Mchezaji bora wa Fifa: Je ni Cristiano Ronaldo, Luka Modric au Mohamed Salah?

Chanzo cha picha, Getty Images
Cristiano Ronaldo, Luka Modric na Mohamed Salah, ni nani aitabuka mshindi wa Fifa
Mchezaji bora wa kiume na yule wa kike wa tuzo ya Fifa watatangazwa katika tuzo za Fifa mjini London leo.
Cristiano Ronaldo, Luka Modric na Mohamed Salah ndio wachezaji watatu wa mwisho ambao watawania tuzo la mchezaji bora wa Fifa mwaka 2018.
Ada Hegerberg, Dzsenifer Marozsan na Marta ni miongoni mwa wale walioteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora mwanamke bora mwaka huu
Mshambuliaji wa Barcelona raia wa Argentina Lionel Messi, mshindi mara tano wa tuzo la Ballon d'Or amekosa kuorodheshwa katika tatu bora.
Pia hakuna mchezaji yeyote aliyekuwa kwenye kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia.
Wing'a mreno Ronaldo ambaye ni mshindi wa mwaka 2016 na 2017, alishinda kombe la tano la ligi ya mabingwa na Real Madrid mwezi Mei kabla ya kujiunga na Juventus kwa pauni milioni 99.2.
Kiungo wa kati wa Real Madrid Luka Modric alitajwa kuwa mchezaji bora kwenye Kombe la Dunia mwaka 2018 wakati Croatia ilifika fainali dhidi ya Ufaransa.
Mmisri Mo Salah alifunga mabao 44 huku Liverpooll ikifika fainali ya ligi ya mabingwa na kushindwa na Real Madrid.
Modric aliwashinda Ronaldo na Salah kwa kushinda tuzo la mwanamume bora wa mwaka wa Uefa wiki iliyopita.
Mshambuliaji wa England Harry Kane ambaye alishinda kiatu cha dhahabu kwenye Kombe la Dunia alikuwa kwenye orodha ya kumi bora lakini amekosa.
Didier Deschamps, ambaye aliiongoza Ufaransa, ameteuliwa kuwania tuzo la kocha wa mwaka, akiwemo raia wa Croatia Zlatko Dalic na meneja wa zamani wa Real Madrid Zinedine Zidane.
Tuzo hizo ni kando la Ballon d'Or, baada ya shirikisho la kandanda duniani kukata uhusiano wake na tuzo hilo mwaka 2016.
Jopo la wataalamu wa Fifa waliunda orodha ya wachezaji 10 kwa kila tuzo huku manahodha wa timu za taifa, waandishi wa habari na mashabiki wakimchagua mshindi kila kundi likiwa na asilimia 25 ya kura.
Washindi watatangazwa tarehe 24 Septemba huko Royal Festivan mjini London.