Diego Maradona amuonya kocha 'kutorudi' Argentina iwapo wataondolewa Kombe la dunia

Kocha wa Argentina Jorge Sampaoli Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kocha wa Argentina Jorge Sampaoli

Kiungo wa zamani wa Argentina Diego Maradona ameikashifu timu yake ya zamani kwa kutoka sare na Iceland kwenye mchuano wao wa kwanza wa Kundi D siku ya Jumamosi.

Maradona ameilaani timu hiyo na kumtahadharisha meneja Jorge Sampaoli dhidi ya kurejea Argentina iwapo wataendelea kucheza vile.

Lionel Messi alipoteza penalti wakati timu hiyo ilipolazimishwa sare na Iceland, wanaoshiriki kombe hilo kwa mara yao ya kwanza .

Image caption Diego Maradona

Maradona, ambaye pia amewani kuinoa timu hiyo, alikuwa uwanjani Spartak kutazama kipute hicho.

"Nahisi kuna hasira kwenye roho ya timu," alisema.

Licha ya Argentina kuongoza kupitia bao la Sergio Aguero dakika ya 19, iliichukua Iceland dakika nne pekee kusawazisha kupitia Alfred Finnbogason.

"Ni aibu kubwa. Kutojiandaa vizuri ukifahamu wachezaji wa Iceland wana urefu wa mita 1.90," mshindi huyo wa kombe la dunia 1986 aliiambia runinga moja ya Venezuela.

Lionel Messi

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Messi inauma kukosa penalti

Messi alisema " inauma" kuona mkwaju wako ukiokolewa

Messi alitarajia kuwa na mchango mkubwa kwenye mchuano huo baada ya mpinzani wake Cristiano Ronaldo kuiinua Ureno kwa kufunga het-triki dhidi ya Uhispania siku ya Ijumaa.

Mbali na kuzimwa na mabeki hodari wa Iceland, mkwaju wa Messi wa dakika ya 63 ulidakwa na kipa Hannes Halldorsson.

"Siwalaumu wachezaji. Naweza kulaumu juhudi zao. Kamwe siwalaumu wachezaji, hata Messi ambaye alijituma," aliongeza Maradona.

"Nimepoteza penalti pia nikiwa Diego Armando Maradona. Sidhani Argentina pia wamepoteza alama kwa kuwa Messi alipokosa bao la penalti," alisema nyota huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 57,aliyeisaidia Argentina kufika robo fainali ya kombe la dunia 2010 nchini Afrika Kusini.

Argentina sasa inajiandaa kukwatuana na Croatia kwenye mchuano wao ujao uwanjani Saint Petersburg, tarahe 21Juni.