Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Liverpool v Real Madrid: Sergio Ramos amshutumu Jurgen Klopp

Sergio Ramos and Mohamed Salah Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Sergio Ramos aliwaongoza Real Madrid kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara ya nne katika miaka mitano

Nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos ameendeleza uhasama wake na klabu ya Liverpool uliozidishwa na kuumia kwa nyota wa Liverpool Mo Salah, wakati huu kwa kumshutumu meneja wao.

Ramos amemwambia Jurgen Klopp kwamba "baadhi yetu tumekuwa tukicheza soka katika kiwango cha hali ya juu sana kwa miaka mingi - Sina uhakika kama yeye mwenyewe anaweza kusema hivyo".

Klopp alimkosoa Ramos baada ya Mohammed Salah kuumia kwenye bega alipokabiliwa na beki huyo wa Real Madrid wakati wa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei.

Salah alilazimika kuondoka uwanjani kabla ya kumaliza hata kipindi cha kwanza.

Klopp alisema mchezaji huyo wa miaka 32 alikuwa "katili".

Lakini Ramos amesema: "Sina nia yoyote ya kumuumiza mchezaji makusudi."

Ameongeza: "Atakuwa anahitajika kueleza ni kwa nini hakushinda mechi hiyo ya fainali, lakini si mara yake ya kwanza kushindwa."

Klopp alishinda fainali yake ya kwanza ya michuano yoyote ile ya kiwango cha juu akiwa meneja mwaka 2012 katika Kombe la Ujerumani akiwa na Borussia Dortmund.

Lakini ameshindwa katika fainali sita alizozicheza karibuni zaidi - ikiwa ni pamoja na fainali hiyo ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid na fainali ya ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League, dhidi ya Sevilla mwaka 2016.

Salah alilazimika kufanyiwa upasuaji kwenye bega baada ya kuumia uwanjani mwezi Mei.

Wengi wa mashabiki wa Liverpool walimlaumu Ramos kwa jeraha hilo ingawa mchezaji huyo hakuadhibiwa na mwamuzi.

Ombi lilianzishwa mtandaoni likiwataka Fifa na Uefa kumwadhibu mchezaji huyo Mhispania.

Wakili mmoja nchini Misri pia aliwasilisha kesi ya kutaka Ramos atakiwe kulipa fidia ya £874m kwa madhara na hasara aliyowasababishia raia wa Misri "kimwili na kiakili."

Ramos pia aligongana na kipa wa Liverpool Loris Karius na inadaiwa kwamba huenda tukio hilo lilimduwaza kwa kumsababishia mtikisiko wa ubongo jambo ambalo pengine lilichangia makosa ya kushangaza aliyoyafanya kipa huyo.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Salah aliondolewa uwanjani kipindi cha kwanza baada ya kuumia

Klopp alikuwa pia amemlaumu kwa hilo.

Makosa yake mawili yalichangia mabao mawili ya Real Madrid ambao walishinda mechi hiyo iliyochezewa Kiev, Ukraine 3-1.

Akiongea Jumanne kabla ya mechi ya Super Cup ya Uefa dhidi ya Atletico Madrid mjini Tallinn leo Jumatano, Ramos amesema bado anamchukulia Klopp kama meneja wa ngazi ya juu.

"Tulipokuwa tunawapigia kura mameneja bora nilimpigia kura yeye, kwa hivyo anaweza kutulia," Ramos amesema.

'Salah anafaa kujilaumu mwenyewe'

Mwezi Juni, Ramos alikuwa pia amejitetea na kusema Salah anafaa kujilaumu mwenyewe.

Ramos amesema hatua ya Mohamed Salah kumshika mkono kwanza ndiyo iliyosababisha mchezaji huyo wa Liverpool kuumia wakati wa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

"Kitu pekee sijasikia ni Roberto Firmino akisema kwamba alipata mafua kwa sababu aliangukiwa na jasho langu," alisema Ramos kwa kutania.

Ramos pia alidai kwamba Salah angeendelea kucheza mechi hiyo "iwapo angedungwa sindano kipindi cha pili".

Ramos, 32, aliambia AS: "Upuuzi mtupu, wamemwangazia Salah sana. Sikutaka kuzungumza kwa sababu kila kitu kimeongezwa chumvi."

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kipa Loris Karius

"Nautazama mchezo vyema, anaushika mkono wangu kwanza na ninaanguka upande mmoja, na jeraha lilitokea kwenye mkono ule mwingine na wanasema kwamba nilishika mkono na kuukatalia kama mchezaji wa judo. Baada ya hapo, kipa wao anasema nilimduwaza kwa kumgonga."

"Niliwasiliana na Salah kupitia ujumbe, alikuwa vyema. Angeendelea kucheza iwapo angedungwa sindano kipindi cha pili. Nimefanya hivyo mara kadha lakini wakati ni Ramos alifanyajambo kama hilo, linakwamilia zaidi.

"Sijui kama ni kwa sababu umekuwa (nimekuwa) Madrid kwa muda mrefu na umeshinda kwa muda mrefu sana kiasi kwmaba watu hulitazama tofauti."