Kombe la Dunia 2018: Maradona asema England waliwaibia Colombia kisha aomba radhi

Argentina legend Diego Maradona Haki miliki ya picha Getty Images

Timu ya taifa ya soka ya Uingereza ikijiandaa kwa mechi ya robo fainali, siku ya Jumamosi, mchezaji wa zamani wa Argentina Diego Maradona amesema kuwa ushindi wao dhidi ya Colombia mechi ya hatua ya mchujo ni ulaghai.

Maradona alimlaumu refa wa mechi hiyo kwa kuipendelea Uingereza dhidi ya Colombia.

Akizungumza katika programu yake ya kila jioni ya katika idhaa ya televisheni ya Telesur inayomilikiwa Venezuela, Maradona aliongeza, ''Ukimchunguza, au kumfanyia utafiti, utagundua kuwa hastahili kusimamia mechi. Utakuta ni raia wa Marekani, ni kinaya''.

Maradona alihisi kuwa Geiger angemwadhibu Harry Kane kwa kumchezea rafu kiungo wa Colombia Carlos Sanchez lakini badala yake aliipa Uingereza penalty iliyomruhusu Kane kuiweka Uingereza kifua mbele.

Lakini leo ameandika kwenye mitandao ya kijamii kuomba radhi.

"Niliyasema mambo kadha na, nakiri, baadhi yalikuwa hayakubaliki," ameandika.

"Ninaiheshimu sana kazi - ambayo si rahisi - ambayo taasisi hiyo (Fifa) na waamuzi huifanya," ameongeza.

Nahodha wa Colombia Radamel Falcao pia ameungana na Maradona kueleza kuwa walionewa kwenye mechi hiyo na refa Geiger. Falcao anahoji kuwa maamuzi yote yaliegemea upande wa Uingereza.

"Ni aibu," alisema Falcao.

Haki miliki ya picha Getty Images

Geiger alionekana kuwa na kazi ngumu alipokuwa akisimamia kipute hicho mjini Moscow, kabla ya Uingereza kushinda kupitia penalti.

"Hali nzima ilituathiria na mabo yalikuwa dhidi yetu," alizidi Falcao.

Maradona alipigwa picha kwenye mechi hiyo akiwa amevalia jezi ya Colombia na pia alinaswa baadaye akisherekea goli la kusawazisha mechi la beki Yerry Mina.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Colombia walipinga uamuzi wa mwamuzi kuwapa England penalti ambayo Harry Kane alifunga na kuwapa uongozi

Shirkilisho la soka la Fifa limelaani tamko la Maradona na kulitaja kuwa ''lisilofaa''.

Fifa imeongeza kuwa imestajaabishwa kusikia kauli hizo kutoka mchezaji aliyechangia historia ya soka duniani.

"Fifa inapinga vikali shtuma dhidi ya utendakazi wa maafisa wa mechi ulioonekana chanya katika mechi ngumu na yenye hisis nyingi.