Eden Hazard: Mshambuliaji wa Chelsea adokeza huenda akaihama klabu hiyo

Eden Hazard Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard anasema "pengine ni wakati wa kujaribu mambo tofauti baada ya miaka 6 ya kuvutia Stamford Bridge''.

Kiungo huo mwenye miaka 27, aliyeihakikishia Ubelgiji ushindi dhidi ya Uingereza kwa kufunga bao la pili, waliposhinda 2-0 mechi ya kuwania nafasi ya tatu Kombe la Dunia, amehusishwa na kuhamia Real Madrid.

"Mnajua ni wapi natamani kutua," Hazard aliwaambia waandishi Jumamosi.

"Ninaweza kuamua iwapo nitaondoka au nitasalia lakini uamuzi wa mwisho ni wa klabu ya Chelsea - iwapo wanataka niondoke."

Hazard ameishauri Chelsea kufanya usajili wa maana kabla ya msimu kuanza.

Chelsea ilimpiga kalamu meneja wake Antonio Conte Ijumaa na kumnasa raia mwenzake wa Italia Maurizio Sarri, chini ya saa 24.

The Blues pia walitangaza usajili wa kiungo wa Italia Jorginho kutoka Napoli.

Hazard, ambaye ameweza kuipa Ubelgiji mabao matatu Kombe la Dunia amebakisha miaka miwili katika mkataba wake wa sasa Chelsea.

Tangu alipojiunga nao kutoka Lille kwa kitita cha pauni milioni 32m mwezi Juni 2012, ameiwezesha Chelsea kutwaa mataji mawili ya ligi ya Premier, Kombe la FA, Europa League na Kombe la ligi yaani League Cup.

Hazard alitoa kauli kama hizi mwezi Juni 2017, kwani alisema angeipa Real Madrid sikio iwapo ingejitokeza kufanya dili huku akizidi kuwa pia angeweza kusalia Chelsea "kwa miaka kadhaa".

"Sote tuna ndoto. Inaweza kuwa Uhispania, inaweza kuwa kuganda na Chelsea," aliongeza.

Manmo mwezi Mei, Naibu mkufunzi wa zamani wa Chelsea Steve Clarke alisema klabu hiyo huenda ikampiga mnada Hazard ili kukusanya fedha za kuwasajili wachezaji wengine.

Mada zinazohusiana