Kombe la Dunia 2018: Mchezo wa kandanda asili yake ni wapi?

Kandanda Haki miliki ya picha Getty Images

Michuano ya Kombe la Dunia imemalizika nchini Urusi, lakini licha ya mchezo huo kuwa na ufuasi mkubwa, ni wachache sana ambao hutafakari kuhusu chanzo cha mchezo huu maarufu.

Suala hilo la ni nani ndiye mtangulizi liliibuka mwezi Oktoba mwaka 2016 baada ya Rais wa China Xi Jinping na wahusika wa soka nchini Uingereza kukutana wakati rais huyo alipozuru uwanja wa Etihad nchini humo. Rais Xi ni shabiki wa Manchester United

Ingawa pia Uingereza imekuwa ikijinadi kuwa waanzilishi wa mchezo huo, na hata timu yake ya taifa kujitungia wimbo wa mpira 'unarejea nyumbani' (It's coming home) walipoandaa kombe la mataifa bora bara Ulaya na mwaka huu wakawa wanaimba tena wakati wa Kombe la Dunia ambapo walimaliza wa nne baada ya kushindwa na Ubelgiji 2-0 mechi ya kuamua mshindi wa tatu, baadhi ya wataalamu wanakiri China ndilo chimbuko la soka.

Kevin Moore, Mkurugenzi wa makumbusho ya kitaifa ya soka nchini Uingereza anakubali hilo.

"Ingawa England ndiyo chimbuko la mpira wa soka wa kisasa kama tuujuavyo, tumekuwa tukikubali kwa muda mrefu kwamba chimbuko halisi la mpira huu ni China," alisema Moore, akiwatembeza Xi na Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo David Cameron.

Baadhi ya taarifa hudokeza kwamba mchezo unaokaribiana na kandanda ulikuwa unacheza visiwa vya Uingereza kati ya karne ya nane na ya 19, ingawa kwa miitndo tofauti inayokaribiana na raga.

Soka ya Shrovetide kama ilivyofahamika wakati huo ulikuwa mchezo wa umati usiokuwa na sheria kamili. Njia zozote zingetumiwa kuhakikisha mpira unafika ulikotakikana, bora isiwe mauaji.

Jina 'football' linadaiwa kuwa na asili ya Anglo-Saxon katika maeneo ya Kingston-on-Thames na Chester. Hadithi moja husema mchezo wa kwanza ulichezewa hapo kwa kutumia kichwa cha mwanamfalme wa Denmark ambacho kilikuwa kimekatwa kutoka kwa mwili wake baada yake kushindwa kwenye vita.

Derby, inaaminika kwamba asili yake ni katika kusherehekea ushindi wa vita karne ya tatu dhidi ya Warumi. Lakini hakuna ushahidi wa kuthibitisha hayo. Kabla ya uvamizi wa wanajeshi kutoka Normandy, hakuna ushahidi wowote wa mchezo kama huo. Kuna hadithi nyingine inayosema mchezo huo wa umati ulikuwa unachezwa pia maeneo ya Ufaransa, hasa maeneo ya kaskazini ya Normandy na Brittany hivyo kuna uwezekano kwamba mchezo huu ulifikishwa England na wavamizi kutoka Normandy karne ya 11.

Ulianzia wapi hasa?

Kwa zaidi ya miaka 2000, Wachina wamekuwa wakicheza mpira wa cuju au zuqiu, ambao hutamkwa tsoo-joo unaohusu upigaji mpira shuti kwa kutumia mguu kwa Kiingereza "kickball". Neno hilo hutumika kumaanisha kandanda hadi wa leo katika lugha hiyo....lakini ndio?

Mchango wa China kwenye Soka

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mchezaji aliyevaa sare ya soka ya Cuju anavyoonekana katika makumbusho ya soka ya Linzi ,Shandong, China.

Mchezo wa 'Kickball' ulivuma sana enzi za watawala wa Song, mwaka 960 hadi 1279. Mchezo huo wakati huo ulikuwa sehemu ya burudani mitaani.

Wajapani nao walikuwa na mchezo unaokaribiana na huo kwa jina Kemari, ambao ulianza kucheza miaka 500-600 baada ya Wachina na bado huchezwa leo. Wachezaji hukaa kwenye mduara na kupatiana mpira na kuhakikisha hauanguki chini.

Wagiriki ingawa kwa kuchelewa walikuwa na 'Episkyros' na Warumi 'Harpastum' ingawa miaka ya baadaye.

Mchezo kama huo wa China umezungumziwa katika kitabu maarufu cha The Splendours of the Eastern Capital (Ufarhari wa Jiji Kuu la Mashariki) kuhusu mji mkuu wa China wa wakati huo Kaifeng, mwaka 1120.

Kulingana na jinsi mchezo huo ulivyochezwa, wachezaji walihitajika kudumisha mpira hewani, yaani usitue. Kwa namna nyingine pia, mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa huku wachezaji wakihitajika kulenga goli. Kila timu pia ilikuwa na meneja, mkufunzi na nahodha.

Kulingana na Msomi wa Kijerumani Hans Ulrich Vogel, wahusika walikuwa ni watu kutoka familia tajiri, na pia wapiga shuti wa kitaalamu.

Cuju ulichezwa kama burudani kwenye sherehe rasmi kama zile za kuwalaki mabalozi.

Mchezo huo, ambao umegawanywa kwa ule wenye goli na lisilokuwa na goli, pia ulichewa kutumia sheria zake. Timu zilitumia sare zenye rangi tofauti, manahodha wakiwa na ishara za kuwatambua. Cha kustajaabisha ni kuwa walicheza bila walindalango. Wachezaji pia walihitaji kudumisha nidhamu ikiwemo kuwa na heshima.

Mshindi alikuwa mwenye mabao mengi na walitunukiwa kwa mvinyo na zawadi tofauti.

Kama tu mastaa wa soka ya sasa kama vile Messi na Ronaldo, wachezaji bora wa enzi hizo walipata umaarufu, kutajirika, na timu zao zilialikwa kwenye sherehe za kifalme. Pia walivutia ufuasi mkubwa kutoka kina dada. Katika mchuano mmoja, maelfu ya mashabiki wa kike waliojipamba kwa njia tofauti, walijitokeza kumtazama mchezaji nyota Li Guangyan ili kumvutia.

Nao pia walicheza jinsi ilivyonakiliwa na waandishi wa historia.

Wanawake waliruhusiwa kucheza?

Wanawake walikuwa pia wanashabikia mchezo huu. Shairi moja lwa karne ya 9 linakariria jinsi Li Guangyan, kansela wa wakati huo, alivyokuwa anacheza mpira huo.

"Alikuwa na kasi kama ya tumbili, uso wake kama wa kipanga, wanawake elfu tatu waliinamisha vichwa vyao kumtazama," shairi hilo linasema.

Wanawake pia waliucheza. Mchoro mmoja unaonesha mwanamke akicheza 'kickball' kwenye bustani, nywele zake zikiwa zinavuma kwenye upepo, na mavazi yake kupepea.

Mwandishi mmoja wa habari za udaku kuhusu enzi ya Tang (mwaka 618-907) anaeleza kisa cha vijana watatu wa kike waliokuwa chini ya mti wanawatazama wanajeshi wakicheza karibu nao.. Mpira ulipotoka nje ya uwanja, mmoja wa wasichana hao "alinyoosha mguu wake kwa utulivu, akaudhibiti mpira kwa kidole chake cha gumba, na kisha akaupiga shuti kali na ukajipinda ukiwa hewani".

Unakubali kuwa asili ya soka ni China?

Haki miliki ya picha Alamy
Image caption Mchoro wa mchezo wa kandanda katika makumbusho ya Linzi

Kufika sasa ni dhahiri kuwa China ilikuwa na vilabu vya soka, sheria, na hata mashabiki zaidi ya miaka 1,000 zilizopita.

Lakini soka hiyo ya upigaji shuti, ni tofauti kabisa na soka ya kisasa.

Juhudi za Uingereza za kutunga sheria, umewezesha kubuniwa kwa mashirikisho ya soka, na kufanya soka mchezo wa kimataifa, mchezo wa watu.

Sasa ya China sio Kandanda tubaki kuiita "kickball"?

Licha ya yote, Rais Xi Jinping anayedaiwa kuwa shabiki wa soka wa Manchester United anashikilia kuwa lengo kuu ni taifa lake kufuzu kwa Kombe la Dunia, kuliandaa kombe hilo na hata kulitwaa.

Usishangae kuwaona mastaa wakitwaa mabunda na kuchagua kucheza soka ya kulipwa nchini China- ni lengo lenye mwelekeo.

Haki miliki ya picha Alamy
Image caption Mfalme Taizu wa enzi ya Song akicheza 'kickball'

Na England je?

Sheffield FC, ndiyo klabu ya soka kongwe zaidi duniani ambayo bado imeendelea kuwepo.

Ilikuwa ndiyo klabu ya kwanza kuweka sheria za kisasa za kucheza mchezo wa kandanda mwaka 1858, ingawa wakati huo bado wachezaji waliruhusiwa kutumia mikono yao.

Miaka ya 1860 mchezo huo ulianza kubadilika na ukaendelea hadi kufikia ule unaochezwa kwa sasa. Mchezaji wa ndani ya uwanja hakuruhusiwa kunawa mpira, kulikuwa na wachezaji 11 kila upande, na kisha muda ukawa dakika 90.

Siku hizi, mchezo wa kandanda huonekana wa kawaida hasa katika jamii zinazotukuza juhudi za pamoja.

Katika enzi za ustaarabu, ilikuwa kawaida kuwepo mchezo wa kugonga teke kitu chochote, kiwe ni kitambaa, au ngozi iliyojazwa vitu ndani mfano manyoya au hata kitu kingine chochote kilichojazwa hewa, mfano siku hizi kucheza na puto.

Haki miliki ya picha Clive Rose
Image caption Ufaransa wakisherehekea kushinda Kombe la Dunia 2018

Lakini kuwepo kwa sheria na kanuni kali mchezoni mara nyingi hutokea katika jamii zenye ustaarabu mkubwa.

Lakini jamii zinazotukuza ufanisi wa mtu binafsi, uchezaji wa timu haukutukuzwa. Mfano enzi za ustaarabu wa Wagiriki ambapo michezo ya mtu mmoja ilienziwa zaidi.

FIFA nao walitoka wapi?

Chimbuko ni mwaka 1863 mashirikisho ya mchezo wa raga na kandanda yalipojitenganisha na Shirikisho la Soka la England likaundwa, na kuwa shirikisho la kwanza la usimamizi wa soka duniani.

Mashirikisho yalianza kuenea, Scotland (1873), FA ya Wales (1875) na FA ya Ireland (1880).Mchezo huo ulieneza duniani kutokana na utawala wa Uingereza maeneo mengi.

Netherlands na Denmark waliunda vyama vya soka 1889, New Zealand (1891), Argentina (1893), Chile (1895), Switzerland, Belgium (1895), Italia (1898), Ujerumani, Uruguay (wote wawili mwaka1900), Hungary (1901) na Finland (1907).

FIFA ilianzishwa mjini Paris, Ufaransa Mei 1904 na mataifa saba waanzilishi: France, Belgium, Denmark, Netherlands, Spain (ikiwakilishwa na Madrid FC), Sweden na Uswizi. Chama cha Soka cha Ujerumani kilituma barua ya kutaka kujiunga siku iyo hiyo.