Kombe la Dunia 2018: Goli la Benjamin Pavard lachaguliwa bao bora zaidi la michuano

Pavard anasema alifuata maelekezo ya washambuliaji juu ya namna ya kufunga akiwa katika eneo kama lile
Maelezo ya picha,

Pavard anasema alifuata maelekezo ya washambuliaji juu ya namna ya kufunga akiwa katika eneo kama lile

Goli la Benjamin Pavard wa Ufaransa limechaguliwa kuwa bora zaidi katika michuano ya Kombe la Dunia iliyomalizika Julai 15 2018.

Goli hilo ni alilolifunga dhidi ya Argentina kwa mkwaju mkali wa kuunganisha uliokwenda moja kwa moja upande wa kulia wa mlinda mlango.

Goli la mlinzi huyo ambaye alionyesha kiwango cha hali ya juu katika michuano ya mwaka huu limepata kura milioni 3 katika mtandao wa Fifa zikiwa ndio nyingi zaidi.

Maelezo ya picha,

Juan Quintero akiachia mkwaju mkali wa adhabu ndogo dhidi ya Japan

''Wala sikuwaza kuhusu hilo.Nilijaribu tu kuupiga mpira ule uelekee nyavuni'', Pavard mwenye miaka 22 alisema baada ya mchezo.

Ufaransa iliifunga Croatia 4-2 katika mchezo wa fainali na kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya pili katika historia.

Pavard aliongeza: ''Mpira ulikua juu kidogo uliponifikia. Nilijaribu kuupiga kuelekea upande uliotokea, kitu ambacho washambuliaji mara zote huniambia.

''Mpira ulipoingia nyavuni nilifurahi sana.''

Maelezo ya picha,

Modric aliibuka pia mchezaji bora wa kombe la dunia 2018

Goli bora la pili limekwenda kwa Juan Quintero wa Colombia alilofunga dhidi ya Japan.

Luka Modric akashika nafasi ya tatu kwa goli lake dhidi ya Argentina.