Tanzania kutoshiriki riadha za mabara Czech mwezi ujao

Wanariadha wa Tanzania wakiwa katika mashindano ya siku za nyuma

Sasa ni rasmi kuwa Tanzania haitakuwa kwenye mashindano ya riadha barani kumaanisha kuwa itakuwa nje ya mashindano ya mabara yatakayofanyika nchini Czech mwezi ujao.

Hii imewafanya wasimamizi wa maandalizi ya mashindano hayo yanayoendelea mjini Asaba nchini Nigeria, na wakuu wa riadha Tanzania kuhusika kwenye majibizano kufuatia hali ya timu ya Tanzania kukwama nchini mwao.

Ingawa taarifa za awali zilisema kuwa timu hiyo huenda ilikwama mjini Lagos, pamoja na vikosi vingine, waandalizi wenyewe wamejitokeza kuonyesha kuwa hawajapokea taarifa rasmi kuhusu kutokuwepo kwa Tanzania mashindanoni.

Timu zote zilizokwama Lagos zimewasili siku ya Jumatano isipokuwa Tanzania.

Kulingana na mwandishi wa BBC anayehudhuhuria mashindano hayo mjini Asaba, Abdinoor Aden, bendera ya Tanzania imewekwa nje ya uwanja na kama ilivyofanywa kwa mataifa yanayoshiriki mashindano hayo. Aidha, bendera nyingine pia ilikuwa imenyanyuliwa wakati wa sherehe za ufunguzi siku ya Jumatano licha ya kutokuwepo kwa mwanariadha yeyote.

Haya yanajiri baada ya makala ya 21 ya riadha barani kanza rasmi mjini Asaba, Nigeria, siku ya Jumatano.

"Wamekwama wapi, Lagos? Wamejiondoa kutoka mashindano hayo? Sina habari" Alisema mwenyekiti Solomon Ogba.

Kamati andalizi nchini Nigeria imetoa lawama kwa vikosi na wasimamizi wao kwa kutowajibika ipasavyo.

"Tuliwapa ualishi wawakilishi wa timu za Afrika lakini wengine hawakuweza kutuhakikishia iwapo wangefika au la," alisema mwenyekiti wa kamati hiyo Solomon Ogba.

Tanzania haikuweka wazi iwapo ingeshiriki na haikufika pia kwenye mkutano wa wanachama wa baraza hili wa kuandaa mashindano."

Kwa upande wake, kupitia barua iliyofafanua sababu za kutofika kwao kwenye mashindano, katibu wa shirikisho la riadha Tanzania, Wilhelm F. Gidabuday amefafanua kuwa zilichangiwa na sababu za usimamizi.

"Wiki tatu nilipokuwa Asaba nilitahadharisha kwamba LOC hawapo makini sana japo wanayo pesa za kutosha, kitendo cha Nigeria kutotuma barua muhimu kwa mataifa ya Africa kimewaudhi wengi kutoka mataifa yote ya Afrika, kitendo hicho kimesababisha nchi nyingi kujitoa mashindano hayo kutokana na utaratibu usioridhisha". Ilisema barua kutoka Wilhelm.

Kulingana na Wilhelm, mawasiliano duni na maandalizi ya kuchelewa ya barua hizo muhimu zikiwemo za mwaliko pamoja na ya Uhamiaji zilitumwa kuchelewa na hata kuwafikia nchini Tanzania kupitia njia ya mtandano wa Whatsapp.

Hata hivyo timu hiyo imekwama katika hatua ya kusaka ndege ya kusafiri hata baada ya sherehe za ufunguzi kuanza.

Hali hiyo imewanyima wanariadha wa mbio za mita 5000 na 10000 akiwemo Failuna Andi Matanga

Gabriel Gerald Geay, Agustino Paullo Sulle huku Ali Khamis Gulam wa mita 100 na 2000 pamoja na Michael Zachariah Gwandu wa kitengo cha kuruka wakilimika kukosa mashindano hayo.

Wakati huo huo, rais wa riadha duniani, IAAF, Sebastian Coe, ameahidi kuwa wataimarisha viwango vya maandalizi vya mbio hizo barani ili kuinua hali hiyo.

"Kama IAAF, tutawapiga jeki waandalizi ili tudumishe viwango bora katika riadha barani".

Mada zinazohusiana