'Africa United': Mataifa ya Afrika yaliyochangia wachezaji timu ya taifa ya Ufaransa Kombe la Dunia 2018

Paul Pogba, N'Golo Kante na Blaise Matuidi wakifanya mazoezi uwanja wa Glebovets mjini Istra Magharibi mwa Moscow

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Paul Pogba, N'Golo Kante na Blaise Matuidi wakifanya mazoezi uwanja wa Glebovets mjini Istra Magharibi mwa Moscow

Ufaransa watakutana na Croatia katika fainali ya Kombe la Dunia Urusi Jumapili na ingawa hakuna timu kutoka Afrika iliyofika hatua ya muondoano, wengi wamekuwa wakilitaja taifa hilo kama Africa United.

Hii ni kutokana na kuwepo kwa wachezaji wengi wenye asili ya bara Afrika.

Kwa jumla, kikosi cha Ufaransa kina wachezaji 14 ambao wana mzazi mmoja au wazazi wote wawili wanaotoka Afrika.

Wachezaji hawa ni kina nani?

Kikosi kamili cha Ufaransa

Walinda lango: Hugo Lloris (Tottenham Hotspur), Steve Mandanda (Marseille), Alphonse Areola (Paris Saint-Germain)

Mabeki: Lucas Hernandez (Atletico Madrid), Presnel Kimpembe (Paris Saint-Germain), Benjamin Mendy (Manchester City), Benjamin Pavard (Stuttgart), Adil Rami (Marseille), Djibril Sidibe (Monaco), Samuel Umtiti (Barcelona), Raphael Varane (Real Madrid)

Viungo wa kati:N'Golo Kante (Chelsea), Blaise Matuidi (Juventus), Steven N'Zonzi (Sevilla), Paul Pogba (Manchester United), Corentin Tolisso (Bayern Munich)

Washambuliaji:Ousmane Dembele (Barcelona), Nabil Fekir (Lyon), Olivier Giroud(Chelsea), Antoine Griezmann (Atletico Madrid), Thomas Lemar (Monaco), Kylian Mbappe (Paris Saint-Germain), Florian Thauvin (Marseille).

Chanzo cha picha, Reuters

Wachezaji hawa wanatokea wapi?

1. Steve Mandanda, 33 (DR Congo)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Steve Mandanda

Ni mlinda lango ambaye huchezea klabu ya Marseille ya Ufaransa. Alizaliwa mnamo 28 Machi 1985 mjini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati huo ikiitwa Zaire na jina lake kamili ni Steve Mandanda Mpidi. Ana ndugu watatu wadogo wote ambao ni walinda lango, na wawili kati yao hucheza soka ya kulipwa.

Mandanda huishi Marseille na amepewa jina la utani 'Frenchie' na jamaa zake kutokana na uamuzi wake wa kuamua kuichezea Ufaransa badala ya DR Congo.

Amekuwa kipa wa akiba kwa sasa nyuma ya Hugo Lloris katika timu ya taifa.

Mandanda aliamua kuwa mlinda lango kibahati akiwa na miaka tisa. Kocha wake wa zamani katika timu ya vijana Evreux anasema wakati mmoja alikuwa anatembea wachezaji wengine wakifanya mazoezi. „Nilimuona akinitazama kwa macho makubwa, na akaniambia: 'iwapo nitacheza kandanda, basi ninataka kuwa mlinda lango kwa sababu (ukiwa kipa) hauhitajiki kukimbia!"

Ndiye mkubwa katika familia ya watoto watano wa kiume na alikuwa akiwatunza utotoni wazazi wao walipoenda kutafuta kazi.

Aliwahi kuichezea Crystal Palace ambapo alitatizika sana alipojaribu kuihama klabu hiyo.

2. Presnel Kimpembe, 22 (DR Congo na Haiti)

Chanzo cha picha, NurPhoto

Maelezo ya picha,

Kylian Mbappe na Presnel Kimpembe

Huyu ni beki wa Paris Saint-Germain ya Ufaransa.

Kimpembe alizaliwa 13 Agosti 1995 karibu na Beaumont-sur-Oise. Babake ni wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mamake alitokea Haiti.

Alianza kucheza soka ya kulipwa 17 Oktoba 2014 alipoingia nafasi ya Thiago Motta.

Alichezeshwa pia badala ya Thiago Silva mechi ya marudiano 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ugenini Real Madrid na kocha wa sasa wa Arsenal Unai Emery hatua iliyowashangaza wengi.

Ni mchezaji anayejiamini sana na hilo hujidhihirisha ndani na nje ya uwanja.

Alichezeshwa mara ya kwanza timu kuu ya taifa Ufaransa wakati wa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Bulgaria na Uholanzi Oktoba 2016 baada ya Eliaquim Mangala kuumia.

Nyota wa zamani wa Ufaransa na Arsenal na Chelsea William Gallas amemweleza kama "tumaini la Ufaransa siku za usoni".

3. Samuel Umtiti, 24 (Cameroon)

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni mchezaji wa miaka 24 ambaye alizaliwa mnamo 14 Novemba mwaka 1993 mjini Yaounde, Cameroon. Mamake ni Annie Ngo Um lakini babake hajulikani ni nani. Ana ndugu kwa jina Yannick Umtiti. Yeye kwa kawaida huwa ni beki wa kati.

Ni mchezaji mrefu kwa kimo, kimo chake ni futi sita (1.83m) jambo ambalo huenda lilimsaidia katika kufunga bao la kichwa dhidi ya Ubelgiji ambapo alikuwa anakamiliana na mchezaji mwingine mrefu wa kimo anayefahamika sana kwa mipira ya kichwa, Marouane Fellaini.

Kutokana na kwamba alizaliwa Cameroon, ni mchezaji ambaye alikuwa na fursa ya kuichezea timu ya taifa ya Cameroon. Ana uraia wa Cameroon na Ufaransa.

4. Djibril Sidibé, 25 (Mali)

Ni beki wa kati ambaye huitwa kwa utani "Tonton" ("Mjomba") na Kylian Mbappé, na kwa sasa huchezea klabu ya AS Monaco.

Wazazi wake walitokea Bamako, Mali ingawa alilelewa Troyes nchini Ufaransa.

Alizaliwa 29 Julai 1993. Ni mchezaji ambaye ni mkabaji kamili lakini wakati mwingine hutumiwa safu ya kati.

Alianza uchezaji wake katika klabu ya Troyes akiwa na miaka minane na alichezea Lille kabla ya kuhamia Monaco.

Wakati mmoja aliulizwa kuhusu kuchezea Mali, ambapo alisema kocha wa Mali wa 2012-2013 Patrice Carteron, aliwasiliana naye wakati mmoja. "Wakati huo nilikuwa ndio nimewasili tu Lille na sikuchezeshwa sana.

Nilitaka nafasi kuchezea The Eagles. Wazazi wangu wanatokea Bamako, sawa na jamaa wengine wangu, na wangelifurahia mimi kuchezea Mali.

"Nilikuwa naichezea timu ya vijana ya Ufaransa, lakini nilifahamu kwamba kama ningekubali kuchezea Mali, ningejitenga na Lille klabu ambayo nilitaka kupata fursa ya kucheza muda zaidi. Hivyo niliweka klabu mbele."

"Familia yangu waliniruhusu nifanye uamuzi wangu bila kunishinikiza."

Alichezea timu ya taifa ya Mali mara ya kwanza 1 Septemba 2016 mechi ya kirafiki dhidi ya Italia.

5. Adil Rami, 32 (Morocco)

Adil Rami ni beki wa kati wa asili ya Morocco aliyezaliwa 27 Desemba 1985.

Kwa sasa huchezea klabu ya Sevilla ya Uhispania.

Alianza uchezaji wake akiwa na miaka tisa na klabu yake ya kwanza kujiunga nayo ilikuwa Étoille Fréjus Saint-Rafaël. Alianza kucheza soka ya kulipwa kirasmi msimu wa 2003/04. Mwanzoni alikuwa anacheza kama mchezaji wa mshambuliaji wa safu ya kati lakini baada ya mwenzake kuumia kwenye timu akasukumwa safu ya ulinzi.

Alifana katika ukabaji na akawavutia Lille. Alichezea Valencia ya Uhispania na AC Milan ya Italia kabla ya kuhamia Sevilla.

6. Benjamin Mendy, 23 (Senegal)

Ni mchezaji mcheshi sana mwenye asili ya Senegal ambaye kwa sasa hucheza kama beki wa kushoto katika klabu ya Manchester City.

Alicheza ligi kuu ya Ufaransa kwa misimu minne kabla ya kuhamia Manchester kwa bei iliyovunja rekodi ya dunia ya kununuliwa kwa beki ambapo alinunuliwa £52m.

Mendy anatokea kusini mwa Paris na alianza uchezaji wake soka ya kulipwa klabu ya Le Havre kabla ya kuhamia Marseille na baadaye kujiunga na Monaco.

Alichezea timu timu ya taifa ya Ufaransa mara ya kwanza 25 Machi 2017 mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Lixembourg ambapo walishinda 3-1 ugenini.

7. Paul Pogba, 25 (Guinea)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Paul Pogba, N'Golo Kantena Blaise Matuidi wakifanya mazoezi Urusi

Jina lake la utani ni La Pioche, maana yake Shoka.

Paul Labile Pogba alizaliwa Lagny-sur-Marne, Seine-et-Marne Ufaransa lakini wazazi wake wanatokea Guinea.

Ni Mwislamu na ana ndugu wawili wakubwa pacha waliozaliwa Guinea ambao ni wachezaji soka pia. Utotoni alikuwa anaipenda sana Arsenal.

Alianza uchezaji wake akiwa na miaka sita akichezea US Roissy-en-Brie na alikaa nao misimu sita kabla ya kuhamia US Torcy alikokaa miaka saba na wakati mmoja akawatumikia kama nahodha wa wachezaji wa chini ya miaka 13.

Alihamia Le Havre na baadaye Manchester United kabla ya kuuzwa Juventus.

Alirejea tena Manchester Agosti 2016 kwa uhamisho uliogharimu £89.3) ambao ulivunja rekodi ya awali ya dunia iliyokuwa imewekwa na Gareth Bale.

Alichezea timu ya taifa mara ya kwanza 2013 dhidi ya Georgia mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia la mwaka 2014.

Soma zaidi kumhusu hapa: Chimbuko la mchezaji Paul Pogba

8. Corentin Tolisso, 23 (Togo)

Kiungo huyu wa kati huichezea Bayern Munich wa Ujerumani. Alizaliwa 3 Agosti 1994 na wazazi wanatokea Togo.

Alilelewa Thizy, katika eneo la Rhône-Alpes nchini Ufaransa na hukumbuka maisha ya ufukara ya utoto wake.

"Nafikiri kuendelea kunyenyekea na kuishi maisha ya kawaida ni jambo muhimu sana. Babangu alikuwa mtu wa posta; mamangu bado hufanya kazi kama mkurugenzi wa kituo cha kuwatunza walemavu. Nafahamu nilikotoka," amenukuliwa na gazeti la Guardian la Uingereza.

Alianza uchezaji wake katika akademi ya Lyon ambao alijiunga nao akiwa na miaka 13.

Alichezeshwa mara ya kwanza Agosti 2013 dhidi ya Nice ligi kuu ya Ufaransa mechi ambayo walishinda 4-0.

Alijiunga na Bayern Munich msimu uliopita.

Ingawa alizaliwa Ufaransa, alikuwa pia anaweza kuiwakilisha Togo na kocha wa timu ya taifa ya Togo mwaka 2016 Claude Le Roy alikuwa amefichua kwamba angejaribu kumshawishi kuwachezea. Tolisso alikiri uhusiano wake na Togo lakini akaamua kuchezea Ufaransa, akisema: „Nilizaliwa hapa na kulelewa hapa."

Alichezea timu ya taifa ya Ufaransa mara ya kwanza Machi 2017 dhidi ya Uhispania nyumbani mechi ambayo walilazwa 2-0.

9. N'Golo Kanté, 27 (Mali)

Chanzo cha picha, Getty Images

Wazazi wake wanatokea Mali. Mchezaji huyu alizaliwa Paris 29 Machi, 1991 na akaanza kucheza soka akiwa na miaka minane JS Suresnes. Alikaa huko kwa karibu mwongo mmoja hadi mwaka 2013 alipojiunga na Caen na baadaye akahamia Leicester City kwa £5.6m mwaka 2015 na kuwasaidia kushinda ligi msimu wa 2015/16.

Uchezaji wake uliwavutia Chelsea waliomnunua kwa £32m Julai 2016 kwa mkataba wa miaka mitano. Aliwasaidia Chelsea kushinda ligi na Desemba mwaka huo gazeti la L'Equipe lilimuorodhesha kuwa wa sita bora duniani kwa uchezaji. Mwaka huo alitawazwa pia mchezaji bora wa mwaka chaguo la wachezaji wa kulipwa Uingereza.

Wazazi wa Kante walihamia Ufaransa kutoka Mali mwaka 1980 na alilelewa katika nyumba ndogo eneo la Rueil-Malmaison, Hauts-de-Seine. Jina lake linatokana na Mfalme Ngolo Diarra wa ufalme wa Bamana.

Eden Hazard humuita "panya" na Michael Ballack alimweleza kama "nzi msumbufu". Ni mchezaji imara sana safu ya kati na hufanikiwa sana kuvuruga uchezaji wa timu pinzani.

Amefananishwa sana na uchezaji wa Claude Makélélé.

Alianza kuchezea timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2016.

10. Blaise Matuidi, 31 (DR Congo na Angola)

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Matuidi akilalamika baada ya kuchezewa visivyo mechi dhidi ya Ubelgiji

Blaise Matuidi alizaliwa 9 Aprili 1987 Toulouse na kukulia eneo la Fontenay-sous-Bois mjini Paris pamoja na ndugu zake wanne.

Ingawa Mamake, Élise Rivelino ni wa asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na babake Faria Rivelino anatokea Angola. Babake alitoroka mapigano ya Angola miaka ya 1980 kuelekea DR Congo na kisha wakahamia mji wa Toulouse, Ufaransa.

Matuidi ni mzungumzaji mzuri wa lugha ya wakoloni wa Angola, Ureno pamoja na Ufaransa.

Mnamo mwaka wa 2006, kiungo huyo wa kushoto alialikwa na timu ya taifa ya soka ya Angola kuiwakilisha, lakini alikataa ombi hilo. Hata hiyo alijitetea kuwa uamuzi huo haukuashiria amekata uhusiano na asili yake.

Aidha, mwaka wa 2010, Angola ilipoandaa Kombe la mataifa bingwa Afrika, Matuidi alizuru taifa hilo huku akihoji kuwa, licha ya kuwa Mfaransa, anahisi kuwa Muangola zaidi.

Ukurasa wake wa soka ulianzia klabu za wachezaji chipukizi US Fortenay-sous-Bois, CO Vincennois na Créteil.

Baada ya kupata uzoefu zaidi, msimu wa 2004/05 alitua Troyes AC na kuisaidia kupandishwa daraja hadi Ligue 1. Alitengana na klabu hiyo pindi walipolishwa upanga hadi daraja la nchini mwaka 2006/07 na kutua Matuidi AS Saint-Étienne.

Bidii yake ilimzolea ufanisi na kumwezesha kufika hadi klabu ya Paris Saint-Germain Julai 2011. Mwaka uliopita alijiunga na Juventus.

Safari yake na timu ya Ufaransa ilianza na kikosi cha wachezaji wasiopungua umri wa miaka 21 aliowachezea kabla ya kualikwa kweye kikosi cha timu ya taifa mwezi Septemba 2010.

11. Steven Nzonzi, 29 (DR Congo)

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Nabil Fekir, Steven Nzonzi, Thomas Lemar na Presnel Kimpembe wakitaniana wakati wa mazoezi Julai 12 mjini Moscow, Urusi

Steven N'Kemboanza Mike Nzonzi kwa kifupi Steven Nzonzi alizaliwa 15 Desemba 1988 La Grenne Colombes, Paris, Ufransa kwa Baba mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mama Mfaransa.

Alianza safari yake 1998, na timu ya Racing Paris.

Kiungo huyu mkabaji alijiunga na klabu ya Amiens SC 2007 na baada ya kipaji chake kujitetea, alisajiliwa na Blackburn Rovers ya England aliyoitumikia kati ya 2009-2012.

Licha ya Blackburn kulishwa upanga 2012, alisalia Uingereza kwa kuhamia klabu ya Stoke City.

Ingawa amekuwa aking'aa, Steven Nzonzi hakuweza kuwavutia wakufunzi wa Ufaransa baada ya kuhamia England mapema katika enzi zake.

Kutokana na hali ya Ufaransa kuwa mkwasi wa viungo wakabaji, Nzonzi hakuweza kuitwa kikosini.

Licha ya changamoto hizo, alidumisha subira ikiwemo kukataa mwaliko wa Jamhuri ya Congo kuiwakilisha Kombe la Afcon Afrika Kusini mnamo mwaka wa 2012 na kuamua kusubiri nafasi katika kikosi cha Ufaransa.

Milango ya fursa na mafanikio ilianza kufunguka alipotua Sevilla ya Uhispania 2015.

Lakini macho makali ya kocha Didier Deschamps yalipomwahi, alijumuishwa kwa mara ya kwanza mwezi Novemba mwaka wa 2017 katika mihuano ambayo Ufaransa ililazwa 2-0 na Wales kabla ya kutoka sare 2-2 na Ujerumani.

Baada ya kuiwakilisha Ufaransa kwa wachezaji wasiozidi miaka 21, alikabidhiwa jezi la taifa hilo tena Kombe la Dunia Urusi 2018 na kocha Deschamps ambaye hajapoteza matumaini kwa nyota huyo.

Amejiweka vyema kwenye mpangilio wa Sevilla kiasi kwamba kocha wao wa zamani Jorge Sampaoli alizoea kumuita "Pweza", kutokana na kujikita kwake na kuwa kitovu cha timu.

Alikaribia kuhamia PSG mwaka jana.

12. Kylian Mbappé, 19, (Cameroon na Algeria)

Chanzo cha picha, Getty Images

Mchezaji huyu alizaliwa mnamo 20 Desemba 1998 katika familia ya wachezaji eneo la Bondy kaskazini mashariki mwa Paris, Ufaransa. Jina lake kamili ni Kylian Mbappe Lottin.

Babake Wilfried Mbappé alitoka Cameroon, ingawa ana mizizi pia Nigeria, na mamake Fayza Mbappé Lamari ni wa asili ya Algeria.

Wawili hao walikutana Ufaransa. Wilfried alikuwa amekimbilia Ufaransa kama mkimbizi na akamuoa Fayza ambaye alikuwa tayari ni raia wa Ufaransa katika juhudi za kutaka kupata idhini ya kusalia Ufaransa.

Fayza alikuwa mchezaji stadi wa mpira wa handiboli naye Wilfried ni mkufunzi wa michezo mbalimbali.

Babake alikuwa ndiye mkufunzi wake utotoni, na anasema kipaji chake kilianza kuonekana akiwa na miaka sita pekee. Kwa sasa, ndiye wakala wake.

13. Ousmane Dembélé, 21 (Mauritania)

Dembele alizaliwa 15 Mei 1997 mjini Vernon, Kaskazini Ufaransa na wahamiaji kutoka Mauritania, akiwemo babake Ousmane na mamake Fatimata Dembele.

Mapenzi ya soka ya Ousmane Dembele yalianza akiwa mdogo na kumfanya apoteze hamu ya masomo. Baada ya kufahamu hayo, wazazi wake waliwekeza katika uimarishaji wa kipaji chake cha Soka.

Alipokuwa umri wa miaka 6, aliondoka na mamake mjini Vernon na kuelekea Kaskazini Mashariki hadi mji wa Rennes kukutana na mjombake, Badou Sambague aliye alianza kumnoa Dembele.

Safari ya soka ya Dembele ilishika kasi na alitua timu ya Madeleine Evreuex mnamo 2004.

Mamake nyota huyu Fatimata Dembele ndiye anahusika pakubwa katika mazungumzo kuhusu usajili wake na mikataba kati yake na vilabu vya soka.

Baadaye alijiunga na Rennes ya Ufaransa akiwa na miaka 13, kabla ya kuihama na kutua Dortmund kwa Euro milioni €15m 2016.

Msimu wa 2015/2016, akiwa Rennes, Dembele alifunga mabao 10 na kumpiku Thierry Henry kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kufanya hivyo.

2017, aligonga vichwa vya habari baada ya Mabingwa wa Uhispania Barcelona kumtia kapuni kwa euro milioni €105m na kusajili mkataba wa miaka 5.

Nyota huyu mwenye umri wa miaka 21, mpaka sasa ameifungia Ufaransa mabao mawili mpaka sasa na tangu alipoiwakilisha kwa mara ya kwanza walipoifunga Italia 3-1 mechi ya kirafiki Septemba 2016.

Samuel Umtiti humuita "le Moustique" - "Mbu" - kutokana na uwezo wake wa kupiga wachezaji chenga uwanjani.

14. Nabil Fekir, 24 (Algeria)

Kiungo mshambuliaji wa Ufaransa Nabil Fekir alizaliwa mnamo 18 Julai 1993 mjini Lyon, Ufaransa na wazazi wenye asili ya Algeria.

Aliwahi kuzua fujo baada ya kuchagua kuiwakilisha Ufaransa badala ya Algeria licha ya kuwa na uraia wa Ufaransa na Algeria kwani babake Mohammad Fekir ana asili ya Algeria.

Akiwa na miaka 12, Fekir aliingia timu ya vijana wasiozidi miaka 12 ya Olympique Lyonnais. Aliachwa na timu hiyo na baadaye akaondoka hadi timu ndogo ya Vaulx-en-Velin.

Nabil Fekir aliiwakilisha Lyon B kutoka 2011 na mnamo mwaka wa 2013, aliitwa kikosi cha Lyon kwenye ligi.

Mnamo 2014 na 2015, aliionyesha uwezo wake kikosi cha Ufaransa na baada ya Maxime Gonalons, nahodha wa Lyon kujiunga na AS Roma 2017,alikabidhiwa Unahodha.

Amebandikwa jina 'Messi wa Lyon' na amejizolea sifa kutoka Arsenal na Liverpool waliotaka kumsajili.

Kufikia sasa ameiwakilisha Ufaransa mechi 10 kabla ya kujumuishwa kikosi cha Kombe la Dunia.

Pia, amewahi kuiwakilisha timu ya Ufaransa kwa wachezaji wasiopungua miaka 21.

Baada ya hapo, Fekir alihamia Saint-Priest. Na katika muda huo, timu nyingi zililenga kumsajili lakini Fekir alidumisha azma yake ya kutua Lyon. Lyon haikuzubaa kumsajili na ilimtia kibindoni.

Ni katika klabu hiyo ndio aliweza kutuzwa mchezaji bora mwenye umri mdogo Ligue 1 pamoja na kujinyakulia nafasi katika timu bora ya msimu wa 2015.

Ingawa kocha wa Algeria Christian Gourcuff alilenga kumshirikisha kikosini, hakuweza kumshawishi kiungo huyo.

Mnamo Machi mwaka wa 2015, Fekir alicheza mechi yake ya kwanza ya Ufaransa na ilipofika Juni mwaka huo, alifunga goli lake la kwanza la timu ya taifa.