Kombe la Dunia 2018: Pweza mtabiri wa mechi Japan ageuzwa kitoweo

Giant Pacific octopus Haki miliki ya picha Science Photo Library

Pweza anayeaminika kuwa na uwezo wa kipekee, na ambaye alikuwa amefanikiwa kutabiri matokeo ya mechi zote za Japan katika Kombe la Dunia Urusi ameuawa na kuuzwa sokoni awe kitoweo.

Pweza huyo aliyekuwa amepewa jina Rabio alikuwa amepata sifa si haba baada yake kujaribiwa kwenye kidimbwi kidogo cha watoto na kuwa mtabiri stadi.

Lakini Kimio Abe, mvuvi aliyemvua kutoka baharini, amesema aliona ni heri kumwuza ageuzwe kuwa chakula.

Anasema alibaini angepata pesa nyingi iwapo angemuuza apikwe na kuwa chakula kitamu cha Kijapani kwa jina sashimi kuliko kama angeendelea kutumiwa kutabiri.

Rabio - ambaye alikuwa pweza mkubwa - alifanikiwa kubashiri matokeo ya Japan dhidi ya Colombia na pia sare yao dhidi ya Senegal kwa kuhamia maeneo mbalimbali kwenye kidimbwi.

Kulikuwa na maeneo matatu kwenye kidimbwi, kila eneo likiwa limewekwa nembo ya kushinda, kushindwa au sare. Kila eneo lilikuwa na chakula cha kumshawishi pweza huyo aelekee huko.

Japan walionekana kukaribia kufika hatua ya robofainali kwa mara ya kwanza walipokuwa wanaongoza 2-0 dhidi ya Ubelgiji mechi ikikaribia kumalizika.

Lakini walivunjwa moyo Ubelgiji walipokomboa na pia kufunga bao la ushindi dakika ya mwisho.

Huku wachezaji wa Japan wakiendelea kutafakari kuhusu vile mambo yangelikuwa iwapo wangefanikiwa, angalau wana afya yao na uhai pia.

Rabio sasa ni mchuzi.

Lakini kazi yake inatarajiwa kuendelea. Mvuvi huyo anapanga kumtumia pweza mwingine kutabiri matokeo mechi za siku za usoni.

Rabio alipelekwa sokoni kabla ya Japan kushindwa 1-0 na Poland mnamo 28 Juni.

Alikuwa ametabiri kushindwa ka Japan, lakini pengine hakufahamu kwamba kifo chake kilikuwa karibu.

Rabio si pweza wa kwanza kupata umaarufu kwa kutabiri matokeo ya mechi za kimataifa.

Kulikuwa na Paul ambaye mwaka 2010 alitabiri kwa ufasaha matokeo ya mechi sita za Kombe la Dunia.

Alifariki mwaka 2012. Alikuwa ametabiri kwamba England wangefanikiwa kuwa wenyeji wa michuano ya sasa ya Kombe la Dunia lakini akanoa kwani Urusi ndio waliopata fursa hiyo.

Mwaka huu kumekuwa pia na paka kwa jina Achilles nchini Urusi.

Soma kumhusu hapa: Paka mtabiri anayetaka kumrithi Paul the Octopus

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Paka mtabiri kwa jina Achilles

Watabiri wengine

Wanyama wengine wametambulishwa kwa umma wakiaminika kuwa na uwezo wa kumrithi pweza Paul, akiwemo nungubandia, yaani guinea pig, kwa Madame Shiva kutoka Uswizi mwaka 2014.

Kulikuwa pia na samaki kwa jina Piranha Pele kutoka Uingereza.

Lakini hakuna aliyeufikia umaarufu wa Paul the Octopus.