Rio Ferdinand: Ni zamu ya Messi na Ronaldo kumpokeza Mbappe taji

Kylian Mbappe Haki miliki ya picha EPA

Beki wa zamani wa England na Manchester United Rio Ferdinand anaamini Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wanakabidhi usukani 'taji lao la mchezaji bora zaidi duniani' kwa mfungaji chipukizi wa Ufaransa Kylian Mbappe.

Mbappe mwenye miaka 19 alifunga goli la nne la Ufaransa walipoichapa Croatia 4-2 fanali ya Kombe la Dunia Moscow, pamoja na kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora mwenye umri mdogo katika michuano hiyo.

"Ni mtu atakuwa akisimama kwenye jukwaa la kupokea Ballon d'Or miaka michache ijayo," alisema Rio Ferdinand, beki mstaafu wa Manchester United.

"Natumai klabu yangu ya zamani (Manchester United) itamkimbiza kumsajili. Ana ushirikiano mzuri na Paul Pogba."

Mshambuliaji huyo wa Paris St-Germain Mbappe ndiye mchezaji wa pili asiyetimiza miaka 20 kutikisa wavu kwenye fainali ya Kombe la Dunia tangu Pele mnamo 1958.

Ronaldo, 33, na Messi, 31, wametawala ulingo wa soka kwa miaka 10 sasa huku wakipokezana mataji 10 ya Ballon d'Or yaliyotangulia kati yao.

Mbappe amesajili magoli manne nhini Urusi huku mabingwa mara mbili wa Dunia Ufaransa wakiondoka na ushindi kwa mara ya kwanza tangu 1998 nchini Urusi.

Pele aliiwezesha Brazil kunyakua Kombe la Dunia 1958, 1962 na 1970.

Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambulizi wa zamani wa Ujerumani Jurgen Klinsmann, amemsifia Mbappe kuwa mchezo wake ulimfanya aonekana kama alikuwa akiichezea Ufaransa kwa miaka 10.

"Kuna mengi zaidi yatakayopatikana kutoka kwake na yaliyo njiani," alizidi Klinsmann.

Haki miliki ya picha .
Image caption Kylian Mbappe alifunga mabao manne Kombe la Dunia, moja dhidi ya Peru, mawili dhidi ya Argentina na moja dhidi ya Croatia

"Kwa kweli Mbappe amevuruga soko la wachezaji. Huku Ronaldo akitua Juventus na nyota wa Paris St-Germain Neymar akihusishwa na uhamisho hadi vilabu vingine, kinda huyu ataishia wapi?"

Mbali na Mbappe, nyota mwingine wa Ufaransa aliyejizolea sifa ni kiungo Paul Pogba.

'Mourinho aanze kumtumia vizuri Pogba'

Pogba atareja Manchester United bingwa wa dunia baada ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Ligi ya Premia kufunga goli fainali ya Kombe la Dunia tangu kiungo wa Arsenal Emmanuel Petit mnamo 1998.

Staa huyo mwenye miaka 25 alitua United kwa usajili wa pauni milioni £89m uliovunja rekodi wakati huo mnamo mwezi Agosti 2016 lakini alionekana kutapatapa msimu uliopita wa 2017-18.

Mourinho hakumshirikisha kwenye kikosi chake kilichovaana na Sevilla michuano ya mikondo miwili kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambapo United ilitemwa kutoka shindano hilo.

"Pogba alionyesha mchezo mzuri - zaidi katika kipindi cha pili," alisema Ferdinand.

"Amekuwa na msimu mgumu kutoka waandishi wa habari na wachanganuzi wa soka ambao hawakumruhusu anawiri akiiwakilisha Manchester United," anasema Ferdinand.