Tanzania: Tunafaa kuwajua wachezaji ‘wetu’ walio nje ya nchi

Poulsen Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Poulsen akisherehekea na wenzake baada ya kufunga dhidi ya Peru

Afisa mmoja mkuu serikalini Tanzania amesena taifa hilo la Afrika Mashariki linafaa kutathmini na kujua idadi ya wachezaji wenye asili ya taifa hilo ambao wanacheza katika mataifa ya nje.

Hii ni baada ya mchezaji ambaye babake ni Mtanzania, Yusuf Yurary Poulsen, kufanya vyema akiichezea timu ya taifa Denmark katika Kombe la Dunia Urusi.

Poulsen alifunga bao pekee wakati wa mechi hiyo dhidi ya Peru Jumamosi na baadaye akatawazwa kuwa mchezaji bora wa mechi na Fifa.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini Yusuph Singo, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuweka utaratibu wa kutambua wachezaji kama hao.

Singo alisema shirikisho hilo ndilo lenye dhamana ya kujua idadi ya wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza Ulaya ambao watawekewa utaratibu na Serikali ili kuitumikia timu ya taifa.

"Serikali hatuwezi kujua kila mchezaji anayecheza Ulaya ndio maana kuna taasisi (TFF) ambayo pamoja na mambo mengine ya kiutendaji, inatakiwa kuweka mfumo mzuri wa kutambua wachezaji wetu wanaocheza nje ya nchi," amenukuliwa na gazeti hilo.

"Kwa mfano huyu Mtanzania anayecheza Denamrk hatukuwa tukimfahamu, kama vyama vyetu vya michezo vingekuwa na utaratibu mzuri wa kujua wachezaji gani wanacheza nje ingekuwa rahisi."

Anapocheza soka ya kulipwa, mchezaji huyo hutumia jina lake la Kidenmark, Poulsen, lakini katika timu ya taifa hutumia jina la babake, Yurary.

Kumekuwa na mjadala mtandaoni kuhusu iwapo anafaa kuchukuliwa kama Mtanzania au kama raia wa Denmark, ikizingatiwa kwamba kwa sasa sheria ya Tanzania hairuhusu uraia wa nchi mbili.

Poulsen ndiye mchezaji wa kwanza wa asili ya Tanzania kucheza fainali za Kombe la Dunia na pia aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa asili ya Tanzania kufunga bao.

Haki miliki ya picha AFP/Getty

Mchezaji mwingine wa asili ya Tanzania Patrick Mtiliga aliwahi kujumuisha kikosi cha Kombe la Dunia lakini hakuingia uwanjani kucheza.

Poulsen, ambaye babake alitokea Tanga, amewahi kuzuru Tanzania mara kadha.

Kwenye mahojiano na vyombo vya habari awali, alisema hakupokea ombi lolote la kuichezea Tanzania ingawa kwa sasa hajui jibu lake lingekuwa gani.

"Kwanza ilikuwa faraja kwangu kucheza timu iliyokuwa daraja la kwanza Denmark mwanzoni na kucheza kwa msimu mzima, kuhusu kwani nini sikucheza timu ya taifa ya Tanzania? ni swali zuri lakini kiukweli sikupokea ofa kutoka Tanzania ya kucheza timu ya taifa lakini pia sijui ingekuwaje kama ofa ingekuja," alisema alipohojiwa na Ayo TV Julai mwaka jana.

Hata hivyo, alikiri kwamba hawezi kusema iwapo angelipokea ofa kama hiyo, uamuzi wake ungekuwa gani.

"Nimecheza timu zote za vijana za taifa za Denmark na sasa timu ya wakubwa lakini sikuwahi kufikiria kama ningepata nafasi ya kucheza timu ya taifa ya wakubwa ya Denmark hadi nilivyoitwa lakini nimezaliwa na kukulia Denmark kama nilivyosema awala kama ofa ya Tanzania ingekuja sijui ningechagua kucheza timu gani".

Ndoto ya Patrick Mtiliga Kombe la Dunia

Yussuf Poulsen amezidi ufanisi wa mchezaji mwingine mwenye asili kama yake, Patrick Jan Mtiliga ambaye kwa sasa amestaafu soka.

Mtiliga alizaliwa 28 Januari 1981 ambapo babake alikuwa Mtanzania.

Alikuwa beki na alichezea timu ya taifa ya Denmark mechi sita na alikuwa ameteuliwa kikosi cha wachezaji 23 wa kucheza Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini. Hata hivyo hakufanikiwa kucheza. Denmark waliondolewa kwenye michuano hiyo hatua ya makundi baada yao kumaliza nafasi ya tatu kundi lao.

Katika soka ya kulipwa, Alichezea klabu kadha za Denmark na Uholanzi kabla ya kuhamia Malaga ya Uhispania mwaka 2009.

Mwanzoni mwa mwaka 2010, aliumizwa kwneye pua na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid jambo lililomfanyakutocheza wiki tatu.

Aliondoka Malaga Juni 2011 baada ya mkataba wake kumalizika na kujiunga na FC Nordsjælland ya Denmark ambapo alimalizia uchezaji wake mwaka 2015 baada ya kuwachezea mechi 150 na kufunga mabao 5.