Kombe la Dunia Urusi 2018: Paka mtabiri anayetaka kumrithi Paul the Octopus atabiri mshindi mechi ya Urusi na Saudi Arabia

Achilles the psychic cat

Chanzo cha picha, Reuters

Paka mmoja maarufu ambaye anadaiwa kuwa na uwezo wa kipekee wa kutabiri ametabiri mshindi wa mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia nchini Urusi.

Kwa mujibu wa paka huyo aliyepewa jina Achilles, Urusi ndio watakaoshinda mechi hiyo.

Achilles, paka wa rangi nyeupe ambaye ni kiziwi, hubashiri mshindi kwa kuchagua moja kati ya bakuli mbili ambazo zimewekwa bendera za mataifa yanayocheza.

Paka huyo ni miongoni mwa paka wanaofugwa kukabiliana na panya katika makumbusho ya Hermitage mjini St Petersburg, ingawa sasa ana majukumu hayo mapya.

Anadaiwa kubashiri kwa ufasaha mshindi wa Kombe la Mashirikisho mwaka 2017.

Paka huyo alitoa utabiri wake wa sasa Jumatano.

Chanzo cha picha, AFP

"Achilles yuko tayari kutumiwa kwa umma na huwa hana wasiwasi kuwa eneo lenye watu wengi," anasema daktari wa mifugo Anna Kondratyeva, ambaye humtunza.

Chanzo cha picha, AFP

Paka huyo anafuata katika nyayo za Paul the Octopus, pweza aliyepata umaarufu sana baada ya kutabiri mshindi wa mechi za Kombe la Dunia mwaka 2010, michuano iliyoandaliwa nchini Urusi.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Paul alikuwa amezaliwa England lakini baadaye akahamishiwa Ujerumani

Alibashiri matokeo ya mechi zote za Ujerumani nchini Afrika Kusini na baadaye ushindi wa Uhispania. Kutokana na kubashiri ushindi wa Uhispania, alipewa uraia wa mji mmoja nchini Uhispania.

Baada ya mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huo pweza Paul alitokea kwenye video akiipigia debe Uingereza kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia 2018.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Paul alitabiri ushindi wa Uhispania mwaka 2010

Hata hivyo, ubashiri wake haukutimia kwani Urusi ndio waliotunukiwa hadhi hiyo.

Paul alifariki Oktoba mwaka 2010 kifo cha kawaida kulingana na hifadhi ya Oberhausen nchini Ujerumani.

Watabiri wengine

Wanyama wengine wametambulishwa kwa umma wakiaminika kuwa na uwezo wa kumrithi pweza Paul, akiwemo nungubandia, yaani guinea pig, kwa Madame Shiva kutoka Uswizi mwaka 2014.

Kulikuwa pia na samaki kwa jina Piranha Pele kutoka Uingereza.

Lakini hakuna aliyeufikia umaarufu wa Paul the Octopus.

Maombi

Mapema Jumatano, kiongozi wa kanisa la Kiothodoksi la Urusi, kanisa ambalo lina waumini wengi sana Urusi, Askofu Mkuu Kirill, alisema atawaombea Urusi wacheze vyema.

Unaweza kusoma pia: