Thibaut Courtois na Willian: Mlinda lango wa Chelsea agomea mazoezi, atahamia Real Madrid? Willian alitafutwa na Barcelona

Thibaut Courtois

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Courtois aliibuka kipa bora wa michuano ya Kombe la Dunia Urusi akichezea Ubelgiji

Mlinda lango wa ChelseaThibaut Courtois, ambaye amehusishwa na kuhamia Real Madrid, hakufika kwa kikao cha mazoezi katika klabu hiyo inayocheza Ligi Kuu ya England siku ya Jumatatu na wala hakutoa taarifa.

Inafahamika kwamba Chelsea hawajui ni lini Mbelgiji huyo mwenye miaka 26 atarejea.

Duru zinasema huenda akawa anataka kulazimisha uhamisho wa kwenda Real Madrid, klabu ya Uhispania ambayo imekuwa ikimtafuta kwa muda mrefu.

Courtois amekuwa mchezaji wa Blues tangu 2011, alipojiunga nao kutoka klabu ya Genk ya Uholanzi. Misimu ya kwanza alitumwa kwa mkopo Atletico Madrid nchini Uhispania.

Winga wa Chelsea Eden Hazard amehusishwa pia na Real, lakini hakuhudhuria pia mazoezi Jumatatu.

Courtois alitawazwa mlinda lango bora wa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi ambapo Ubelgiji waliwazidi nguvu England na kumaliza wa tatu katika michuano hiyo.

Amechezea Chelsea mechi 154 na kumaliza mechi 58 bila kufungwa. Amefungwa jumla ya mechi 152.

Akiongea Ijumaa, meneja mpya wa Chelsea Maurizio Sarri alisema hana uhakika iwapo Courtois atasalia katika klabu hiyo.

"Kwa sasa Courtois ni kipa wa Chelsea. Sijui kuhusu siku zijazo. Inategemea klabu, lakini pia inamtegemea zaidi yeye binafsi, lakini natumai kwamba Courtois ataendelea kuwa golikipa wetu."

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Willian amechezea Chelsea mechi 237 tangu aiunge nao 2013 kutoka Shakhtar Donetsk

Mbrazil Willian, mchezaji mwingine ambaye ameonekana kutotulia Chelsea amethibitisha kwamba alikuwa anatafutwa na Barcelona wakitaka kumnunua.

Willian, 29, amekuwa Stamford Bridge kwa miaka mitano lakini alikuwa anadaiwa kupanga kuondoka kabla ya soko la kuhama wachezaji kufungwa.

Akizungumza baada ya Chelsea kushindwa 2-0 na Manchester City mechi ya Ngao ya Jamii Jumapili, aliambia ESPN Brasil: "Daima nimeweka wazi kwamba nilitaka kusalia katika klabu hii.

"Klabu pekee ambayo ninafahamu iliwasilisha rasmi ofa ya kunitaka ilikuwa ni Barcelona."

Alikuwa amehusishwa pia na kuhamia Manchester United na Real Madrid.

Willian aliongeza: "Kichwa changu kipo hapa na natumai kuendelea kusalia katika klabu hii, pengine klabu yenyewe iamue kuniuza."

Meneja Sarri amewanunua wachezaji wawili pekee kipindi cha sasa cha kuhama wachezaji - kiungo wa kati wa Napoli Jorginho na kipa wa akiba Rob Green.