Martin Olsson: Mchezaji Mkenya anayecheza Kombe la Dunia Urusi 2018

Martin Olsson akipigania mpira na Marco Marin wa Ujerumani wakati wa mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Uefa U21 uwnajani Malmoe, Ujerumani 2007 Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Martin Olsson akipigania mpira na Marco Marin wa Ujerumani wakati wa mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Uefa U21 uwnajani Malmoe, Ujerumani 2007

Katika kikosi cha timu ya taifa ya Sweden kinachocheza katika Kombe la Dunia Urusi ni vigumu kufikiria kuna uhusiano wowote kati ya kikosi hicho na Kenya.

Lakini katika kikosi kinachowakilisha taifa hilo la Ulaya, kuna mchezaji aliye na uhusiano wa karibu sana na Kenya, kimsingi ni raia wa Kenya ikizingatiwa kwamba uraia pacha unaruhusiwa Kenya chini ya katiba ya sasa.

Mchezaji huyo si mwingine ila ni Martin Tony Waikwa Olsson mwenye miaka 30 anayechezea klabu ya Swansea City ya Uingereza.

Aliwahi kuchezea pia klabu za Blackburn Rovers na Norwich City.

Olsson amewakilisha timu za taifa za vijana za Sweden na amekuwa katika timu kuu ya taifa tangu mwaka 2010.

Amekuwa kwenye benchi katika kikosi cha Sweden kufikia sasa.

Sweden wanacheza dhidi ya Mexico Jumatano jioni. Waliwashinda Korea Kusini 1-0 mechi yao ya kwanza 18 Juni lakini wakashindwa na Ujerumani 2-1 dakika za mwisho kupitia bao la Toni Kroos.

Mchezaji huyu alizaliwa 17 Mei 1988 mjini Gavle, Sweden.

Babake ni raia wa Sweden lakini mamake Maggie Olsson alikuwa Mkenya ingawa kwa sasa ni marehemu. Alitokea Nanyuki, karibu na Mlima Kenya.

Familia yao ni ya wachezaji kwani ndugu yake ambaye ni pacha Marcus Jonas Munuhe Olsson ni mchezaji kandanda na sawa na Martin yeye pia ni mkabaji wa upande wa kushoto uwanjani ambaye pia hucheza safu ya kati.

Dada yao Jessica Olsson, ambaye ni mkubwa wao, ameolewa na mchezaji wa mpira wa kikapu kutoka Ujerumani Dirk Nowitzki ambaye huichezea Dallas Mavericks katika NBA. Wawili hao wana watoto watatu, na wa kwanza na msichana pekee alipewa jina Malaika. Wawili hao walifanya harusi Kenya na nchini Ujerumani na hata akalipa mahari Kiafrika.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Marcus Olsson (kushoto) ameichezea Derby mechi 67 tangu ajiunge nao kutoka Blackburn 2016, akikabiliana na Jesse Lingard wa Manchester United

Martin na Marcus wana majina ya Kiafrika kwenye majina yao rasmi - Waikwa na Munuhe.

Martin Olsson alianza uchezaji soka kwa kujiunga na timu cha wachezaji chipukizi katika klabu ya Hogaborgs BK ya Sweden na baadaye akahamia klabu ya Blackburn Rovers ya Uingereza.

Baada ya kupanda ngazi Blackburn Rovers alijiunga na timu kuu ya klabu hiyo mwaka 2007 na kuwachezea mechi yao ya kwanza wakati wa mechi za kufuzu kwa michuano ya ubingwa Ulaya msimu wa 2007/08.

Martin alicheza mechi yake ya kwanza Ligi ya Premia 30 Desemba 2007 dhidi ya Derby County.

Baadaye alitia saini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo mwaka 2008 na kuwafungia bao lake la kwanza dhidi ya Everton Septemba mwaka huo.

Alihamia Norwich City kwa mkataba wa miaka minne Julai 2013.

Martin Olsson alijiunga na Swansea City Januari mwaka jana kwa uhamisho wa thamani ya $ 5.54 milioni na akawafngia bao la kwanza dhidi ya Leicester City 12 Februari 2017.

Katika timu ya taifa, alicheza vikosi vya wachezaji wa chini ya miaka 19 na 21 kabla ya kujiungana kikosi kikuu mwaka 2010.

Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Martin Olsson alianza uchezaji wake Hogaborgs BK, Sweden

Amewachezea Sweden mechi 41 na kuwafungia mabao matano.

Katika kipindi ambacho amekuwa na timu ya taifa ya Sweden, amecheza na wachezaji nyota wa Sweden. Alikuwa na wachezaji kama vile Seb Larsson na Mikael Lustig chini ya nahodha Zlatan Ibrahimovic katika Euro 2012 na 2016.

Kujivunia kuwa Mkenya

Katika mahojiano na mtandao wa Wales Online, Martin alisema anajivunia sana asili yake.

"Ninajivunia sana asili yangu, mamangu alifariki miaka michache iliyopita na tulilelewa katika utamaduni huo na najivunia kuwa raia wa Sweden na Mkenya pia," alisema.

"Nina jamaa wengi sana huko, huwa twajaribu kutembea na kuzuru, dadangu husafiri huko mara nyingi kwa sababu ya ratiba yangu hapa. Nilikwenda huko miaka kadha iliyopita na nilifurahia kuwaona jamaa zangu."

Anasema alifurahia kuona kwamba mtindo wa maisha ni tofauti, watu huwa wametulia, na "kila mtu huwa hazungumzi kwa simu."

"Napenda maisha sana huko na hali ya afya ni nzuri."

"Tuna jamaa Nairobi na Mombasa. Nairobi ndiko tulikozoea kuishi, na tuna jamaa Nanyuki pia, mwendo wa saa mbili hivi kutoka mji huo mkuu."

"Binamu zangu wako huko na hutazama mechi kupitia runinga, kwa hivyo Swansea wana mashabiki Kenya."

Kikosi kamili cha Sweden Kombe la Dunia

Walinda lango: Robin Olsen (Copenhagen), Karl-Johan Johnsson (Guingamp), Kristoffer Nordfeldt (Swansea).

Mabeki: Mikael Lustig (Celtic), Victor Lindelof (Manchester United), Andreas Granqvist (Krasnador), Martin Olsson (Swansea), Ludwig Augustinsson (Werder Bremen), Filip Helander, Emil Krafth (both Bologna), Pontus Jansson (Leeds United).

Viungo wa kati: Sebastian Larsson (Hull), Albin Ekdal (Hamburg), Emil Forsberg (RB Leipzig), Gustav Svensson (Seattle Sounders), Oscar Hiljemark (Genoa), Viktor Claesson (Krasnador), Marcus Rohden (Crotone), Jimmy Durmaz (Toulouse).

Washambuliaji: Marcus Berg (Al Ain), John Guidetti (Alaves), Ola Toivonen (Toulouse), Isaac Kiese Thelin (Waasland-Beveren).