Serena Williams asema 'anabaguliwa' katika vipimo vya kubaini utumizi wa dawa za kusisimua misuli katika tenisi

Serena Williams

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

Serena Williams alirudi katika tenisi mwezi Februari baada ya likizo ya mwaka ,mmoja ambapo alimzaa mwanawe wa kwanza.

Serena Williams amesema kuwa yeye ni mwathiriwa wa ubaguzi kwa kuwa ndiye mchezaji anayefanyiwa vipimo vya mara kwa mara vya matibabu ikilinganishwa na mchezaji mwengine yeyote yule katika mchezo wa tenisi nchini Marekani.

Bingwa huyo mara 23 wa taji la Grand Slam alitoa madai hayo katika ujumbe wa twitter baada ya maafisa wa kukabiliana na dawa za kusisimua misuli kumtembelea.

Raia huyo wa Marekani alikuwa ameonyesha kukerwa kuhusu kiwango cha vipimo anavyofanyiwa mapema mwezi huu.

"Kati ya wachezaji wote imethibitishwa kuwa mimi ndio nafanyiwa vipimo vingi zaidi, Ubaguzi nadhani,'' alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36.

Chanzo cha picha, Williams/Twitter

Taarifa iliochapishwa na tovuti ya Deadspin mwezi Juni ilibaini kwamba Williams amepimwa licha ya kutokuwa katika mashindano na shirika la kukabiliana na utumizi wa dawa za kusisimua misuli la Marekani katika matukio matano 2018.

Pia limedai kwamba mchezaji huyo hakuwepo wakati maafisa wa Usada walipomtembelea nyumbani mnamo tarehe 14 mwezi Juni -mtu anayefanya vipimo hivyo aliwasili nyumbani kwake saa 12 mapema zaidi ya muda walioafikiana.

Baadaye vipimo hivyo viliorodheshwa kuwa 'vipimo ambavyo havikufanyika-vitatu kati ya hivyo vilikiuka vipimo vya Usada .

Wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hiyo ya Deadspin, Williams alifanyiwa vipimo mara mbili zaidi ya wachezaji wengine nyota -ikiwemo wanaume na wanawake-pamoja na bingwa wa taji la US Open Sloane Stephens na dadake Venus Williams.

Williams aliulizwa kuhusu matokeo ya ripoti hiyo wakati wa mashindano ya Wimbledon mapema msimu huu wa joto.

"Sikujua kwamba nilifanyiwa vipimo mara nyingi zaidi ya mchezaji mwengine yeyote yule'' , alisema bingwa huyo mara saba ambaye alipoteza kwa Mjerumani Angelique Kerber katika fainali.