'Ningejua ningefuata nyayo za Weah' asema mchezaji wa zamani wa Kenya Nashon Oluoch

George Weah at AC Milant Haki miliki ya picha Hutton Archive
Image caption George Weah akiwa AC Milan

Nashon Oluoch ni miongoni mwa wachezaji kandanda hodari walioiwakilisha kilabu mashuhuri ya Kenya Gor Mahia katika mashindano mbali mbali ya kimataifa.

Mnamo mwaka wa 1982 Oluoch alishangaza wachezaji wenzake, maafisa wa kilabu hiyo na mashabiki wao alipotangaza anaondoka Gor Mahia akiwa na mwenzake Sammy Owino kwenda Marekani kwa masomo.

``Tuliangalia hali duni ya maisha ya wachezaji wa zamani wa Kenya kama vile Joe Kadenge na William ''Chege'' Ouma tukaamua ni afadhali tuachane na kandanda ya Kenya tukasome zaidi huko Alabama nchini Marekani,'' anaeleza Oluoch.

``Kenya haitilii maanani kabisa maslahi ya wachezaji wake hasa walioifanyia kazi kubwa timu ya taifa. Hatukutaka nasi pia tujikute kwenye maisha hayo duni tukistaafu kwa kandanda.''

Mbali na Wakenya hao wawili kujiunga na chuo hicho kikuu cha Alabama, mchezaji mwengine aliyetarajiwa kuwa huko ni Rais wa sasa wa Liberia George Weah ambaye naye alivuma kwenye uwanja wa kandanda.

Kulingana na Oluoch, Weah aliamua kucheza kandanda ya kulipwa badala ya masomo, na uamuzi huo ukamletea ufanisi zaidi ya wachezaji hao wa Kenya ambao wakati huo walikua na uwezo wa kufanya vyema zaidi ya Weah kwenye uwanja wa kandanda.

Image caption Nashon Oluoch ni miongoni mwa wachezaji kandanda hodari walioiwakilisha kilabu mashuhuri ya Kenya Gor Mahia

Hatimaye Weah alivuma sana mpaka akachaguliwa mchezaji bora zaidi duniani, mchezaji wa kwanza wa Afrika kupata tuzo hilo. Pesa alizopata Weah kama mchezaji wa kulipwa hangezipata endapo angeendelea na masomo Marekani.

Je, mbona Oluoch na Owino hawakufikiria kucheza kandanda ya kulipwa kama Weah?

``Hawa wenzetu wa Afrika Magharibi walifunguka kiakili mapema sana upande huo zaidi yetu hapa Afrika Mashariki,'' anaeleza Oluoch.

``Hapa Kenya sidhani mwaka huo wa 1982 tulikua na Wakala wa kandanda kutuunganishia mkataba wa kucheza kandanda barani Ulaya. Na bado tuko nyuma hapo.Pweza mtabiri wa mechi Japan ageuzwa kitoweo

``Mimi na mwenzangu Owino tulikua juu sana kwa kandanda, na kama tungepata ushauri mzuri tungecheza kandanda ya kulipwa lakini inaonekana shirikisho la kandanda nalo pia lilizembea upande huo ama labda maafisa wake hawakutaka kuona wachezaji wanajiendeleza zaidi. Hatahivyo sijuti kamwe kwa sababu uamuzi wetu na Owino wa kusoma zaidi umetusaidia sana. Kwa sasa naishi maisha mazuri.''

Oluoch, kwa jina la utani Lule, alirejea nyumbani mwaka wa 1987 na kupata kazi ya mhadhiri katika chuo kikuu cha Egerton eneo la bonde la ufa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption George Weah akicheza soka mjini Monrovia mnamo 2016

Alifanya biashara pia na kuanzisha jumba la starehe kwa jina Lules Club akiuza vinywaji vya kila aina. Lakini mwaka wa 2007 wakati wa uchaguzi mkuu wa Kenya jumba hilo lilichomwa kutokana na ghasia zilizozuka.

Sasa Oluoch anajishugulisha na biashara ya ujenzi mjini Nakuru, na ana nia ya kuanzisha mradi wa kukuuza vipaji vya wachezaji chipukizi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii