Kombe la Dunia2018: Nani atakayewika kati ya Ufaransa na Croatia?

Ufaransa itamtegemea Mbappe huku Croatia wakimtegemea Modric Haki miliki ya picha Getty Images

Croatia itakwaruzana na Ufaransa uwanja wa Luzhniki Moscow Jumapili ikilenga kushinda taji kwa mara yake ya kwanza nao wapinzani wake Croatia wakishiriki fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya tatu.

Aidha, wanasaka taji lao la pili Kombe la Dunia baada ya kulinyakua miaka 20 iliyopita. mjini Paris.

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps, naye huenda akaweka historia kwa kuwa mtu wa tatu kubusu Kombe la Dunia akiwa mchezaji na mkufunzi.

Kinyume na mpinzani wake, Zlatko Dalic, ameinoa Croatia miezi 9 pekee lakini amebakisha dakika 90 kuweka historia kwa kuwaongoza kuinua Kombe la Dunia licha ya kutopigiwa upatu.

Croatia: 'Kudumisha ndoto'

Taifa lenye idadi ya watu milioni 4.17, huenda wakaonekana wachache lakini rekodi ya taifa lenye idadi chache ya watu kuwahi kubeba Kombe la Duia mpaka sasa ni Uruguay, walioondoka na ubingwa 1930 wakiwa na idadi ya watu milioni 1.7

Ingawa wanaorodheshwa nafasi ya 20 jedwali la FIFA, kikosi cha Dalic ndicho cha nafasi ya chini zaidi kuwahi kufika fainali ya Kombe la Dunia.

Kufika fainali ni ufanisi unaostahili kongole kwani inakuja baada ya miaka 20 walimaliza wakiwa nafasi ya 3 baada ya kung'olewa hatua ya nusu fainali na Ufaransa.

Ingawa waliiacha England na huzuni kwa kuzima ndoto zake, mji mkuu wa taifa hilo wa Zagreb ulikuwa kinyume huku maelfu ya wananchi wakijaa kwenye barabara za miji kwa nyimbo na shamrashamra wakiwa wamejihami kwa jezi za rangi nyeupe na nyekundu.

Isitoshe, Croatia ilijinyakulia uhuru wake mnamo 1991.

Mtazamo wa Ufaransa: 'Kupona kutoka uchungu wa 2016'

Ufaransa ilipokuwa mwenyeji wa Dimba la Euro 2016, ililizwa na Ureno baada ya kufungwa mbele ya wafuasi wa nyumbani.

Taifa zima na mashabiki wake hawajasahau jeraha walilopata kutokana na matokeo hayo.

Ufaransa imekuwa ikisukumwa na azma ya kurudisha tabasamu nyuso za mashabiki wake kwa kuwategemea wachezaji wake waliokomaa akiwemo kinda Kylian Mbappe ambaye kasi yake imekuwa kibarua kwa mabeki wa wapinzani.

Tofauti na Croatia, Ufaransa haijasubiri kufika kipindi cha dakika za ziada kwani ilikuwa na mazoea ya kumalizana na mahasimu wake ndani ya muda wa kawaida.

Lakini licha ya kufanikiwa kwa matuta na dakika za ziada, haijakuwa kikwazo Croatia.

Nani ataibuka na tuzo ya mchezaji bora Urusi 2018?

Luka Modric analenga kujizolea medali nyingine baada ya kupokea dhahabu akiiwakilisha Real Madrid walipoibuka na Kombe la Champions League mwezi mei.

Hapo awali, macho yote yalielekezwa kwa mabingwa wa vizazi vya sasa, Mreno Cristiano Ronaldo na nyota wa Argentina Lionel Messi lakini wote waliondoka mapema alfajiri katika hatua ya mchujo na kuwapisha mastaa wapya watakaojulikana baada ya fainali Urusi.

La kustajaabisha ni kuwa, hakuna mshindi wa Kombe la Dunia aliyewahi kutunukiwa mchezaji bora kwa miaka 24. Hata iwapo timu ya nyota itafungwa, haitamzuia kuzawadiwa.

Kuna uwezekano mambo yakabadilika mwaka huu kwani kiungo wa Croatia Luka Modric amemiminiwa sifa kedekede kutokana na fomu yake mechi zote alizoiwakilisha Croatia Urusi.

Amekabidhiwa taji la mchezaji bora wa mechi katika mechi 3 kati ya sita walizocheza ikiwemo mechi aliyoidhalilisha Argentina hatua ya makundi mbele ya Maradona.

Mshambulizi chipukizi wa Ufaransa Kylian Mbappe amejitambulisha kwenye jukwaa la Urusi kutokana na umahiri wake mechi dhidi ya Argentina kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kasi, chenga za dhihaka na mabao ya maana yaliyoirahisishia Ufaransa kuizima Argentina.

Anasaka kuwa chipukizi wa pili tangu shujaa wa Brazil Pele mnamo 1958 kufunga goli fainali ya Kombe la Dunia.

Antoine Griezmann, ni mwingine ambaye anatishia ufanisi wa Mbappe.

Wote wawili, licha ya kuwa katika safu moja, wanashikilia mabao sawa na wanahitaji mabao matatu kutuzwa mfungaji bora kwani anayeongoza jedwali, Mfungaji wa England Harry Kane amefunga mabao sita.

Beki bora wa Kombe la Dunia?

Mlinzi wa Croatia Dejan Lovren anazidi kuzua gumzo na kuwagawanya mashabiki lakini rekodi yake inamtetea.

Iwapo ataanza mechi, Lovren atakuwa kiungo wa pili kuiwakilisha klabu ya Uingereza fainali ya Champions League na Kombe la Dunia ndani ya mwaka mmoja tangu Thierry Henry mnamo 2006.

Haikuwa mwaka mzuri kwa Henry kwani aliishia kuwa katika pande iliyofungwa katika mechi mbili zote kwani Arsenal ilinyamazishwa na Barcelona huku Ufaransa ikilazwa na Italia kupitia penalti.

Mwanzoni wa msimu huu, Lovren alidunishwa na kocha wake wa Liverpool Jurgen Klopp baada ya dakika 31 walipohangaishwa 4-1 na klabu ya Tottenham, huku mfungaji wa Spurs Harry Kane aking'aa Wembley.

Lakini Lovren aliweza kulipiza kisasi nusu-fainli kwa kumzuia Kane kuona wavu na kubadili mtazamo wa watu kuhusu uwezo wake.

"Ni jambo spesheli kwangu," Lovren amenukuliwa. "Kwa mtazamo wangu, watu wanasema nimekuwa na msimu mgumu lakini sikubaliani na hayo.

"Nilidhibitisha hayo kwa kuiwezesha Liverpool kutua fainali ya Champions League na sasa nikichangia ufanisi wa timu yangu kutinga fainali Kombe la Dunia.

"Ni wakati sasa watu wakubali kuwa mimi ni mmoja wa mabeki mahiri duniani sio kuropokwa."

Takwimu zinasemaje?

Kati ya walinzi waote walioingia uwanjani Urusi, beki Lovren mwenye umri wa miaka 29-ameshinda uwaniaji wa mpira hewani mara 32, tano chini ya beki wa England Harry Maguire aliyefikisha 37.

Jamani tumhurumie Nikola Kalinic

Mfungaji wa Croatia Nikola Kalinic amepachika mabao 15 mechi 41 akiiwakilisha taifa lake.

Mshambulizi huyo wa zamani wa Blackburn anayeitumikia AC Milan kwa sasa, Kalinic alifurushwa kutoka kikosi cha timu hiyo baada ya kukataa kuingia mechi waliyoisambaratisha Nigeria 2-0.

Alikataa kuingia uwanjani licha ya kupiga jaramba na kusema kuwa alikuwa na jeraha la bega.

Kuondoka kwake iliiathiri Croatia ambayo haikuruhusiwa kujaza pengo aliloliacha na kusalia na wachezaji 22.

Wenzake watakuwa wanaweka historia na kusakata mechi muhimu maishani mwao wakati Kalinic atajiunga na mashabiki maelfu ya maili nje ya Urusi kufuatilia fainali.