Leroy Sane aondoka katika hoteli ya timu ya taifa ya Ujerumani kwa sababu zisizojulikana

Leroy Sane dhidi ya N'golo Kante

Chanzo cha picha, Getty Images

Winga wa klabu ya Manchester City Leroy Sane ameondoka katika hoteli inayoishi timu ya Ujerumani kwa sababu za kibinafsi na hatoshiriki katika mechi ya kirafiki siku ya Jumapili dhidi ya Peru.

Sane mwenye umri wa miaka 22 aliwachwa nje katika kikosi cha Ujerumani cha kombe la dunia nchini Urusi.

Hatahivyo, alicheza kama mchezaji wa ziada katika mechi ya ligi ya kimataifa dhidi ya Ufaransa siku ya Alhamisi iliokamilika 0-0.

Ujerumani ilichapisha ujumbe wa twitter kwamba baada ya majadiliano na kocha mkuu Joachim Low, Leroy sane ameondoka katika hoteli ya Munich ambapo timu ya taifa hilo inapiga kambi kwa sababu za kibinafsi.

Mchezaji mwenza Toni Kroos alidai mapema wiki hii kwamba Sane ambaye ameichezea timu hiyo ya taifa mara 13 hajaonyesha uwezo wake na ni sharti abadilishe tabia yake.

''Mara nyengine mwili wake unakupatia hisia kana kwamba ni sawa tu iwapo tutashinda ama kupoteza'',Alisema kiiungo wa kati wa Real Madrid Kroos''.

''Ni mchezaji ambaye ana kila kitu unachohitaji kuwa mchezaji bora wa kimataifa lakini mara nyengine lazima umwambie aonyeshe kiwango cha mchezo wake.

Sane ambaye aligharimu £37m alipojiunga na Manchester City kutoka klabu ya Schalke mwezi Agosti 2016, hajaanzishwa hata mechi moja katika ligi ya Uingereza msimu huu.

Aliwachwa nje katika kikosi cha wachezaji 18 kwa mechi yao ya hivi majuzi ambapo walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Newcastle Septemba Mosi, ijapokuwa mkufunzi wake Pep Guardiola baadaye alikataa ripoti kwamba alikuwa hana raha na tabia ya mchezaji huyo.