Mbappe.

Aidha, wana wachezaji nyota kutoka Ligi ya Premia wakiwemo kipa wa Tottenham Hugo Lloris, kiungo wa kati wa Manchester United Paul Pogba na mshambuliaji wa Chelsea Olivier Giroud.

Walio wageni Kombe la Dunia ni kina nani?

Panama na Iceland watakuwa wanashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Iceland ambalo ni taifa la watu 335,000 pekee ndilo taifa ndogo zaidi linaloshiriki.

Watatumai watarudia ufanisi wao wa miaka miwili iliyopita walipofika robofainali Euro 2016 mara yao ya kwanza kushiriki michuano mikubwa. Walifanya hivyo kwa kuwaaibisha England njiani.

Mechi ya kwanza kwa Iceland nchini Urusi itakuwa dhidi ya Argentina 16 Juni.

Sikukuu ya taifa ilitangazwa Panama baada yao kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Taifa hilo la Amerika ya Kati limeorodheshwa la 55 katika viwango vya soka vya Fifa. Wana mkufunzi mwenye uzoefu mkubwa Hernan Dario Gomez, aliyekuwa na taifa lake la Colombia Kombe la Dunia la 1998 na Ecuador mwaka 2002.

Kuna mataifa kadha pia ambayo yamerejea baada ya kuwa nje kwa muda mrefu.

Misri na Morocco wamerejea baada ya kutoshiriki kwa miaka 28 na 20 mtawalia.

Kuna mataifa yanayofahamika sana kwa soka ambayo hayashiriki.

Mabingwa mara nne Italia, mabingwa wa Amerika ya Kusini Chile na mabingwa wa Africa Cameroon wote hawakufanikiwa kufuzu.

Uholanzi, waliomaliza wa pili mwaka 2010 pia hawakufanikiwa.

Marekani nao wanakosa michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu 1986.

Waamuzi kusaidiwa na VAR

Teknolojia ya kuwasaidia waamuzi (VAR) itatumiwa kwa mara ya kwanza Kombe la Dunia wakati huu.

Teknolojia hiyo itatumiwa kuwasaidia waamuzi kuepuka makosa ambayo yanaweza kusaidia kuamua mshindi wa mechi, hasa wakati wa kukubali goli, mikwaju ya penalti au kadi nyekundu.

VAR tayari imekuwa ikijaribiwa England, Ujerumani na Italia.

Teknolojia hiyo ilitumiwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia la Klabu Desemba 2016 na ikajaribiwa katika Kombe la Mashirikisho 2017.

Maelezo ya picha,

BBC Idhaa ya Kiswahili itatangaza moja kwa moja mechi za michuano hiyo

Usalama

Urusi inapanga kuandaa michuano ya kufana baada ya kuwashinda England, Uhispania na Ureno, na Uholanzi na Ubelgiji, katika kupigania haki za kuwa mwenyeji.

Ni mara ya kwanza Urusi kuandaa michuano hiyo.

Mashabiki karibu 10,000 wa England wanatarajiwa kusafiri Urusi, lakini baadhi huenda wasisafiri kutokana na uhasama uliozidi kati ya nchi hizo mbili na wasiwasi pia kuhusu usalama.

Makabiliano yalitokea kati ya mashabiki wa Urusi na England mataifa hayo yalipokutana Marseille wakati wa Euro 2016.

Ghasia pia zilizuka kati ya mashabiki wa England, Urusi na Ufaransa.

Unaweza kusoma pia: