Alexis Sanchez: Mshambuliaji wa Man Utd azuiwa kwenda Marekani

Alexis Sanchez
Maelezo ya picha,

Sanchez (kulia) talifanya mazoezi na wachezaji wenzake Carrington wiki iliyopita

Alexis Sanchez ameshindwa kujiunga na wachezaji wengine wa Manchester United nchini Marekani kwenye ziara yao nchini humo baada ya kushindwa kupata viza.

Mshambuliaji huyo kutoka Chile alikubali hukumu ya miezi 16 jela ambayo imeahirishwa mwezi Februari kutokana na ulaghai wakati wa ulipaji kodi Uhispania.

Chini ya sheria za Marekani, mtu aliyepatikana na kosa la ulaghai hawezi kupewa viza ya kuingia nchini humo.

Hata hivyo, kuna utaratibu fulani ambao huenda ukatumiwa kuepuka hilo na mawakili wa Sanchez, 29, wanadaiwa kuwa mbioni kujaribu kuona kama watatumia mfumo huo kuhakikisha anaruhusiwa kuingia Marekani na kujiunga na wenzake.

Hata hivyo, taarifa zinasema shughuli hiyo inachukua muda zaidi ya ilivyotarajiwa.

United wataaza mechi za kujiandaa kwa msimu mpya kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Club America ya Mexico siku ya Ijumaa.

Baadaye watacheza dhidi ya San Jose Earthquakes inayocheza Ligi Kuu ya Soka ya Amerika Kaskazini na Canada.

Kisha watacheza na AC Milan, Liverpool na Real Madrid kama sehemu ya shindano la Kombe la Kimataifa la Klabu.

Sanchez hakuwepo pamoja na wachezaji wa United walioshiriki Kombe la Dunia kikosi cha klabu hiyo kilipoondoka kwenda Los Angeles Jumapili kuanza ziara yao itakayoshirikisha mechi tano.

United walikuwa wamepakia mtandaoni picha za Sanchez akifanya mazoezi katika uwanja wao wa mazoezi wa Carrington wiki iliyopita na baadaye picha zake na marafiki Cheshire zikaibuka Jumapili.

Miongoni mwa waliosafiri kwenda Los Angeles ni Juan Mata na Ander Herrera pamoja na beki Antonio Valencia.