Maurizio Sarri azinduliwa rasmi Chelsea, huku Xhedan Shaqiri akinyakuliwa na Liverpool

Maurizo Sarri Haki miliki ya picha Getty Images

Meneja wa zamani wa Napoli amezinduliwa baada ya Antonio Conte kutemwa.

Maurizio Sarri amewaahidi mashabiki wa klabu hiyo mpira wa kuburudisha tofauti na mpira wa nguvu na ukabaji uliozoeleka Chelsea.

Carlo Ancelotti amejaza pengo la meneja huyo wa miaka 59 aliyeiongoza Napoli kumaliza nyuma ya mabingwa wa ligi ya Italia, Juventus waliowazidi kwa alama nne pekee.

Napoli ni timu ya kwanza kuogofya Juventus iliyotamalaki ligi hiyo kwa kuibeba misimu saba mfululizo.

"Ni mwanzo mpya wa kupendeza katika taaluma yangu,"alisema Sarri.

"Natumai tunaweza kuwatunuku mashabiki wetu kwa mpira wenye mvuto na kuwania mataji mbalimbali mwisho wa msimu, ndio namna klabu inayostahili."

Hizi huenda sio semi tu za Sarri kwani amethibitisha kugeuza mchezo wa Napoli na kuboresha ushambulizi wa klabu hiyo.

Napoli ilifunga mabao 94 msimu wa 2016-17 na kuwa timu yenye mabao zaidi Seria A baada ya kipindi kirefu.

Vile vile, Napoli ilipachika mabao 251 ya ligi miaka mitatu akikalia kiti cha unahodha.

Sarri ni wa kumi na tatu kusajiliwa kuifunza Chelsea na Muitalia wa sita tangu bilionea wa Urusi Roman Abramovich kuinunua 2003.

Wengine ni Gianluca Vialli, Claudio Ranieri, Ancelotti, Roberto di Matteo na Conte.

Je maurizio Sarri ni nani?

Alitua Napoli 2015 baada ya kuipandisha Empoli hadi ligi kuu ya Italia.

Ingawa hajawahi kuzoa taji, Chelsea ndio timu ya kwanza nje ya Italia atakayoifunza.

Pia, Sarri hajafanikiwa akiwa mchezaji na baada ya kukwama, aligeuka kufanya kazi kwenye biashara ya sarafu za kigeni.

Ingawa the blues wamemsaini kuwaisidia kwenye Kombe la Champions, Sarri pia amekuwa na wakati mgumu kuisaidia Napoli kufika hatua ya mchujo Kombe hilo.

Msimu uliopita, walimaliza wa tatu kwenye kundi lao nyuma ya Manchester City na Shakhtar Donetsk.

Xherdan Shaqiri aingia Anfield

Haki miliki ya picha Getty Images

Wakati huohuo Liverpool imezidi kuimarisha safu yake ya ufungaji tayari kwa msimu ujao kwa kumtia kapuni nyota wa Uswizi Xherdan Shaqiri baada ya kuwanyakua viungo wa Monaco Fabinho, na Naby Keita kutoka RB Leipzig.

Licha ya kulishwa upanga pamoja na klabu ya Stoke City kutoka ligi ya Premier msimu uliopita, haijaizuia Liverpool kumnasa Shaqiri kwa pauni milioni £13m na kutia wino kandarasi ya miaka 5.

Shaqiri mwenye umri wa miaka 26, alikuwa mfungaji bora wa Stoke akiwa na mabao 8 baada ya kujiunga nao kutoka Inter Milan Agosti 2015.

Shaqiri aliwahi kutwaa taji la Champions League akiwa Bayern mnamo 2013.

Shaqiri alisajili bao Kombe la dunia dhidi ya Serbia ingawa timu yake iliondolewa hatua ya mchujo na Sweden.

"Miaka chache iliyopita, nilitarajiwa kufika hapa lakini sikufaulu. Nafurahi sana hatimaye imetimia na nimetua. Nataka kujiimarisha, kuwa pamoja na wachezaji bora na kushinda mataji. "

"Ni timu kubwa yenye historia, wachezaji tajika na kocha hodari."

Aidha, nyota huyo amejizolea sifa kutoka Meneja Jurgen Klopp.

Mada zinazohusiana