Mashindano ya Riadha Afrika: Wafahamu wanariadha watakaowakilisha Afrika Mashariki Nigeria

Wanariadha wa mataifa tofauti wakishiriki katika mbio Haki miliki ya picha Getty Images

Ingawa Afrika mashariki imetajwa na kuonekana kuwa ni washiriki katika baadhi ya mashindano mengine kama vile soka hapa barani, na duniani, kwa upande wa raidha, sehemu hii ya Afrika imekuwa moto wa kuotewa mbali.

Licha ya kukabiliwa na madai ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli na udanganyifu, Afrika Mashariki ni baadhi ya maeneo yanayowatia baridi nyota wa riadha pindi mataifa hayo yanapotajwa.

Hata licha ya kuwa na uhasimu wa wenyewe kwa wenyewe kupitia Kenya na Ethiopia, mataifa mawili maarufu kwenye mbio za masafa marefu, Uganda pia imekuwa ikiinuka miaka ya hivi karibuni na kuzidisha ukali wa Afrika Mashariki.

Ingawa bado Afrika Mashariki inazidi kuchecheta na kukosa dira mbio fupi kama vile mita mia 100 na mia 200, imekuwa ikidhibitisha ukali wake katika mashindano mengine kama vile kitengo cha kurusha mkuki ambapo Mkenya Julius Yego 'You Tube' amejiweka kwenye ramani ya shindano hilo.

Hapa tunaangazia ni kina nani watakuwa wanabeba matumaini ya Afrika mashariki mjini Asaba, nchini Nigeria katika mashindano ya riadha barani yaani CAA?

TANZANIA

Haki miliki ya picha Getty Images

Tanzania itawakilishwa na wanariadha watano watakaokamilisha kikosi cha taifa hilo mjini Asaba nchini Nigeria kushiriki mbio hizo.

Wilhelm Gidabuday katibu mkuu wa Riadha Tanzania amethibitisha kuwa Tanzania itakuwa na kikosi cha wanariadha wachache wakiwemo: Failuna Abdi, Gabriel Geay na Agustino Sulle watakaokuwa uwanjani mbio za mita 5000 na 10000, pamoja na Ali Gula atakayeshiriki vitengo viwili vya mbio za mita 100 na 200.

Katika kitengo cha Marathon, Michael Gwandu atakuwa anapepea bendera ya Tanzania.

Matumanini ya timu hiyo yanabebwa pia na Gabriel Gerald ambaye amekuwa akijino nchini Marekani kabla ya kujiunga na timu hiyo nchini Nigeria.

SOMALIA

Ingawa Somalia, haijwaika ipasavyo kwenye riadha, rais wa Shirikisho hilo, Kadija Adem Dahin, amefafanua kuwa watakuwa na kikosi cha wanariadha watano na afisa mmoja na zamu hii, hawatakuwa washiriki tu, bali watakuwa wanalenga kuondoka na medali.

"Tutakapo wasili, tutaanza safari ya kusaka medali na kushindana na wapinzani wetu" alisema Khadija.

UGANDA

Haki miliki ya picha Getty Images

Timu ya Uganda, inayoongozwa na Domenic Otucet, Rais wa shirikisho la riadha Uganda (UAF) imeshirikisha kikosi chenye mchanganyiko wa fomu nzuri, wanariadha chipukizi na nyota wenye uzoefu.

Walipokuwa wakifanya mazoezi, kikosi hicho kiligwanywa kwa upande wa wanariadha wanaoshiriki mbio fupi, na zile za masafa marefu.

Kikosi cha mbio za masafa marefu kilikita kambi Kapchorwa na wanariadha wa kwend kasi walikusanyika Namboole wakiwa pamoja na wale wa kurusha mkuku na kisahani.

Ingawa bingwa mara mbili wa mbio za Commonwealth Joshua Cheptegei anauguza jeraha, majukumu yametikwa kwa Timothy Toroitich na Jacob Kiplimo katika kitengo cha mita elfu 10,000.

Katika mbio za mita elfu 5,000 - Kevin Kibet na Stephen Kissa watakuwa wakibeba matumaini ya Uganda lakini pengo lililoachwa na bwana Cheptegei kimeumiza kikosi hicho.

Cheptegei aliumia akiwania mbio za Commonwealth Gold Coast, Australia, mwaka huu.

Matumaini kwa Chesang

Stella Chesang (21), ambaye hivi majuzi alipaishwa madaraka, ndiye tegemeo la Uganda baada ya kuzoa dhahabu mbio za Commonwealth za mita elfu 10,000.

Chesang ana kibarua kigumu dhidi ya Wakenya Alice Aprot na bingwa mara mbili wa dunia Pauline Korikwiang.

Chesang alikimbia muda wa dakika 31:45.30 kule Gold Coast na nchini Nigeria, atakuwa anatafuta dhahabu yake ya kwanza mbio za Afrika.

Kikosi cha Uganda Nigeria

Haki miliki ya picha Getty Images

Kina dada: Stella Chesang, Mercyline Chelangat (10,000m), Janet

Chemusto (5,000m), Winnie Nanyondo, Halima

Nakaayi (800m), Peruth Chemutai (3000mSC), Shida Leni

(200/400m), Scovia Ayikoru (100m/200m), Lucy Aber (javelin)

and Josephine Lalam (Javelin).

Wanaume: Timothy Toroitich, Jacob Kiplimo (10,000m),Albert

Chemutai (3000m SC), Ronald Musagala (1500m), Geoffrey

Ruto, Rashid Atiau (800m), Pius Adome (100m/200m),

Leonard Opiny (400m), Stephen Kissa, Kevin Kibet (5,000m)………

Rwanda

Haki miliki ya picha Getty Images

Taifa la Rwanda litakuwa linamtegemea Beatha Nishimwe mwenye umri wa miaka 19 kuiletea sifa katika mbio za mita1,500 upande wa kina dada.

Nishimwe alifuzu kwa mashindano ya riadha barani kwa kukimbia muda wa dakika 4 minutes na sekunde 14 huku akiponea kwa kumaliza chini ya sekunde 21 muda unaohitajika kufuzu.

Nishimwe atakuwa na Salome Nyirarukundo na kukamilisha kikosi cha Rwanda chenye wanariadha wawili Nyirarukundo anashiriki mbio za mita elfu 10,000.

Wawili hao, ambao walijikatia tiketi ya mashindano haya kwenye mbio za Commonwealth zilizofanyika kati ya tarehe 4-15 Aprili kule Gold Coast, Queensland, Australia watakuwa wanalenga kutua mashindano ya riadha kati ya bara tofauti yatakayopigwa mwezi Septemba nchini Czech.

"Nimejiandaa vizuri hapa uwanja wa Amahoro na matarajio yangu ni kufuzu kukimbia mashindano ya riadha ya dunia nchini Czech.," Alisema Nishimwe ambaye alikosa mbio za Olympiki 2016 kwa sekunde moja.

Nishimwe ambaye anashiriki mbio hizi kwa mara yake ya pili, atakuwa na mwenzake Nyirarukundo mshindi wa mbio za kimataifa za Kigali Peace Half ambaye amekuwa akipiga jaramba nchini Kenya tangu mwezi Mei.

Nyirarukundo atakayekimbia kitengo cha mita elfu 10,000, pia anashiriki mbio hizi kwa mara yake ya pili tangu Makala ya mwisho yaliyogaragazwa mjini Durban, Afrika Kusini.

Ethiopia

Haki miliki ya picha Getty Images

Baada ya kutapatapa mbio za Durban, shirikisho la riadha Ethiopia (EAF) limewekeza pakubwa katika makala ya mwaka huu.

Walimaliza nafasi ya nane Makala ya 2016 nchini Durban kwa kushinda medali 6 pekee.

Dhahabu pekee waliozoa ilikuwa katika kitengo cha mita elfu 3000 upande wa wanaume kutoka Chala Bayou na kumaliza nafasi ya nane katika mashindano hayo.

Mkurugenzi wake wa kiufundi, Dube Jillo, amesema wameweka mzaha kando na kutaja kikosi kikali pamoa na kuwajumuisha wakufunzi imara na wanariadha matata.

EAF imewajumuisha wanariadha chipukizi, nyota maarufu duniani, na wakimbiaji wazoefu.

Licha ya changamoto za Makala ya mwisho, Ethiopia imekuwa mpinzani wa kuogofya katika mbio hizi ambapo kufikia sasa wamejizolea medali 141 zikiwemo 40 za dhahabu.

Genzebe Dibaba na Solomon Barega watakuwa wakiongoza kikosi cha wasimamizi na wanariadha 64 kitakachoimarisha na wakufunzi 13.

Kenya

Haki miliki ya picha Getty Images

Kenya itawakilishwa na wanariadha 61 kwenye mashindano ya mwaka huu.

Wanariadha wa mbio fupi kutoka Kenya, Eunice Kadogo, Joan Cherono na Fresha Mwangi, wamefunguka kuwa, mbali na kulenga kumaliza nafasi nzuri mbio za CAA Asaba 2018, malengo yao pia yatakuwa kuimarisha muda wao wa mbio hizo na kuzidisha nafasi zao za kutua Ostrava Czech, baadaye mwaka huu.

Watatu hao wataiwakilisha Kenya mbio za kupokezana vijiti 4 x100m wakiwa na Millicent Ndoro.

Mbali na Nigeria, Cote d'Ivoire na Afrika Kusini, Kenya ni taifa la kupigiwa upatu mbio fupi.

Abraham Mutai, mmoja wa wasimamizi wa kikosi cha Kenya, amefafanua kuwa watakuwa wakilenga kuboresha matokeo yao kutoka nafasi ya pili Makala yaliopita hadi nafasi ya kwanza.

Kenya, ilimaliza nafasi ya pili katika awamu ya mwisho ya mashindano haya yaliyopepetwa nchini Afrika Kusini mnamo 2016 na kudhihirisha ni kwa nini Afrika Mashariki imekuwa kiungo muhimu barani katika riadha.

Ndio kwa sababu imekuwa ni rahisi kutabiri kuwa Afrika mashariki itakuwa na wawakilishi kwenye mashindano katika bara tofauti mwezi Septemba mwaka huu nchini Czech.