Ahmed Musa awapa Nigeria ushindi wa 2-0 dhidi ya Iceland Kombe la Dunia 2018

Ahmed Musa Haki miliki ya picha AFP

Nigeria wamewashinda Iceland 2-0 na kuandikisha ushindi wao wa kwanza katika Kombe la Dunia Urusi. Awali Brazil waliwacharaza Costa Rica 2-0.

Baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa uwanja wa Volgograd Arena, mashabiki wa soka Afrika waliungana kusherehekea ushindi huo wa kihistoria wa Nigeria. Furaha zilizoletwa na Senegal siku chache zilizopita zikionekana kusahaulika.

Magoli mawili ya Ahmed Musa kipindi cha pili yalitosha kuzamisha taifa ndogo la Iceland na kufufua matuimaini ya Nigeria.

Kundoka kwa wawakilishi wengine wa Afrika; Misri na Morocco, Kombe la Dunia, kuliwatia hofu Nigeria.

Baada ya dakika 90: Mambo yakawa yamebadilika

Nigeria maarufu Super Eagles walianza mechi wakiwa na kikosi tofauti na kile kilicholazwa 2-0 na Croatia.

Wafungaji wanaoichezea Leicester City Ahmed Musa na Kelechi Iheanacho wakianza mechi Kombe hili kwa mara ya kwanza .

Aidha, kiungo wa Arsenal Alex Iwobi aliachwa kwenye benchi huku beki wa Chelsea Kenneth Omeruo akiingia nafasi yake.

Kipindi cha kwanza kilikamilika bila pande hizo kufungana

Goli la kwanza:

Dakika nne tu baada ya awamu ya pili kuanza, Ahmed Musa alituliza mpira na kufyatua kombora lililoiweka Nigeria mbele.

Victor Moses alimuandalia krosi safi kutoka wingi ya kushoto.

Iceland yaanza kushambulia

Iceland ilijaribu kusawazisha lakini ngome ya Nigeria ikiongozwa na Kenneth Omeruo ilizuia.

Ahmed Musa tena

Katika dakika ya 75, Musa aligeuka Messi alipomchenga kipa Hannes Halldorsson na kwa ujasiri, akazidisha uongozi wa Nigeria.

Aidha, sherehe za Nigeria zilikaribia kukatizwa dakika ya 83 baada ya Iceland kupata Penalti. Kiungo wa kutegemewa wa Iceland Gylfi Sigurdsson aliupaisha mkwaju huo.

Mabao hayo mawili ya Ahmed Musa yamebadilisha muundo wa kundi D huku Nigeria ikichupa hadi nafasi ya pili ikiwa na alama 3.

Kutoka Kundi D, Croatia tayari imefuzu kwa hatua ya muondoano huku macho yote yakiwa kwenye mechi kati ya Argentina na Nigeria.