Kombe la Dunia 2018: Kylian Mbappe ana uhusiano na Tanzania?

Kylian Mbappe in action for Bondy as a youngster and playing for France Haki miliki ya picha Bondy/AFP
Image caption Mbappe

Mchezaji wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 19 Kylian Mbappe alicheza kwa ustadi wa hali ya juu Jumamosi katika mechi ambayo wengi wanasema iliashiria kukabidhiana kwa mwenge kutoka kwa kizazi kimoja cha wachezaji hadi kingine.

Chipukizi huyu alitawala mechi dhidi ya Argentina katika hatua ya 16 bora Kombe la Dunia na kugubika nyota ya mchezaji wa Barcelona Lionel Messi uwanjani Kazan Arena.

Ufaransa waliibuka washindi 4-3 dhidi ya Argentina na kuonekana kufuta kabisa matumaini ya Messi, 31, kushinda Kombe la Dunia.

Kasi ya Mbappe na nguvu zake pia viliwatatiza sana mabeki wa Argentina na alifunga mabao mawili (dakika ya 64 na 68) pamoja na kuchangia penalti ambayo ilisaidia Antoine Griezmann kufunga dakika ya 13

Kijana huyo kutoka viungani mwa Paris aliibuka kuwa mchezaji wa kwanza wa chini ya miaka 20 kufunga mabao mawili Kombe la Dunia tangu Pele wa Brazil alipofanya hivyo akiwa na miaka 17.

Pele mwenyewe aliandika kwenye Twitter: "Hongera, @KMbappe. Mabao mawili katika Kombe la Dunia ukiwa na umri mdogo hivyo yanakuweka katika kundi la watu maarufu!"

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mbappe alijiunga na Monaco mwaka 2015

Paul Pogba alisema: "Ana kipaji zaidi yangu. Na hatakomea hapa. Ana kipaji adimu."

Kuangaziwa kwake kuliwafanya baadhi kuanza kujadili kuhusu asili yake. Chimbuko lake ni wapi? Na wazazi wake je?

Mbappe anatokea Rungwe au Mwanza?

Katika makundi ya WhatsApp na baadhi ya mitandao ya kijamii, kulizuka taarifa kwamba babake Mbappe ni Mtanzania.

"Mfahamu Kylian (Ambakisye) Asumwike Mpepe almaarufu Mbappe ni kijana wa Kitanzania aliyezaliwa huko Ufaransa.Mbappe ni mchezaji wa kimataifa wa timu ya Ufaransa.Baba yake mzazi anatokea kitongoji cha Itebe katika kijiji cha Ikubo huko Mwakaleli-Busokelo (zamani Rungwe Mashariki)," taarifa moja ilisoma.

Haki miliki ya picha Twitter

"Mr. Asumwike Mpepe Mwalugelo ni Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na watoto, alikwenda nchini Ufaransa mwaka 1995 kufanya kazi katika taasisi ya Afya ya Ufaransa."Alikutana na mwanamke mwenye asili ya Algeria anayeitwa Fayza mwaka 1997 na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na walioana January 2 mwaka 1998 huko Paris."Tarehe 20 Decemba walibahatika kupata mtoto wa kiume waliyempa jina la Kylian lakini Baba yake akampa jina la Kinyakyusa Ambakisye."Huyu ndio Kylian Mbappe kijana wa Kitanzania aliyepeleka kilio huko mjini Buenos Aires, Argentina!"

Baadhi wamekuwa wakiandika kwenye mitandao ya kijamii wakisema anatokea maeneo mengine ya Tanzania, mfano Mwanza.

Haki miliki ya picha Facebook

Kuna chembe ya ukweli kwenye madai haya? Na Nigeria basi?

Haki miliki ya picha TWITTER

Kwa mujibu wa mtandao wa Punch wa Nigeria, Kylian alipewa jina la pili na babake Adesanmi ambalo maana yake kwa lugha ya Kiyoruba ni "taji linanitosha mimi".

Kakake mdogo kwa jina Ethan jina lake la pili ni Adeyemi ambalo maana yake kwa Kiyoruba ni "taji linakutoshea wewe."

Chimbuko la Kylian Mbappe

Mchezaji huyu alizaliwa mnamo 20 Desemba 1998 katika familia ya wachezaji eneo la Bondy kaskazini mashariki mwa Paris, Ufaransa. Jina lake kamili ni Kylian Mbappe Lottin.

Babake Wilfried Mbappé alitoka Cameroon, ingawa ana mizizi pia Nigeria, na mamake Fayza Mbappé Lamari ni wa asili ya Algeria.

Wawili hao walikutana Ufaransa. Wilfried alikuwa amekimbilia Ufaransa kama mkimbizi na akamuoa Fayza ambaye alikuwa tayari ni raia wa Ufaransa katika juhudi za kutaka kupata idhini ya kusalia Ufaransa.

Fayza alikuwa mchezaji stadi wa mpira wa handiboli naye Wilfried ni mkufunzi wa michezo mbalimbali.

Babake alikuwa ndiye mkufunzi wake utotoni, na anasema kipaji chake kilianza kuonekana akiwa na miaka sita pekee. Kwa sasa, ndiye wakala wake.

Mchezaji huyo alizaliwa takriban miezi sita baada ya Ufaransa kushinda Kombe la Dunia wakiwa wenyeji mwaka 1998 katika uwanja wa Stade de france ambao unapatikana kilomita 11 kutoka nyumbani alikozaliwa Mbappe.

Eneo alikozaliwa lilikuwa zamani limeathiriwa na ghasia, mauaji na maandamano lakini hayo hayakumvunja moyo.

Uwezo wake wa kuchagua nini cha kuangazia ulimuwezesha kuangazia vyema soka na kuanza kufanikiwa tangu utotoni, akisaidiwa na wazazi wake.

Alijifunza kushambulia kwa kasi, na kutumia vyema mguu wake wa kushoto, pamoja na kuwapiga wachezaji chenga akiwa na mpira.

Akiwa na miaka sita, alikuwa tayari anatazamwa kama miongoni mwa watoto wachezaji soka bora zaidi Ufaransa.

Alitambuliwa na Shirikisho la Soka la Ufaransa wakati mmoja akiwa bado mtoto.

Klabu ya AS Bondy kwa sasa hucheza ligi ya daraja la 10 nchini Ufaransa, katika ligi ya Paris ile-de-France lakini wana mfumo unaofanikiwa sana wa kukuza wachezaji tangu wakiwa wadogo.

Wachezaji ambao wamepitia mfumo wao ni pamoja na nyota wa Sevilla Sebastien Corchia na mchezaji wa timu ya taifa ya DR Congo Fabrice N'Sakala.

Hadi kufikia miezi mitatu iliyopita, babake Mbappe, Wilfried alikuwa mmoja wa wakurugenzi wa michezo katika klabu hiyo akiwashughulikia watoto wa chini ya miaka 10 na wa chini ya miaka 17, lakini katika majukumu tofauti kwa kipindi cha miaka 25 katika AS Bondy.

Mbappe alijifunzia soka katika akademi ya kitaifa ya soka Clairefontaine ambayo huangazia kukuza wachezaji wa Ufaransa wenye kipaji cha kucheza kandanda kuanzia akiwa na miaka 12 lakini mwanzoni aliendelea kuwachezea AS Bondy.

Wachezaji nyota kama vile Thierry Henry, Nicolas Anelka, Blaise Matuidi na William Gallas walipitia katika chuo hicho.

Akiwa na miaka 15, ambapo kawaida wachezaji huondoka Clairefontaine baada ya kukamilisha mafunzo ya miaka miwili, Mbappe alikataa fursa ya kujiunga na klabu nyingi kuu za Ulaya zikiwemo Real Madrid, Chelsea, Manchester City, Liverpool na Bayern Munich, na nyingine kuu za Ufaransa na kuamua kujiunga na Monaco ambako aliendelea na masomo yake mjini humo.

Alianza kuwachezea akiwa na miaka 16 na siku 347 mnamo 2 Desemba 2015 ambapo alivunja rekodi iliyowekwa na Henry ambaye alianza kuwachezea akiwa na miaka 17 na siku 14. Aliingia mchezoni akiwa kama nguvu mpya.

Taarifa zinasema hata hivyo kwamba alikubali angejiunga na Monaco akiwa na miaka 14.

Haki miliki ya picha John Bennett
Image caption Umaarufu wa AS Bondy umepanda tangu kuanza kufahamika kwa Mbappe

Ingawa babake alikuwa ameahidiwa kwamba Monaco wangempa fursa ya kucheza na kujikuza, kufikia Oktoba, miezi miwili baada ya Monaco kukataa ofa kutoka kwa Manchester City ya thamani ya £40m, hakuwa ameanza mechi hata moja.

Babake aliwatishia na kuwaona kwamba angemhamisha Januari iwapo mambo hayangebadilika.

Meneja wa Monaco Leonardo Jadim ni hapo alipoamua kumchezesha kikosi cha kuanza mechi dhidi ya Montpellier ambapo alichangia pakubwa ushindi wao wa 6-2.

Mbappe alikuwa miongoni mwa wachezaji waliong'aa michuano ya ubingwa Ulaya kwa wachezaji wa chini ya miaka 19 nchini Ujerumani mwaka 2016.

Alifunga mabao matano, mawili katika nusufainali. Mfungaji mabao bora wa michuano hiyo alikuwa Jean-Kevin Augustin, aliyekuwa ndio tu ameondoka PSG na kujiunga na RB Leipzig ya Ujerumani.

Henry alisema si haki kumuita 'Thierry Henry mpya' lakini kuna wengine wanaomuita 'Neymar mpya'.

Si ajabu kwamba baada ya uchezaji wake dhidi ya Argentina Kombe la Dunia, wengi walianza kumtazama kama mrithi wa Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, akiwa pamoja na nyota wa Misri Mo Salah.

Katika chini ya miaka miwili, ameshinda taji la Ligue 1 mara mbili na amekuwa akichezeshwa kama mchezaji muhimu kikosini timu ya taifa ya Ufaransa na Paris St-Germain.

Anatarajiwa kukamilisha uhamisho wa kudumu wa kusalia PSG kwa euro 180m hivi karibuni.

Kusherehekea mabao

Mbappe ana kaka mdogo wa umri kwa miaka saba kwa jina Ethan.

Kylian wakati mmoja alikuwa na makubaliano na Monaco kwamba angeandamana na kakake kama mtoto wa kusindikiza wachezaji.

"Alitaka hilo. Ulikuwa wakati muhimu sana kwake. Alikuwa akinisisitizia kwamba niende naye uwanjani, na nikamwambia, basi nitakuchukua siku moja," anasema.

Ethan ndiye sababu ya Kylian kusherehekea mabao akiwa ameikunja mikono yake kifuani na kuinua vidole vya gumba.

Anasema hivyo ndivyo Ethan alivyozoea kusherehekea kila akimshinda katika mchezo wa video wa Fifa kwenye playstation.

Haki miliki ya picha Alex Scott Tiwtter
Image caption Mbappe na picha za wachezaji aliowaenzi utotoni

Ndugu raia wa DR Congo

Mbappe ana ndugu wa kambo kwa jina Jires Kembo-Ekoko kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye aliasiliwa na babake.

Babake na Wilfried Mbappe walikuwa marafiki wa karibu na aliichezea Zaire katika Kombe la Dunia mwaka 1974.

Jires alihamia Ufaransa akiwa mtoto kukaa na Wilfried ambaye alichukua majukumu ya kuwa mlezi wake.

Ni mkubwa wa Kylian kwa miaka 10 lakini wote wawili huenziana. Jires aliwahi kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Rennes.

Ukomavu wa mtu wa miaka 40

Uso wake huwa na sura ya mtu wa umri mkubwa lakini si uso wake pekee ulio na ukomavu.

Ni mkomavu wa tabia na masomoni pia.

Mbappe mara kwa mara huandika mitandaoni kuhusu familia yake na ana uhusiano wa karibu sana na babake Wilfried na mamake Fayza.

Alifaulu mtihani wake wa shule ya upili katika somo la usimamizi wa sayansi na teknolojia.

Alikamilisha masomo yake ya sekondari akiwa bado anajifunza masuala ya soka.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii