Cristiano Ronaldo atua Juventus kutoka Real Madrid

Ronaldo is Real Madrid's all-time record goalscorer

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Ronaldo alijiunga na Real akitokea Manchester United kwa pauni milioni 80 mwaka 2009

Mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amejiunga na Juventus, kwa mujibu wa klabu hiyo ya Uhispania.

Inaaminiwa kuwa mkataba wa thamani ya pauni milioni 105 uliafikiwa kati ya vilabu hivyo viwili, ambao utamwezesha mchezaji huyo wa miaka 33 kufikisha kikomo taaluma yake wa miaka 10 huko Bernabeu.

Ronaldo alishinda mataji manne ya ligi kuu huko Real lakini hakuwa na uhusiano mzuri na rais wa klabu Florentino Perez.

"Kwa Real, Cristiano Ronaldo siku zote atakuwa mchezaji muhimu," ilisema taarifa ya klabu.

"Real Madrid inataka kuonyesha heshima kwa mchezaji ambaye amedhihirisha kuwa ndiye bora zaidi duniani na ambaye amekipa sifa kubwa klabu katika historia ya mpira.

"Real Madrid kawaida itakuwa nyumbani kwako."

Ronaldo alijiunga na Real akitokea Manchester United kwa pauni milioni 80 mwaka 2009, na kufunga jumla ya mabao 451 na kushinda tuzo la Ballon D'Or analopewa mchezaji bora zaidi duniani mwaka 2008, 2013, 2014, 2016 na 2017.

Amewasaidia kushinda ligi ya mabingwa misimu minne kati ya mitano akifunga katika fainali ya mwaka 2014 na 2017.

Chanzo cha picha, .

Maelezo ya picha,

Alifunga jumla ya mabao 451 na kushinda tuzo la Ballon D'Or analopewa mchezaji bora zaidi duniani mwaka 2008,

Kipi kinatarajiwa kufuata?

Licha ya kutawala mechi za Ulaya, Real walikuwa na wakati mgumu ndani ya Uhispania wakimaliza pointi 17 nyuma ya mabingwa Barcelona.

Real wako makini kukiboresha kikosi chao chini ya meneja mpya Julen Lopetegui na washindi hao mara 33 wa La Liga pia wametajwa kumwinda mshambuliaji wa Paris St-Germain raia wa Brazil Neymar.

Maelezo ya picha,

Ronaldo alifunga magoli mawili katika fainali ya ligi ya mabingwa 2017 dhidi ya Juventus

Hata hivyo itakuwa hatua ambayo itakumbwa na utata kwa sababu Neymar aliwachezea mahasimu wa Real, Barcelona kabla ya kujiunga na Paris St-Germain kwa rekodi ya pauni milioni 200.

Raal nao wamehusishwa na mshambualiaji mwingine wa PSG Kylian Mbappe, mchezaji wa miaka 19 ambaye ameisaidia Ufaransa kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia.