Leroy Sane: Mshambuliaji wa Manchester City asema Chelsea watatoa ushindani mkali

Leroy Sane Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sane alitawazwa kinda bora zaidi Ligi ya Premia msimu uliopita

Mshambuliaji wa Manchester City Leroy Sane amesema anatarajia Chelsea ndio watakaotoa ushindani mkali zaidi kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya England msimu ujao.

Klabu hiyo ya London imekuwa na kipindi cha misukosuko tangu mwishoni mwa msimu uliopita.

Walimfuta meneja wao Antonio Conte siku chache zilizopita mwanzoni mwa kipindi cha kujiandaa kwa msimu mpya.

Mwitaliano Maurizio Sarri aliteuliwa kuchukua nafasi ya Conte, na Sane anamfahamu kiasi kutokana na mechi mbili City walizocheza dhidi ya Napoli wakiwa na Sarri msimu uliopita.

Amesema anaamini mkufunzi huyo ataimarisha klabu hiyo ya Stamford Bridge.

"Chelsea wamemleta kocha mzuri sana. Jinsi Napoli walivyocheza msimu uliopita, walikuwa wanapendeza sana. Tulioa taabu sana tukicheza dhidi yao," amesema Sane.

"Huenda pengine wakahitaji muda kidogo kuzoea mbinu zake lakini wanaweza kuta timu hatari sana."

Alipoulizwa ni nani anatoa tishio zaidi kwa City katika juhudi zao za kutaka kutetea taji hilo, alisema: "Nafikiri ni Chelsea."

City walikutana na Napoli hatua ya makundi Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu uliopita ambapo waliwashinda 2-1 nyumbani na 4-2 ugenini.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chelsea walishinda Ligi ya Premia na Kombe la FA miaka miwili FA waliyokuwa na Antonio Conte

Sane, 22, ni mmoja wa wachezaji wachache wa kikosi cha timu kubwa ya City ambao wamo kwenye ziara ya Marekani ambapo watacheza mechi tatu. Amesafiri kwani hakuwa kwenye kikosi cha Ujerumani kilichocheza Kombe la Dunia.

Bernardo Silva, ambaye alikuwa na kikosi cha Ureno kilichoondolewa Kombe la Dunia hatua ya 16 bora alijiunga na kikosi New York Jumatatu kujiandaa kwa mechi ya Alhamisi dhidi ya Liverpool.

Mada zinazohusiana