Kombe la Dunia 2018: Kocha wa Uhispania Fernando Hierro ajiuzulu kabla ya kumaliza mwezi

Fernando Hierro Haki miliki ya picha EPA
Image caption Fernando Hierro alishinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara tatu akiwa na Real Madrid

Fernando Hierro, aliyewaongoza Uhispania katika Kombe la Dunia 2018, amejiuzulu wadhifa wake kama kocha wa muda na taarifa zinasema hatarejelea kazi yake ya awali ya mkurugenzi wa michezo.

Hierro alipewa kazi ya kuwa kocha wa muda baada ya kocha wa taifa hilo Julen Lopetegui kufutwa kazi mkesha wa kuanza michuano hiyo.

Hata hivyo, mabingwa hao wa dunia wa mwaka 2010 waliondolewa kwenye michuano hiyo kupitia mikwaju ya penalti na wenyeji Urusi hatua ya 16 bora.

Hierro, 50, ameamua kutafuta mambo mengine ya kufanya, kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Uhispania.

Taarifa imesema mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid amekataa kurejea katika wadhifa wake wa awali kama mkurugenzi wa michezo na kuamua "kuchukua changamoto mpya."

Lopetegui alifutwa kazi siku mbili kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Ureno baada yake kutangazwa kuwa meneja mpya wa Real Madrid, wadhifa uliobaki wazi baada ya kujiuzulu kwa Zinedine Zidane.

Lopetegui aliteuliwa meneja wa Uhispania mwaka 2016 baada ya kustaafu kwa Vicente del Bosque na alikuwa hajashindwa hata mechi moja kufikia wakati wa kuondoka kwake.

Uhispania waliongoza Kundi B chini ya Hierro katika Kombe la Dunia. Hata hivyo, walikuwa wametoka sare ya 3-3 dhidi ya Ureno baada ya kufungwa dakika za mwisho, na walikuwa nyuma 2-1 dhidi ya Morocco kabla ya kusawazisha dakika za mwisho.

Baada ya kutupwa nje kwao Urusi, Hierro alisema aliamua kuwajibika kutokana na kushindwa kwao kusonga.

"Tulijitolea kadiri ya uwezo wetu lakini hii ni soka," alisema.

"Sifikiri unaweza kuzungumzia kuhusu timu kusambaratika au kuporomoka. Kuna mstari mwembamba sana kati ya kushinda na kushindwa."