Kombe la Dunia 2018: Messi wa Iran Sardar Azmoun astaafu kwa sababu ya matusi

Iran forward Sardar Azmoun Haki miliki ya picha AFP

Mshambuliaji wa Iran ambaye amekuwa akicheza Kombe la Dunia Sardar Azmoun amestaafu kuchezea timu ya taifa akiwa na miaka 23.

Anasema amestaafu kwa sababu mama yake ameanza kuugua kutokana na matusi aliyoyapokea.

Azmoun - ambaye amepewa jina la utani 'Messi wa Iran' - alikuwa amefunga mabao 23 katika mechi 33 alizokuwa amelichezea taifa lake kabla ya michuano ya sasa.

Hata hivyo, hakufanikiwa kufunga bao lolote Urusi huku vijana hao waliokuwa chini ya mkufunzi Carlos Queiroz walimaliza wa tatu katika Kundi B nyuma ya Uhispania na Ureno.

Azmoun amesema uamuzi wake wa kuacha kuichezea Iran ni "mchungu".

Alifunga mabao 11 katika mechi 14 alizowachezea za kufuzu kwa Kombe la Dunia na alicheza muda wote katika mechi zao tatu walizocheza katika hatua ya makundi ambapo Iran waliwashinda Morocco, wakashindwa na Uhispania na wakatoka sare na Ureno.

Hata hivyo, Azmoun amesema ukosoaji ulioelekezwa kwake umemfanya mamake kuugua.

"Mamangu alikuwa mgonjwa sana na alikuwa ameanza kupata nafuu na nilikuwa na furaha," anasema Azmoun anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Rubin Kazan.

"Inasikitisha kwa sababu ya ukatili wa baadhi ya watu, na matusi ambayo mimi na wenzangu hatukustahili, sasa amezidiwa na ugonjwa.

"Hili limeniweka katika njia panda ambapo inanilazimu kuchagua moja kati ya hayo mawili - na nimeamua kumchagua mamangu."

Azmoun alianza kuchezea timu ya taifa ya Iran akiwa na miaka 19.

Anashikilia nafasi ya tano katika orodha ya wafungaji mabao bora wa Iran na alikuwa anafananishwa na shujaa wa taifa hilo Ali Daei, anayeongoza akiwa na mabao 109 katika mechi 149.