Kombe la Dunia 2018: Mwandishi aacha kazi Rwanda kwa sababu ya Messi na Argentina

Joe

Wakati mashabiki wa soka duniani wakiendelea kufuatilia yanayojiri Kombe la Dunia Urusi, kwa mwandishi mmoja Rwanda, ni wakati wa kulipia gharama kutokana na ahadi aliyoitoa.

Rutamu Elie Joe alikuwa amewaahidi wasikilizaji akiwa hewani kwamba angeacha kazi iwapo Argentina wangekosa kushinda Kombe la Dunia mwaka huu.

Ndoto yao ilizimwa Jumamosi walipolazwa 4-3 na Ufaransa.

Mwandishi huyo anasema alitoa ahadi siku ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia na kusema ''Mwaka huu ndio Lionel Messi atachukua Kombe la Dunia.''

''Messi asipochukua Kombe la Dunia basi mimi naachana na hii kazi yangu ya utangazaji wa mpira pamoja na kufanya kazi katika kituo hiki cha redio."

Anasema kwake alikuwa analichukulia kama jambo la kawaida, kutoa ahadi tu lakini baadaye amekuja kuwajibishwa.

''Mimi nilikuwa nafikiria ni kawaida tu kama kipindi cha kawaida tu ambacho kimepita kumbe watu wamekirekodi na wakasalia kimya''.

"Mechi za Kombe la Dunia, mechi ya kwanza Iceland ilitoka droo na Argentina ndio nikaanza kuona sasa zile kanda zikianza kusambaa mitandaoni kila mahali na hapo ndipo watu walianza kuuliza kwamba nilisema Messi atakuwa mshindi kwenye Kombe la Dunia sasa wanatazamia ahadi yangu itimie.''

"Mechi ya pili Croatia ikafunga magoli matatu wakasema ahh…aga mapema basi acha kazi ulitwambia kwamba Messi asipochukua Kombe la Dunia utaacha kazi yako''

"Hapo ndipo nilipoanza kupingana na umma, raia walikuwa wakisema Messi akitoka ondoka.

Kwa hivi sasa nitaacha kazi yangu."

Joe anasema kwamba hii si mara yake ya kwanza kutoa ahadi kama hiyo.

''Kuna wakati nilitoa ahadi nilipokuwa msemaji wa timu ya Sunrise ya daraja la kwanza nikasema Espoir haiwezi kuishinda mechi mbili, ikinishinda mechi mbili mfululizo mimi nitaiacha kazi hiyo," anasema.

Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Joe akitangaza mpira

"Na kwa kweli Espoir ilijitahidi na wakanifunga mechi ya pili kwa hivyo tangu siku hiyo nilitoka kwenye Sunrise lakini ni ahadi niliongea hata mimi mwenyewe sikutarajia kama itafika hapa na kusambaa mitandaoni kama hivi."

Lakini kama kawaida yangu ndio hivyo michuano ya Kombe la Dunia inamalizika tarehe 15 Julai.

"Nitakuwa nimemalizika miaka tisa kwenye hii kazi ya kutangaza mpira na vipindi mbalimbali vya michezo basi nitaiweka chini niendelee na mambo mengine."

Mwandishi huyo amesema anatarajia kuanza kufanya kazi tofauti sasa.

"Kuna vitu vingi tayari nilikuwa nafaa kufanya. Kuna vitu nilivyokuwa nimeshaanza kufanya kama kuuza wachezaji, ndio kazi ambayo kwa hivi sasa naweza kufanya kwa makini kwa hivi sasa."