Mkusanyiko wa habari za soka Ulaya 03.03.2018: Gabriel Jesus, Pedro, Ahmed Musa, Willian, Mourinho

Gabriel Jesus atia saini kandarasi mpya

Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji wa Manchester City Gabriel Jesus ametia saini kandarasi mpya itakayomweka katika klabu hiyo hadi 2023.

Jesus mwenye umri wa miaka 21 aliwasili katika uwanja wa Etihad kutoka klabu ya Brazil ya Palmeiras kwa dau la £27m mnamo mwezi Januari 2017 na kufunga magoli saba katika mechi 11 akiichezea klabu hiyo.

Alifunga magoli 17 na kuisaidia City kushinda taji la ligi kuu Uingereza na kombe la Carabao.

Pedro aongeza kandarasi ya mwaka mmoja Chelsea

Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji wa Chelsea Pedro ametia saini kandarasi ya mwaka mmoja itakayomweka katika klabu hiyo ya Stamford Bridge hadi 2020.

Pedro mwenye umri wa miaka 31 alijiunga na Blues kutoka Barcelona mnamo mwezi Agosti 2015 kwa dau la £21m na kuisaidia klabu hiyo kushinda taji la ligi ya Uingereza 2016-17 na Kombe la FA msimu uliopita.

Winga huyo wa Uhispania alifunga magoli 28 katika mechi 131 na alifunga katika mechi ya maandalizi ya msimu mpya dhidi ya Perth Glory na Inter Milan.

''Nafurahia kuwa hapa na nataka kushinda mataji mapya'' , alisema Pedro ambaye alihudumu misimu tisa akiichezea Barcelona

Musa aamua kuondoka Leicester

Haki miliki ya picha Getty Images

Mshambuliaji wa Nigeria Ahmed Musa ameondoka katika klabu ya Leicester City na kuelekea Al-Nassr kwa dau lisilojulikana , klabu hiyo ya Saudia imetangaza.

Mchezaji huyo wa Leicester mwenye umri wa miaka 25 ndio mchezaji aliyesainiwa kwa dau lililovunja rekodi wakati alipojiunga na klabu hiyo kwa kitita cha £16m kutoka CSKA Moscow mwaka 2016.

Lakini baada ya magoli mawili katika mechi 21, alirejeshwa kwa mkopo katika timu hiyo ya Urusi msimu uliopita.

Musa aliichezea Nigeria katika michuano iliopita ya kombe la dunia nchini Urusi , akifunga mabao mawili katika ushindi wa Nigeria dhidi ya Iceland.

Mkufunzi wa Chelsea: Willian atasalia lakini hatma ya kipa Courtois siijui

Haki miliki ya picha Getty Images

Mkufunzi wa Chelsea Maurizio Sarri anasema kuwa ana matumaini kwamba Willian atasalia katika klabu hiyo -lakini amesema hajui hatma ya kipa Thibaut Courtois.

Winga huyo wa Brazil Willian, 29, amehusishwa na uhamisho wa Manchester United, Real Madrid na Barcelona na aliwasili kuchelewa katika mazoezi ya kuandaa msimu mpya .

Sarri anasema kuwa alikuwa na mazungumzo mazuri na mchezaji huyo siku ya Alhamisi.

''Hakuna tatizo na Willian'', alisema Mkufunzi huyo wa zamani wa Napoli.

Kipa wa Ubelgiji Courtois,26, amehusishwa na uhamisho wa kuelekea Real Madrid.

Jose Mourinho anafaa kutabasamu, asema Brian McClair

Haki miliki ya picha Getty Images

Mkufunzi wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho anafaa kuonyesha kwamba anafurahia kuwa na kazi nzuri zaidi katika kandanda duniani na kwamba mashabiki wanataka kumuona akitabasamu zaidi, kulingana na mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo Brian McClair.

Mourinho ameonakana kutokuwa na raha katika mechi za maandalizi ya msimu mpya, akiwalaumu wachezaji na hatua ya klabu hiyo kutosajili wachezaji wapya mbali na mchezo mbaya dhidi ya Liverpool.

Tetesi za soka Ulaya Ijumaa 03.08.2018

Tetesi za soka

  • 'Real imemwekea Luca Modric bei ya £670m .
Haki miliki ya picha Getty Images

Sasa ni wazi kwamba klabu yoyote inayotaka kumsajili kiungo huyo wa kati ambaye alikabidhiwa taji la mchezaji bora katika kombe la dunia atalazimika kulipa £670m katika kandarasi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32.

Modric amehusishwa na uhamisho wa Inter Milan.