Mamia ya wanariadha wakiwemo WaKenya wakwama Nigeria

kenya

Zaidi ya wanariadha 300 wakiwemo wa kutoka Kenya na kutoka mataifa mengine ya Afrika wamekwama katika uwanja wa ndege wa Murtala Muhammad 2 mjini Lagos Nigeria.

Wanariadha hao walitarajiwa kushiriki kwenye mbio za riadha za Afrika zitakazoanza leo.

Jumatano, mjini Asaba, jimbo la Delta, Nigeria. Ingawa mbio hizo zitang'oa nanga leo, matayarisho yalianza mwezi Novemba mwaka wa 2017.

Kikosi cha Zambia kilichowasili Nigeria siku ya Jumamosi, kilifika uwanja wa mashindano siku ya Jumanne.

Mji huu wa Asaba ulitarajiwa kujizolea sifa kwa kuandaa Makala ya 21 ya riadha barani, lakini kuanzia siku ya jumamosi wiki hii, wanariadha kutoka matafa 52 wamekabiliwa na changamoto za uchukuzi na za usimamizi.

Wanariadha wa Kenya ndio walioathirika Zaidi huku Zaidi ya wanariadha 40 wakisalia uwanja wa ndege wenzao wakifanya mazoezi uwanjani wa Lagos.

Wengine wamegeuza uwanja wa ndege kuwa chumba cha malazi na uwanja wa kupiga jaramba. Wameonekana wakijinyoosha kwenye maeneo ya kuabiri ndege.

Tatizo hili limezidi mpaka baadhi ya wanariadha wamelazimika kutumia njia mbadala kama usafiri kwa gari na kuhatarisha usalama wao.

Maelezo ya picha,

Mwanariadha wa Kenya Gilbert Osure alilazimika kusafiri kwa gari

"Sikutarajia mhangaiko wa aina hii. Nimesafiri kwa gari kwa Zaidi ya saa mbili hadi hapa. Imekuwa ni safari ndefu na yenye uchovu," alinukuliwa mwanariadha wa Kenya, Gilbert Osure.

Wengine waliowasili siku ya jumanne wamekashifu vikali mipango duni ya waandalizi.

"Sijawahi kuona maandalizi ya aina hii. Nimeshiriki mashindano mengi, lakini hakuna mabaya Zaidi ya tuliyoyapitia hapa Nigeria," alisema mkufunzi wa Algeria, Benid Amar, ambaye kikosi chake kilipitia Paris kufika hapa.

Lakini eneo lenyewe lilikuwa na uwezo wa kuandaa mashindano haya?

Gavana wa eneo la Delta linalosimamia mji wa Asaba, Ifianye Okowa, amedokeza kuwa awali walikuwa na wasiwasi wa kubeba mzigo wa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kiwango hiki.

''Miezi chache zilizopita, tulipofahamishwa kuwa waandalizi, nilikuwa na woga akilini mwangu," alisema Okowa.

Ingawa baraza kuu la riadha barani liliandaa mkutano wake, tatizo hili limetia dosari kwa maandalizi kwa jumla.

"Sikuamini Asaba ingeweza kuwa mwenyeji. Nilipozuru uwanja huu mwaka uliopita,nilihisi haungekuwa tayari." Rais wa Riadha barani, Kalkaba Malboum, amesema.

Mataifa kama vile Botswana yenye nyota kama vile Nijel Amos waliwasili Jumatatu baada ya kusubiri kwa siku mbili uwanja wa ndege.

Mabingwa watetezi Afrika Kusini, walifika Jumanne.

Sio kila mmoja ameshangazwa na hali hii. Nyota wa mbio fupi kutoka Nigeria, Blessing Okagbare, amelitetea taifa lake. Biashara ya Benki Tanzania yasuasua kutokana na wateja kutolipa madeni

"Linaweza kutokea, lakini ni uchungu kwa mwanariadha" alisema Blessing Okagbare.

"Ndio mara ya kwanza tunaandaa mashindano haya na sio rahisi " alizidi.

Meneja wa Afrika Kusini John Matiani aliwalaumu waandalizi pia.

"Tulikwama Lagos licha ya kuwasili tarehe 28 Julai. Hatuna pasipoti zetu kufikia sasa na hatujui zilipo," alimaliza.

Maelezo ya picha,

Solomon Ogba mwenyekiti wa kamati andalizi

Hata baada ya mwenyekiti wa kamati andalizi bwana Solomon Ogba, kujipiga kifua na kujigamba kuwa hakuna shindano bora litakalokuwa kama hili, wanariadha wa Afrika wametishia kujiondoa kutoka mashindano haya.

Maafisa hawa wameanza juhudi za kuwasafirisha wanariadha hawa lakini yanajiri saa chache tu kabla ya shindano lenyewe kufunguliwa rasmi.

Serikali ya Kenya imeahidi kuingilia kati na kuwasafirisha wanariadha wake, lakini bado wamesalia uwanja wa ndege.

Sahihisho 02 Agosti 2018: Taarifa hii awali ilitaja kwamba wanariadha wa Tanzania ni miongoni mwa waliokuwa wamekwama katika uwanja wa ndege Lagos kuelekea kushiriki katika mashindano hayo Asaba. Katibu mkuu wa riadha Tanzania, Wilhelm F. Gidabuday katika taarifa yake amesema timu ya Tanzania ilijiondoa kutoka kwenye mashindano hayo baada ya kushindwa kuondoka nchini mwao kutokana na kucheleweshwa kwa barua ya mwaliko kutoka kwa waandalizi, na sababu za kiusalama. Hawakuwa wameondoka nchini Tanzania.