Donald Trump v John McCain: Uhasama wa kisiasa baina ya vigogo wa chama cha Republican waendelea hata baada ya mauti

Trump na McCAIN UHASAMA WAENDELEA

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Seneta wa Arizona John McCain atakumbukwa kwa kuwa mmoja wa wapinzania wakuu wa sera na mwenendo wa Rais Donald Trump.

Kitu kimoja, walau, kiliwaunganisha Bw John McCain na Rais Donald Trump, vigogo hao wawili ni wanachama wa chama cha kihafidhina cha Republican. Uhasama wao wa kisiasa ni mkubwa.

Bw McCain aliyefariki Jumamosi, alikuwa ni mpinzani mkuu wa Trump ndani ya Republican toka siku alipotangaza nia yake ya kugombea urais wa Marekani.

Kwa upande wake, Trump amekuwa akijibu mapigo kwa kukashifu rekodi ya McCain juu ya ushujaa wake na kukamatwa kwake mateka katika vita ya Vietnam.

Hata baada ya kifo cha McCain ambaye pia ni Seneta wa Arizona, bado Trump anaonekana hajasamehe yaliyopita baina yao.

Awali ilikuwa ni ujumbe wa twitter alioutuma Trump kufuatia kifo cha McCain, wakosoaji walishangazwa na Trump kutogusia heshima alojipatia marehemu kwa utumishi uliotukuka kwa taifa lake. Watangulizi wa Trump katika Ikulu ya White House, Barrack Obama na George W Bush wote walimmiminia sifa McCain kupitia Twitter.

Ni ada ya Wamarekani anapofariki mtu mwenye wadhfa mkubwa kama McCain basi bendera hupepea nusu mlingoti mpaka siku atakayozikwa.

Wakati majengo yote mengine ya serekali yakidumisha utamaduni huo, ajabu ikawa, Jumatatu ikiwa siku mbili tu baada ya McCain kufariki, bendera katika ikulu ya White House zikarudi kupepea katika urefu wa kawaida.

Kelele za upinzani zikapazwa, viongozi wa vyama vyote viwili vikuu vya Democrats na Republican pamoja na vyombo vya habari vikiitaka ikulu ya White House kumpa McCain heshima yake.

Baada ya kukwepa maswali ya waandishi juu ya sakata hilo la bendera, Trump akagiza bendera zote ndani ya ikulu zipepee tena nusu mlingoti mpaka baada ya mazishi.

"Licha ya tofauti zetu za kisera na kisiasa, namuheshimu Seneta John McCain kwa kwa utumishi wake kwa nchi yetu, na kwa heshima yake nimeagiza bendera ya Marekani ipepepee nusu mlingoti mpaka atakapozikwa," imeeleza sehemu ya taarifa ya Trump kwa vyombo vya habari.

Taarifa hiyo pia ilithibitisha pia kuwa Trump hatohudhuria mazishi ya McCain yatakayofanyika siku ya Jumamosi.

Lakini, uhasama wa wakubwa hao wawili wa chama cha Republican na siasa za Marekani kwa ujumla ulianzia wapi? Fuatilia matukio matano yaliyochagiza vigogo hao kufarikiana.

1. Trump 'ameamsha hasira za wehu'

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Trump alipiga kampeni kwa kuahidi kujenga ukuta mpakani na Mexico na kuwashutumu wahamiaji kutoka huko kuwa ni wahalifu.

Mwezi Juni 2015 Trump alianza mbio za kugombea tiketi ya kuania kiti cha urais kupitia chama cha Republican kwa kuwashutumu wahamiaji kutotoka Mexico.

"Wanaingiza (Marekani) mihadarati, wanaleta uhalifu, ni wabakaji, baadhi yao nadhani ni watu wema," alisema Trump na kualika juu yake upinzani wa hali juu kwa wakati huo. Ni kipindi hicho pia Trump alitangaza kujenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.

Seneta McCain ni moja ya waliopinga vikali tamko la Trump juu ya wahamiaji na kumtuhumu kwa "kuamsha hasira za wehu."

2. McCain sio shujaa wa vita

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Seneta McCain aliumizwa vibaya katika Vita ya Vietnam na alishikiliwa mateka kwa miaka mitano, hata hivyo Trump alitilia shaka ushujaa wake.

Seneta ndiye alikuwa wa kwanza kutuma shutuma, na Trump hakujivunga kumjibu.

Wiki chache tu baadae, akihutubia mkutano wa kampeni jimboni Iowa, Trump akamshusha hadhi McCain kwa kusema McCain sio shujaa wa vita.

"Sujaa kwa sababu alitekwa. Mimi nawapenda wale ambao hawakutekwa."

Seneta McCain alishikiliwa mateka katika vita ya Vietnam kwa miaka mitano unusu baada ya ndege vita aliyokuwa akiiendesha kutunguliwa.

Kauli ya Trump dhidi y McCain ilikashifiwa vikali na wagombea wenzake wa urais, japo aliifuta lakini hakuomba radhi kwa kile alichokisema.

McCain pia wale hakutaka aombwe radhi yeye bali familia za wale ambao walijotoa mhanga na kupigana vita.

Haikuishia hapo, McCain baadae aliwashutumu watu alosema walikuwa ni matajiri na waliweza kuepuka kwenda vitani kwa kupata madaktari "waliosema kuwa wana matatizo ya mifupa."

Trump aliweza kukwepa kuingia jeshini mara tano na kwenda kupigana Vietnam miaka ya 1960 - mara nne kwa sababu za kimasomo na mara moja kwa matatizo ya mifupa.

3. 'Trump hana kisingizio'

Baada ya Trump kufanikiwa kupata tiketi ya kugombea urais kupitia chama cha Republican, Seneta McCain alitangaza kumuunga mkono.

Hata hivyo, wiki chache kabla ya uchaguzi wa 2016, mkanda wa video ya Trump akitoa maneno ya udhalilishaji kwa wanawake mwaka 2005 ukaibuliwa. had blown away his challengers for the nomination, Mr McCain came behind the Republican.

"Ukiwa mtu maarufu unaweza kufanya lolote ulitakalo kwa wanawake," alisema Trump huku akijigamba namna gani alivyokuwa akilazimisha kuwabusu na kushika sehemu za siri za wanawake.

Mara tu mkanda huo ulipotoka, Seneta McCain akatangaza kusitisha kumuunga mkono Trump katika safari yake kuelekea uchaguzi na kusema yampasa awajibike kwa matamshi yake.

"Tabia ya Donald Trump inaniwia vigumu kuendelea kumuunga mkono katika kampeni zake," alisema Seneta, "hana kisingizio…Na yeye pekee ndio anawajibika kubeba mzigo wa mwenendo wake."

"Mwanamke yeyote hapaswi kudhalilishwa kwa kiwango cha namna hii."

4. Dole gumba la McCain lakwamisha mipango ya Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Seneta McCain alikuwa ni moja kati ya maseneta watatu wa chama cha Trump kupinga mabadiliko ya sheria ya Obamacare

Mfarakano baina ya wawili hao uliendelea hata baada ya Trump kuingia madarakani.

Moja ya ahadi zake alipokuwa akiwania urais ilikuwa ni kuondosha sheria ya matibabu kwa watu wenye kipato cha chini iliyoanzishwa na mtangulizi wake rais Obama maarufu kama Obamacare.

Mabadiliko ya sharia hiyo yakafika kwenye Bunge la Seneti, Republican wana viti 52 na Democrats 48. Walio wengi ndani ya Republicans waliungana mkono mabadiliko ya sharia hiyo.

Kura ilipopigwa, kama ilivyotarajiwa maseneta wote 48 wa Democrats wakaipinga. Ulipokuja upande wa Republicans, wengi wakikubali kasoro watatu ambao waliipinga.

McCain alivuta hisia za wengi kwa namna alivyopiga kura yake, tayari alishapatwa na maradhi ya saratani, hivyo hakutumia sauti yake, aliinua mkono wake wa kulia musawa wa kifua, kisha akakunja ngumi, akafyatua kidole gumba badala ya kukinanyua juu, akageuza mkono wake na kidole gumba chake kikainamia chini kuashiria anapingana na mapendekezo ya serikali ya Trump.

Mwisho waliopinga wakapata kura 51 na waliounga mkono wakapata kura 49.

"Hawana uthubutu wa kupigia kura mabadiliko haya," maneno ya Trump kwa maseneta wa chama chake waliopiga kura ya kupinga.

5. 'Rais wa Marekani hatakiwi kupongeza madikteta'

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Kwa mujibu wa McCain, mkutano wa Trump na Putin ulikuwa ni kosa kubwa kufanyika.

Bw McCain alikuwa mtu mashuhuri katika uga wa siasa za kimataifa na kufikia mpaka kuwa mwenyekiti wa kamati yenye nguvu ya seneti inayoshughulikia masuala ya silaha.

Alikuwa ni mhubiri mkubwa wa nafasi ya Marekani katika dunia. Hivyo haikushangaza kila alipomshutumu Trump kwa kumsifia rais wa Urusi Vladmir Putin.

Mwezi Machi Putin alishinda uchaguzi na kusalia madarakani, Trump akampongeza kwa ushindi.

"Rais wa Marekani haongozi Dunia Huru kwa kuwapongeza madikteta kwa kushinda chaguzi bandia," alisema McCain.

Na pale Trump alipokutana na Putin mwezi Julai, na kusema kuwa anakubaliana na kauli ya Putin kuwa Urusi haikuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016, McCain alioneshwa kukerwa zaidi.

Kwa mujibu wa seneta McCain mkutano huo ulikuwa ni "moja ya matukio ya aibu kabisa kufanywa na rais wa Marekani katika historia. "

"Hasara iliyosababishwa na jeuri ya Trump na kufumbia macho kwake wa watawla wa kiimla ni ngumu sana kuijumlisha," ilisema sehemu ya taarifa ya Seneta McCain. "Lakini ni Dhahiri kuwa kufanyika kwa mkutano wa Helsinki ilikuwa ni kosa kubwa."