Mambo muhimu yaliyotokea siku ya mwisho ya kuhama wachezaji: Tottenham na Manchester United, Yerry Mina, Paul Pogba, Eden Hazard

Mateo Kovacic Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mateo Kovacic alihamia Chelsea kwa mkopo kutoka Real Madrid

Everton, Fulham na Leicester wote walitumia kiasi kikubwa cha pesa kuwanunua wachezaji siku ya mwisho ya dirisha kuu la kuhama wachezaji Alhamisi.

Hata hivyo, kiasi cha pesa zilizotumiwa siku hiyo na klabu za Ligi ya Premia kilishuka kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minane, ambapo klabu zilitumia £1.2bn pekee.

Tottenham - hawakumnunua mchezaji yeyote kipindi cha sasa cha kuhama wachezaji.

Manchester United nao, jambo ambalo huenda lisimfurahishe meneja wao Jose Mourinho, hawakumnunua mchezaji yeyote siku ya mwisho sokoni 9 Agosti.

Uhamisho wa Yerry Mina wa £27m kwenda Everton kutoka Barcelona ulikuwa ndio wa kiasi kikubwa zaidi cha pesa siku ya mwisho mwaka huu.

Siku ya mwisho ya kuhama wachezaji ilibadilishwa kutoka 31 Agosti kama ilivyokuwa kawaida miaka ya nyuma na kuwa siku moja kabla ya Ligi Kuu ya England kuanza.

Ligi itaanza leo kwa mechi kati ya Leicester City na Manchester United uwanjani Old Trafford.

Uamuzi wa kubadilisha siku hiyo ulitokana na kura iliyopigwa na klabu, na ni baada ya mameneja wengi kulalamika kwamba wachezaji hukosa kutulia mechi za kwanza za msimu wengine wakijaribu kulazimisha kuhamia klabu nyingine. Msimamo hata hivyo haikuwa wa kauli moja, kuna klabu zilizokuwa zinapinga.

Siku ya mwisho ya kuhama wachezaji katika ligi za mataifa mengine Ulaya, pamoja na Scotland bado ni 31 Agosti.

Mabadiliko yanaathiri pia ligi nyingine za England na Wales (Ligi ya Championship, League One na League Two) lakini bado wanaruhusiwa kuwasajili wachezaji ambao hawana mikataba na klabu yoyote au kwa mkopo hadi 31 Agosti.

Tofauti hiyo ina maana kwamba klabu za Uhispania, Ujerumani, Ufaransa na Scotland bado zitaweza kuwasajili wachezaji hadi kufikia mwisho wa mwezi. Kwa hivyo usishangae Mfaransa Paul Pogba ambaye tetesi zimedai anataka kuhamia Barcelona akifanikiwa kuhama. Eden Hazard ambaye amekuwa pia anatafutwa na Real Madrid bado anaweza kuhama.

Tatizo pekee ni kwamba wawili hao wakaondoka, klabu za hazitaweza kuwasajili wachezaji wengine nyota kujaza nafasi zao.

Italia siku yao ya mwisho ya kuhama wachezaji ni Ijumaa 17 Agosti, siku moja kabla ya ligi yao ya Serie A kuanza.

Mambo makuu kuhusu siku ya mwisho

Pamoja na tarehe ya siku ya mwisho kuwa mapema, wakati wa kufungwa kwa soko siku hiyo ya mwisho pia ulikuwa mapema - saa 17:00 BST (saa moja jioni Afrika Mashariki) badala ya 23:00 ilivyokuwa kawaida.

Ilionekana kama ingekuwa ndiyo siku ya shughuli chache zaidi ya mwisho sokoni tangu kauznishwa kwake mwaka 2003 - ambapo ni uhamisho wa wachezaji wanane pekee uliokuwa umethibitishwa kufikia saa 17:00.

Uhamisho wa juu zaidi kufikia wakati huo ulikuwa wa kiungo wa kati wa Croatia Mateo Kovacic kujiunga na Chelsea kwa mkopo kutoka Real Madrid naye kipa Thibaut Courtois akahamia Madrid kwa mkataba wa kudumu.

Lakini klabu zilikuwa na saa nyingine mbili za kukamilisha mikataba baada ya saa ya mwisho na ni hapo ambapo Everton walifanikiwa kumpata mchezaji wa Colombia Yerry Mina ambaye ni beki pamoja na Andre Gomes kwa mkopo kutoka Barcelona.

Alikuwa awali wamemsajili Bernard ambaye hakuwa na mkataba siku moja awali.

Fulham walitangaza kuwapata wachezaji watano baada ya muda wa mwisho kupita - kiungo wa kati wa Marseille Andre-Frank Anguissa kwa uhamisho wa £22.3m, beki wa kushoto wa Bristol City Joe Bryan kwa £6m na Sergio Rico, Luciano Vietto na Timothy Fosu-Mensah kwa mkopo.

Hilo liliwafanya kuwa klabu ya kwanza iliyopandishwa daraja kutumia zaidi ya £100m kuwanunua wachezaji dirisha kuu la kuhama wachezaji.

Leicester City nao walithibitisha usajili wa beki wa Freiburg na Uturuki Caglar Soyuncu, uhamisho unaokadiriwa kuwa na thamani ya hadi £19m. Awali walikuwa wamemnunua beki Filip Benkovic kutoka Dinamo Zagreb kwa £13m.

Image caption Wachezaji 10 ambao uhamisho wao ulikuwa wa thamani ya juu zaidi EPL (ada ya msingi ya uhamisho bila kuzingatia marupurupu)

Wengine waliohama ni pamoja na Danny Ings kujiunga na Southampton kutoka Liverpool kwa mkopo ambao utageuzwa kuwa uhamisho wa kudumu mwaka ujao, Jordan Ayew kwenda Crystal Palace kutoka Swansea kwa msimu mmoja na West Ham kumsajili mshambuliaji wa Arsenal Lucas Perez napia kiungo wa kati wa Fiorentina Carlos Sanchez.

Walioambulia patupu?

Kuna klabu sita ambazo hazikumnunua mchezaji hata mmoja Alhamisi.

Tottenham wanadaiwa kuwa klabu ya kwanza katika enzi ya Ligi ya Premia kutomsajili mchezaji hata mmoja dirisha kuu la kuhama wachezaji.

Hata hivyo meneja wao Mauricio Pochettino hajasikitika, ingawa kinda wake wawili waliondoka kwenye klabu.

"Ni vigumu kwa watu kuelewa kwamba Tottenham hawakununua au kuuza mchezaji hata mmoja, wakati mwingine katika soka unahitaji kuwa tofauti na tumeridhika na kikosi chetu," alisema.

Manchester United walinunua wachezaji watatu pekee kipindi chote cha kuhama wachezaji, wote kufikia mapema Julai.

Lakini walijaribu pia kumnunua beki mkabaji wa kati na meneja wao Jose Mourinho Jumapili alitahadharisha kwamba huenda wakakabiliwa na wakati mgumu msimu huu wasipofanikiwa kumsajili mchezaji mwingine.

Walikuwa wamehusishwa na Toby Alderweireld wa Tottenham, Harry Maguire wa Leicester na nyota wa Bayern Jerome Boateng dirisha la sasa la kuhama wachezaji.

Na Mashetani hao Wekundu waliwasilisha ofa ya kushangaza nyakati za mwisho wakimtaka beki wa Atletico Madrid Diego Godin - lakini mchezaji huyo sasa anatarajiwa kutia wino kwenye mkataba mpya katika klabu hiyo ya Uhispania.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Thibaut Courtois alihamia Rea Madrid na kutia saini mkataba wa miaka sita

Spurs walikuwa miongoni mwa klabu 14 zilizopiga kura Septemba mwaka jana kutaka siku ya mwisho ya kuhama wachezaji ibadilishwe. United walipinga.

Arsenal na Liverpool pia hawakumsajili mchezaji yeyote siku ya mwisho ya kuhama wachezaji ingawa si wengi waliotarajia wanunue wachezaji ikizingatiwa kwamba walikuwa wamewanunua wachezaji kadha wa thamani ya juu mapema kwenye soko.

Pesa nyingi kutumiwa nje

Takwimu za Deloitte zinaonesha pesa zilizotumiwa dirisha la sasa zilishuka kwa £200m ukilinganisha na mwaka jana ambapo rekodi ya £1.4bn iliwekwa.

Siku ya mwisho pesa zilizotumiwa zilikuwa ni kidogo tu zaidi ya nusu ya pesa zilizotumiwa mwaka 2017 - £110m, chini kutoka £210m.

Lakini klabu za England zilitumia £880m, ambayo ni rekodi mpya, kuwanunua wachezaji wa ligi za nje, ukilinganisha na £770m mwaka jana. Asilimia 72 ya pesa hizo zote zilitumiwa na klabu za ligi kuu England - mwaka jana kiasi hicho kilikuwa asilimia 54.:

  • Ligiinayofuata kwa kutumia pesa nyingi ni Serie A, kwa jumla wakitumia £910m (ikiwa ni pamoja na £99m za kumnunua Cristiano Ronaldo), wakifuatwa na La Liga (£680m), Bundesliga (£400m) na Ligue 1 (£350m) - lakini soko katika ligi hizo bado halijafungwa
  • Klabu za Championship zilitumia £155m uhamisho wa wachezaji - kiasi kimepungua kutoka £195m mwaka jana
  • Klabu zilizotumia pesa nyingi zaidi Ligi ya Premia ni Liverpool (£165m), Chelsea (£120m), Fulham (£105m) na Leicester City (£100m)
  • Ni klabu tatu pekee zilizolipwa pesa nyingi kuliko walizolipa kuwanunua wachezaji EPL - Newcastle United, Tottenham Hotspur and Watford

Ni kwa nini soko mwaka huu biashara ilikuwa chini?

Uhamisho wa dakika za mwisho ulifikisha idadi ya wachezaji waliohama siku ya mwisho hadi 25 ukilinganisha na 17 mwaka jana.

Idadi hiyo ni ya juu zaidi tangu 2014 lakini jumla ya wachezaji waliohama kipindi chote ilishuka kwa mwaka wa tano mtawalia.

Kabla ya uhamisho huo wa dakika za mwisho, dalili zilikuwa zinaonesha pengine kungeshuhudiwa idadi ndogo zaidi ya wachezaji kuhama siku ya mwisho sokoni katika historia ya Ligi ya Premia.

Mtaalamu wa masuala ya fedha katika soka Rob Wilson kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam anasema: "Klabu ziliwekeza sana mwaka jana tuliposhuhudiwa kutumiwa kwa £1.5bn. Bila mkataba wa mafao kutoka kwa utangazaji wa mechi kwenye runinga ambao utaongeza mapato kwa klabu, ilitarajiwa klabu hazingetumia pesa nyingi sana.

"Isitoshe, bei kwa sasa ni za juu mno, na hilo limezuia baadhi ya klabu zisizo na uwezo mkubwa wa kifedha kununua. Manchester United, kwa mfano, hawajatumia pesa nyingi sana na kawaida wangelichangia kiasi cha jumla cha pesa zilizotumiwa. Nashuku kwamba ni kutokana na klabu nyingi kupandisha bei (Man United) moja ya klabu tajiri zaidi duniani ilipotaka kununua mchezaji ambapo United pengine waliamua tu kwamba hawatashikwa mateka."

Wilson anafikiri uhamisho wa Neymar wa £200m uliovunja rekodi ya dunia akitoka Barcelona kwenda Paris St-Germain mwaka jana umebadilisha mambo.

"Inaonekana bei ya wachezaji imepanda, hasa baada ya Philippe Coutinho kuhama kwa £140m+ kutoka kwa Liverpool kwenda Barcelona. Hii ina maana kwamba bei kimsingi imepanda maradufu kuliko ilivyotarajiwa kabla ya mkataba uliopita wa mafao ya runinga. Ni ishara ya wachezaji wachache kuhama lakini kwa bei ya juu."

Ongezeko la bei linadhihirika wazi ukilinganisha na ada ya awali ya uhamisho wa wachezaji 10 wa thamani ya juu zaidi kwa sasa walionunuliwa miaka ya nyuma na klabu ya Ligi ya Premia. Hakuna aliyekuwa amenunuliwa zaidi ya £13m.

Mada zinazohusiana